Kocha Mkuu wa Yanga Miguel Gamondi amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya CBE SA yamekamilika na kazi iliyobaki ni kwa wachezaji kutimiza wajibu wao kuipeleka Yanga hatua ya makundi
Akizungumza katika mkutano na wanahabari mapema leo, Gamondi alisema katika kikosi chake ana wachezaji bora na wenye uzoefu mkubwa na kila mchezaji anafahamu umuhimu wa kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo
Gamondi amesema hataki kuwaweka kwenye presha wachezaji wake kutokana na kile kilichojitokeza katika mchezo uliopita ambapo walipoteza nafasi nyingi za wazi, lakini anatambua mchezo wa kesho watafanya kilichobora zaidi
"Mechi iliyopita kweli tulikosa nafasi nyingi. Lakini kama kocha kukosa nafasi hutokea, muhimu ni kuwa na timu yenye uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi"
"Ukweli ni kwamba lazima kesho tutumie nafasi tunazopata. Sitaki kuwapa wachezaji wangu presha kisa tulikosa nafasi nyingi, najua watacheza kwa utulivu lakini muhimu ni kuhakikisha tunatumia nafasi tunazopata"
"Hali ya wachezaji wangu ni nzuri, tumejiandaa vizuri sana na tumepata muda wa kujiandaa. Nina wachezaji wakubwa sana ambao wanaweza kufanya jambo bora kuliko wapinzani wetu, najua wachezaji wangu wanafahamu umuhimu wa kufuzu hatua ya makundi," alisema Gamondi
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, beki Ibrahim Bacca amesema kwake ni heshima kubwa kucheza mechi muhimu akiwa katika ardhi ya nyumbani
Bacca amesema wachezaji wana ari na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo
"Tunamshukuru Mungu asilimia kubwa wachezaji wote tupo salama. leo tunafanya mazoezi ya mwisho ni matumaini yetu tutamaliza salama, nina furaha kubwa sana mchezo huu kufanyika hapa Zanzibar nami nina matumaini makubwa kwenye mchezo huo"
"Hapo awali nilikuwa naangalia mpira wa ligi ya mabingwa kwenye TV, leo hii watu wanakuja kunitazama mimi. Nina farijika sana na kuona nina jukumu zito la kuhakikisha naisaidia Yanga kufikia malengo yake," alisema Bacca
Post a Comment