Yanga wameamua kurudi nyuma kwanza kuangalia kuna ulazima gani wa kusajili kiungo mkabaji mzawa ikiwa kuna uwezekano wa kuendelea kubaki na Jonas Mkude na Zawadi Mauya ambao watashirikiana vema na Khalid Aucho raia wa Uganda.
Wakakubaliana na wazo la Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kwamba wanaweza kusubiri dirisha kubwa lipite na kutumia kipindi hiki kutafuta mtu sahihi kabla ya kufika dirisha dogo, Desemba mwaka huu ambapo ndipo wafanye jambo.
Uamuzi huo wa Yanga umekuja baada ya hivi karibuni kuripotiwa kwamba walikuwa wamemfuata Yusuph Kagoma na kukubaliana baadhi ya mambo, lakini Simba wakachangamkia dili na kumchukua kiungo huyo mkabaji aliyetisha ndani ya Geita Gold na Singida Fountain Gate.
Yanga inasaka kiungo mkabaji mzawa ili kwenda kuchukua nafasi ya Zawadi Mauya ambaye mkataba wake kikosini hapo umemalizika baada ya msimu wa 2023-2024 kufikia tamati hivi karibuni, lakini sasa imebadili mawazo.
Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kimeliambia Mwanaspoti kwamba, viongozi wameanza harakati za kuzungumza na Mauya kwa ajili ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Mtoa taarifa huyo alibainisha kwamba, wanachotaka kufanya viongozi wa Yanga ni kwamba wakati ambao michuano ya msimu ujao 2024-2025 ikiwa inaendelea, taratibu watakuwa wakifuatilia wachezaji wa nafasi ya kiungo mkabaji mzawa na watakayeridhika naye watamsajili wakati wa dirisha dogo.
“Baada ya ishu ya Yusuph Kagoma kushindikana, imeonekana suala la kumpata kiungo mkabaji mzawa halitakiwi kufanyika kwa haraka kwani viongozi hawataki kumsajili mtu tu ilimradi kuziba nafasi, wanataka akisajiliwa mchezaji awe sahihi kuja kuisaidia timu.
“Kutokana na hilo, kuna uwezekano mkubwa wa Mauya kuendelea kuichezea Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya ule wa awali kumalizika,” kilisema chanzo hicho.
Mauya aliyejiunga na Yanga mwaka 2020 akitokea Kagera Sugar, Mei 2022 alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea timu hiyo ambao umemalizika mwishoni mwa msimu wa 2023-2024.
Mbali na Kagoma, Yanga pia ilitajwa kuwa kwenye mikakati ya kumsajili kiungo wa Azam FC, Adolf Mtasingwa Bitegeko ambaye mkataba wake kikosini hapo umebaki miezi sita, lakini kuna ugumu wanaweza kukutana nao kutokana na wamiliki wa mchezaji huyo kuwa tayari kumuongezea mkataba baada ya kazi nzuri aliyoifanya katika msimu wake wa kwanza klabuni hapo.
Hivi karibuni, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, alizungumzia ishu ya usajili ndani ya kikosi cha Yanga akisema: “Tunajukumu kubwa la kujenga timu yetu, tunaenda kujenga timu bora kuliko msimu huu, tunaenda kusaini wachezaji bora zaidi na wale ambao bado wanahitajika kwenye timu watabaki.”
Yanga imempa Gamondi mkataba mpya na moja ya malengo ni kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao au fainali kabisa na yeye amekiri.
BONYEZA HAPA KUANGALIA VIDEO ZA WAKUBWA UJIFUNZE MAUTUNDU YA KITANDANI
Post a Comment