Uongozi wa Singida Black Stars (zamani Ihefu) inadaiwa umeanza mazungumzo ya kumpata beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe kwa lengo la kuwaongezea nguvu kwa msimu ujao wa mashindano.
Kapombe aliyeichezea Simba kwa misimu saba mfululizo tangu aliposajiliwa 2017-2018 akitokea Azam FC sambamba na nahodha John Bocco, Erasto Nyoni na kipa Aishi Manula, ni mmoja ya wachezaji wanaodaiwa wanaweza kutemwa Msimbazi, licha ya kuwa na mkataba hadi Juni mwakani kutokana na fyagia fyagia iliyoanza kupitishwa Msimbazi.
Hatua ya nyota huyo kuhitajika na kikosi hicho inakuja muda mfupi baada ya kumtambulisha aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems atakayeinoa msimu ujao ambaye hapo awali ameshawahi kufanya kazi na beki huyo hodari alipokuwa Msimbazi kabla ya kwenda Kenya.
Kapombe (32) aliyejiunga na Simba Julai Mosi, 2017 akitokea Azam na amekuwa mmoja wa nguzo imara ya timu hiyo kwa safu ya ulinzi akishirikiana na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwa eneo hilo la pembeni.
Post a Comment