Staa wa Taifa Stars, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amewaambia mashabiki kwamba mechi ya leo jioni dhidi ya Zambia katika Uwanja wa Levy Mwanawasa nchini humu; “haina kujuana.”
Amesisitiza kwamba anaamini hakutakuwapo na mabadiliko ya kutisha sana kwenye kikosi cha Zambia na wao kama wachezaji wanajua pakuanzia na wameshaifanyia kazi kubwa mechi hiyo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
Staa wa Yanga, Mzambia Kennedy Musonda ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuanza leo saa 10:00 jioni ingawa Clatous Chama wa Simba hakuitwa kwenye mechi hiyo iliyobeba matumaini kwa timu zote mbili kukata tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026. Kundi hilo lina Morocco, Zambia, Tanzania, Niger na Congo na Eritrea walioondolewa.
Stars na Chipolopolo hazijawahi kufuzu michuano hiyo na sasa zinalingana alama katika kundi hilo, kila moja ikiwa na pointi tatu, ambapo Zambia imecheza mechi tatu ikipoteza mbili na kushinda moja huku Tanzania ikiwa imecheza mbili, imepoteza moja na kushinda moja.
Timu hizo tano zote zinawania nafasi moja ya juu ili kufuzu kucheza fainali hizo zitakazopigwa mwaka 2026 katika mataifa ya Canada, Mexico na Marekani. Ikumbukwe kuwa, katika makundi tisa yaliyopangwa, vinara watafuzu moja kwa moja, wakati washindi wanne bora ‘best loser’ watakaobaki watacheza kwa mfumo wa mtoano na mshindi atashiriki Mashindano ya FIFA Play-off kuwania nafasi ya kufuzu. Katika mechi nane za hivi karibuni timu hizo mbili zilipokutana rekodi zinaonyesha kutoshana nguvu ambapo kila timu imeshinda mara mbili, sare nne na kupoteza mbili. Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Januari mwaka huu kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika hatua ya makundi na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, ambapo Stars ilianza kufunga kupitia Saimon Msuva dakika ya 11 kabla ya Patson Daka kuisawazishia Zambia dakika ya 88.
Tanzania itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa imetoka kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Indonesia iliyomalizika kwa suluhu huku Zambia ikiwa imefungwa mabao 2-1 na Morocco.
Msuva na Daka ni wachezaji wanaotarajiwa kuzibeba timu zao leo kutokana na wasifu wa kila mmoja na kikosi kizima. Stars iliyoko Zambia imesheheni wachezaji wengi vijana tofauti na ile iliyocheza mechi ya mwisho dhidi ya Zambia kwani mastaa kama nahodha Mbwana Samatta, kipa Aishi Manula, Kibu Denis na Dickson Job sio sehemu ya kikosi hicho kilicho chini ya Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Msuva na Himid Mao wataiongoza Stars iliyo na nyota wengine kama Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.
Kwa upande wa Zambia kikosi chake hakijabadilika sana ila Watanzania wengi macho yao yatakuwa kwa Kennedy Musonda anayeichezea Yanga ambaye ni mchezaji pekee kutoka Ligi ya Tanzania aliyeitwa katika kikosi hicho baada ya Clatous Chama kuenguliwa.
Hata hivyo, Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Morocco alisema anawaamini wachezaji aliowaita kikosini hapo wanaweza kushinda mbele ya Zambia kama kila mmoja atatimiza vyema majukumu yake.
Morocco aliyekuwa kwenye benchi la ufundi kikosini hapo Januari mwaka huu wakati Stars ikitoa sare na Zambia alisema anawajua vyema wapinzani wao hao hivyo ana njia sahihi za kuwakabili.
“Tumejiandaa kushinda, ni mechi itakayotupa matumaini zaidi kama tutapata pointi tatu na naamini vijana wako tayari kulipambani hilo.
“Mara ya mwisho tulipokutana na Zambia tulitoa sare, hivyo wanatujua na tunawajua lakini hatutaingia kwa mazoea kwani mipango na maandalizi ni tofauti. Tunawaheshimu na tupo tayari kupambana nao,” alisema Morocco anayesaidiana na Juma Mgunda kukinoa kikosi cha Taifa Stars.
Kocha Avram Grant wa Zambia alisema ni mchezo muhimu kwao na lengo ni kushinda.
“Tumepoteza mechi iliyopita, hatutaki kupoteza tena na Tanzania. Tunajua umuhimu wa ushindi kwenye hatua hiii na lengo letu ni kushinda ili kuwa katika nafasi nzuri,” alisema Grant.
Kiungo wa Taifa Stars, Himid Mao alisema anaamini kila mchezaji kikosini anajua umuhimu wa mechi hiyo na yupo tayari kupambana kuhakikisha Stars inashinda.
“Awe mpya au mzoefu kikosini kila mmoja anajua nini tunatakiwa kufanya. Tunaamini kwa atakayepata nafasi kucheza atapambana kuhakikisha malengo yanatimia,” alisema Mao.
BONYEZA HAPA KUTAZAMA VIDEO ZA WAKUBWA UJIFUNZE MAUTUNDU YA CHUMBANI
Post a Comment