Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga pamoja na Simba wataanzia ugenini katika mashindano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, watakayoshiriki katika msimu mpya wa michuano hiyo.
Timu nyingine za Tanzania Bara zitakazoshiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ni Azam FC ambayo itapambana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Coastal Union iliyofuzu kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, Azam na Coastal Union, zenyewe zitaanza michuano hiyo kwenye hatua ya awali na mechi zao za kwanza zitachezwa nyumbani kati ya Agosti 16 na 18, mwaka huu.
Katika taarifa iliyotolewa na CAF, inasema klabu hizo mbili kutoka Tanzania, Yanga na Simba zitaanza kuwania ubingwa wa mashindano kuanzia raundi ya pili na mechi zao za kwanza zitachezwa ugenini na kumalizia nyumbani.
CAF katika taarifa yake imesema pia hatua ya awali ya mashindano hayo ya ngazi ya klabu kwa msimu wa 2024/2025 itaanza rasmi kufanyika kati ya Agosti 16 na 18, mwaka huu.
Shirikisho hilo pia limesema mechi za hatua ya makundi zitafanyika kati ya Oktoba na Desemba, mwaka huu huku michezo ya mtoano ya mashindano yote ikitarajiwa kuchezwa kati ya Machi na Mei, mwakani.
CAF pia imethibitisha nchi 12 ambazo zina pointi nyingi katika viwango vya ubora vitatoa timu mbili katika kila mashindano (mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika), ni pamoja na Algeria, Angola, Ivory Coast, Misri, Libya, Morocco, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Afrika Kusini, Sudan, Tunisia na Tanzania.
Wakati huo huo CAF pia imefungua ukurasa kwa nchi wanachama wake kuwasilisha majina ya timu zitakazoshiriki mashindano hayo Mfumo wa Mashindano wa shirikisho hilo (CMS).
Timu zitakazoshiriki mashindano hayo pia zitatakiwa kufuata kalenda ya usajili ambayo itaanza Julai Mosi hadi 20, mwaka huu kwa ajili ya wachezaji watakaocheza mechi za hatua ya awali wakati usajili utakaoanza Julai 21 hadi Agosti 31 utawahusu nyota watakaoshiriki mechi ya hatua ya pili.
Dirisha lingine la tatu litafunguliwa kuanzia Septemba Mosi hadi 30 na litawahusu wachezaji watakaoshiriki mechi za hatua ya makundi na timu zitakazosonga mbele katika michuano hiyo zitaruhusiwa kuongeza idadi ya wachezaji wasiozidi saba katika kipindi cha Januari Mosi hadi 31, mwakani.
Iliongeza hatua ya pili ya mashindano ya Kombe la Shirikisho imeondolewa wakati timu zitakazotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika hazitahamia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kama ilivyokuwa misimu iliyopita.
Hata hivyo kwa upande wa visiwani, bado haijajulikana itawakilishwa na timu zipi katika mashindano hayo ya CAF mpaka pale Ligi Kuu Zanzibar na mashindano ya Kombe la ZFF yatakapomalizika.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), limesema zimebaki raundi tatu ili kukamilisha kwa msimu wa 2023/2024.
Post a Comment