Klabu ya Simba iko kwenye mazungumzo ya kumpata aliyekuwa kiungo wa SC Villa Mganda, Kenneth Semakula ili kujiunga nao msimu ujao.
Uongozi wa Simba unaamini kiungo huyo wanaweza kumpata kwa gharama ndogo kwa sababu ni mchezaji ambaye yupo huru sokoni na wanamuona ataleta tija kikosini humo baada ya kutokuwa na matumaini na Msenegali, Babacar Sarr.
Kennedy kutua Coastal Union
WAGOSI wa Kaya, Coastal Union wameanza hesabu za kumnasa beki wa Simba, Kennedy Juma baada ya nyota huyo mkataba wake kumalizika msimu huu.
Hatua ya Coastal inatokana na kuondokewa na beki wa kikosi hicho, Lameck Lawi ambaye tayari msimu ujao atajiunga na Simba baada ya kufikia makubalino baina ya timu hizo na kusainishwa kandarasi ya miaka miwili.
Mkenya aingia rada za Ihefu
KLABU ya Ihefu, inawania saini ya kiungo mshambuliaji wa Gor Mahia, Austin Odhiambo kwa ajili ya kujiunga nayo msimu ujao.
Taarifa zinaeleza nyota wawili wa Kenya, Elvis Rupia na Duke Abuya ndio ambao wanatumika kama chambo cha kumshawishi kiungo huyo japo changamoto kubwa inayoweza kutokea ni kutokana na Gor Mahia kufuzu Ligi ya Mabingwa.
ERICK Johora haendi kokote
UONGOZI wa Mashujaa, umeanza mazungumzo ya kumpa mkataba mpya kipa wa timu hiyo, Erick Johora ili kuendelea naye msimu ujao.
Kipa huyo aliyejiunga na timu hiyo Januari mwaka huu akitokea Geita Gold, mkataba wake wa miezi sita umemalizika na yupo huru.
Awali, kipa huyo wa zamani wa Yanga, alipewa mkataba mpya ingawa aligoma kusaini kwanza.
Post a Comment