Uongozi wa Simba ya jijini Dar es Salaam umeanza vikao vya kufanya uamuzi kwa ajili ya kujenga kikosi imara kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mbalimbali watakayoshiriki, imefahamika.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya timu hiyo zimesema kikao hicho kitaanza na mchakato wa kuwaacha wachezaji ambao haiwahitaji kuelekea msimu ujao na kuwapa mikataba wote ambao wako kwenye mipango yao.
"Tutakuwa na kikao 'kizito' kwa ajili ya kuhakikisha mikakati ya usajili inakwenda vizuri, tunatarajia kufanya usajili wa kishindo utakaorudisha timu yetu kwenye makali yake," kilisema chanzo chetu.
Kiliongeza kuwa viongozi wa timu hiyo wameamua kuunganisha nguvu na ili kuhakikisha wanakamilisha vyema mipango ya usajili na programu ya mazoezi na mambo yote muhimu kwa ajili ya msimu ujao.
"Hata suala la usajili linajadiliwa kwa pamoja, tayari kuna mambo mengi mazuri yapo katika hatua ya utekelezaji, mashabiki na wanachama wa Simba wasubiri kuona mabadiliko katika timu," kiliongeza chanzo hicho.
Taarifa zaidi ziliongeza tayari ipo orodha ya wachezaji wanaowawinda na kilichobakia ni uamuzi wa mwisho ambao utafanyika kwa kufuata mapendekezo yaliyotolewa na benchi la ufundi.
"Wapo wachezaji ambao ki ukweli wamepoteza sifa ya kuendelea kuwa katika kikosi cha Simba, matokeo ambayo tumeyapata msimu huu yametuumiza sana, tunataka kujenga kikosi kipya, imara ambayo kitarudisha heshima yetu.
Simba itafanya maboresho ya kikosi katika maeneo mengi ambayo yatapelekea kuwa na kikosi kipana na timu 'iliyobalansi," aliongeza.
Pia kikao hicho kinatarajia kupendekeza mahali ambayo kikosi chao kitaenda kuweka kambi.
"Usajili utafanyika kwa nafasi nyingi, safu ya ulinzi itaongezewa watu, kiungo na ushambuliaji pia, Simba ya msimu ujao itakuwa ya tofauti sana, kwa kifupi tunataka kudumisha umoja wetu ambao utasaidia kufikia malengo, viongozi wakiwa pamoja hakuna tutakapofeli," alisema mtoa habari huyo.
Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kila kitu kinachofanywa na klabu hiyo kitawekwa hadharani ili mashabiki na wanachama watafahamu muda wake sahihi utakapofika.
"Kwa sasa sina la kusema, lakini muda ukifika kila kitu kitafahamika, tunafahamu Wana-Simba wanashauku ya kujua nini kitafanyika," alisema Ahmed.
Mbali na Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Fa, Simba itajiandaa kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa Yanga na Azam FC.
Post a Comment