Duru za kispoti zimeliambia Mwanaspoti kwamba kuna fagio la chuma litaanza kupita Simba na Yanga kwenye kipindi kisichozidi wiki moja kuanzia leo. Ni fagio ambalo huenda likawa na sapraizi ambazo huenda zikaacha mijadala kwenye vijiwe vya kahawa.
Lakini za ndaani kabisa ni kwamba hilo lazima lifanyike ili mabadiliko yaonekane kwenye pichi msimu ujao wa kimashindano kwa Simba na Yanga.
Kitendo cha Simba kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara 2023-24 na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao kimewakera. Lakini kinachowaumiza kichwa zaidi kwamba kule Shirikisho lazima wafuzu kwanza hatua ya fainali ili kupunguza kejeli za mtani wao.
Hali hiyo inawafanya Simba kupitisha fagio la chuma kwenye chumba cha kubadilishia ili kubakiwa na sura chache na kuingiza vyuma visivyopungua tisa vilivyoko tayari kwa kazi ngumu ingawa kumekuwa na kelele mitandao pia zikiwashinikiza viongozi kukaa pembeni. Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba katika kikosi cha Simba chenye wachezaji 30, nusu yake wanakwenda na maji. Yanga wao watapukutisha wasiozidi watano wa kigeni;
WANAOONDOKA
Aishi Manula
Anahusishwa sana na kurejea Azam klabu iliyomuuza Simba.Inaelezwa amewaambia viongozi na asilimia kubwa wameridhia kwavile hali yake ya majeruhi bado haiwapi matumaini kwamba anaweza kurejea kwenye ubora wake.
Manula ambaye amejenga ufalme mkubwa katika goli la Simba akidaka kwa mafanikio, msimu huu uliomalizika kwake haukuwa mzuri sana kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu ambayo yanatarajiwa kumuweka nje ya uwanja hadi Oktoba mwaka huu.
Ayoub Lakred
Alisaini mkataba wa mwaka mmoja. Na ndiyo roho ya Simba kwa sasa, lakini kuna viongozi wameanza kujiandaa kisaikolojia baada ya kusikia kwamba anaweza kuibukia Wydad Casablanca ya kwao Morocco. Tayari wameanza mazungumzo na Mgaboni, Loic Owono na Mkongo, Ley Matampi wa Coastal Union kuchukua nafasi hii.
Kennedy Juma
Huenda akapewa baraka za kujiunga na Ihefu. Hali yake ya kutojiamini na kufanya makosa katika mechi za hivikaribuni kumepunguza imani yake kwa viongozi na wameingia sokoni kusaka mtu. Alijiunga nayo Julai 2019 akitokea Singida United.
Henock Inonga
Mkataba wake na Simba umebaki mwaka mmoja hadi 2025, raia huyu wa DR Congo ameonyesha nia ya kuondoka na viongozi wa Simba wamebainisha kwamba wapo tayari kumuuza kwa timu itakayowasilisha rasmi ofa yao, hivyo suala lake la kubaki ndani ya Simba ni dogo sana huku kuondoka kukiwa ni asilimia kubwa.
Inonga alijiunga na Simba Agosti 2021 akitokea DC Motema Pembe ya DR Congo. Juni 2025 ndiyo mkataba unamalizika.
Shomari Kapombe
Anaachwa kwa heshima. Sababu mbili zinatajwa umri pamoja na majeraha ya mara kwa mara ambayo humuweka nje kwa muda mrefu. Kapombe kwa sasa ana miaka 32.
Ameitumikia timu hiyo kuanzia 2017 hadi sasa 2024 alipojiunga nayo akitokea Azam. Kabla ya hapo, Kapombe aliichezea 2011 mpaka 2013.
Fabrice Ngoma
Aliweka bayana anaondoka Simba mwishoni mwa msimu huu akiwa ameitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja pekee baada ya kujiunga nayo Julai 2023 huku mkataba wake ukimalizika Juni 2025. Ngoma raia wa DR Congo, alitua Simba akitokea Al-Hilal.
Katika eneo la kiungo la Simba, msimu huu Ngoma amekuwa mchezaji muhimu, lakini mwenyewe ameamua kuondoka kutokana na kuhitaji kwenda kwenye timu ya nje ya Tanzania yenye ushindani zaidi ya alipo sasa.
Babacar Sarr
Januari 2024 alijiunga na Simba, lakini katika kipindi cha takribani miezi mitano aliyokuwa hapo ameshindwa kuonyesha kile kilichotarajiwa.
Sarr raia wa Senegal, alitarajiwa kuwa kiungo mkabaji wa shoka ndani ya Simba, lakini ameshindwa kufanya hivyo jambo linalowafanya mabosi wa timu hiyo kumuweka kwenye listi ya wanaoachwa.
Saido Ntibazonkiza
Wapo wanaosema kiungo huyu raia wa Burundi abaki, wengine wanataka aondoke lakini asilimia kubwa yupo kwenye kundi la wanaoondoka.
Saido msimu huu amemaliza kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Simba katika michuano ya ligi kuu akifunga mabao 11, msimu uliopita alikuwa kinara wa mabao pia katika ligi kwa ujumla akifunga 17 sawa na Fiston Mayele aliyekuwa Yanga.
Wanaotaka Saido aondoke wanasema umri umemtupa mkono kwani hivi sasa ana miaka 37, lakini pia mabao yake asilimia kubwa anayafunga kwa penalti, machache sana ya kawaida. Katika mabao yake 11 msimu huu, sita amefunga kwa penalti kati ya saba alizopiga.
Wale wanaosema abaki, wanaangalia namba zake zinambeba kwani ndiye mchezaji mwenye mchango mkubwa wa kufunga mabao kuliko wachezaji wengine katika misimu ya karibuni ambayo Simba imekuwa ikisuasua katika ligi.
Clatous Chama
Anadengua lakini za ndani zinadai kwamba Simba hawako tayari kumbembeleza. Anataka dau kubwa akiwatishia kwenda Yanga ingawa viongozi wanadai ni geresha ya kuongeza dau. Kuna uwezekano mkubwa wakamuachia aondoke kama ataendelea kususia mkataba akishinikiza mambo makubwa ambayo wanadai hayaendani na ubora wake wa sasa.
Abdallah Hamis
Anaachwa. Ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza. Katika eneo la kiungo analocheza amekutana na watu wa shoka wanaomuweka benchi, hivyo suala la kubaki ndani ya Simba kwake ni dogo kwa mujibu wa viongozi. Anaondoka.
Willy Onana
Anashinikiza kuondoka lakini viongozi wanamshawishi abaki.Mkataba wa mwaka mmoja umebaki kati ya ile miwili aliyosaini msimu huu akitokea Rayon Sports ya Rwanda. Nyota huyu raia wa Cameroon mwenyewe anataka kuondoka huku Simba ikiwa tayari kumuuza ambapo Klabu ya Super Sport ya Afrika Kusini inaelezwa kumtaka.
Aubin Kramo
Msimu huu hajacheza mechi ya kimashindano, muda mwingi amekuwa nje akiuguza majeraha, hivyo amewekwa kwenye kundi la wanaoondoka. Ingawa baadhi ya viongozi wamempa masharti ya kupunguziwa dau ili abaki aonyeshe alichonacho.
Luis Miquissone
Wanamuondoa. Gharama kubwa zinazotumika na klabu kwake haziendani na uhalisia wa uwanjani. Viongozi wanadai si Luis yule. Kiwango chake kwa sasa kimeshuka hivyo anasubiri muda ufike apewe mkono wa kwaheri kwani hata alipopewa nafasi ya kucheza ameshindwa kudhihirisha uwezo wake.
John Bocco
Alijiweka pembeni mwenyewe. Anaingia kwenye kundi la wachezaji wenye heshima ndani ya Simba, baada ya msimu wa ligi kumalizika aliaga hivyo msimu ujao hatakuwa mchezaji wa timu hiyo na badala yake amejikita katika ukocha akipewa nafasi ya kuinoa timu ya vijana ya Simba.
Pa Omar Jobe
Huyu nae ameshindwa kazi, wanamtoa kuingiza mbadala wenye nguvu zaidi. Amefunga bao moja pekee katika miezi mitano aliyokuwa Simba kwani aliingia kipindi cha dirisha dogo msimu huu. Ameshindwa kuonyesha ubora wake.
WANAOBAKI
Hussein Abel
Kipa ambaye amepata muda mchache wa kucheza lakini kila alipopewa nafasi ameonyesha uwezo wake, bado ana nafasi ya kuendelea kuwepo Simba kwa msimu ujao ukiwa ni wa pili kwake kikosini hapo.
Ally Salim
Kipindi ambacho makipa namba moja na namba mbili walipokosekana, golini alikaa yeye na kuifanya kazi kwa ufasaha. Anakumbukwa kwa kuiwezesha Simba kubeba Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu alipowazuia baadhi ya mastaa wa Yanga kumfunga katika mikwaju ya penalti ambayo aliiokoa. Bado ana nafasi ya kuendelea kuwepo Simba akiwa bado ana umri mdogo.
Ahmed Ferouz
Ni kipa aliyepandishwa kutoka timu ya vijana, bado ana muda wa kuendelea kujifunza zaidi, kama akiondolewa basi atatolewa kwa mkopo kwenda kujiimarisha zaidi.
Che Malone Fondoh
Katika safu ya ulinzi ya Simba, beki huyu raia wa Cameroon amekuwa mtu muhimu sana. Amekuwa akitengeneza ushirikiano mzuri na Inonga, hata alipopangwa kucheza na Kennedy Juma, bado alibaki kuwa imara ingawa tatizo kubwa amekuwa na makosa ya hapa na pale, akijirekebisha atakuwa bora zaidi.
Mohamed Hussein
Nahodha msaidizi wa Simba akicheza beki wa kushoto tangu mwaka 2015. Katika nafasi hiyo wamekuja walinzi tofauti lakini wameshindwa kuuondoa ufalme wake, hivyo ataendelea kubaki Simba lakini anahitaji kutafutiwa msaidizi sahihi.
Hussein Kazi
Huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya Simba, alipewa nafasi ya kucheza na kuonyesha ana kitu, hivyo ataendelea kubaki na kama kuna wazo la kumtoa basi itakuwa kwa mkopo kwenda kuwa imara zaidi kabla ya kurejea kundini.
Israel Mwenda
Hesabu zilizopo ni Mwenda kurithi moja kwa moja mikoba ya Kapombe aliye kwenye rada za kuondolewa ndani ya Simba. Mwenda pia ana uwezo wa kucheza beki wa kushoto ingawa kiuhalisia ni beki wa kulia. Bado umri wake ni mdogo na akitumika vizuri atakuwa msaada mkubwa kwa Simba.
David Kameta
Anajulikana kama Duchu, msimu huu amerejea Simba lakini bado ameendelea kusubiri mbele ya Kapombe na Mwenda, amepata muda mchache wa kucheza ingawa bado akipewa nafasi anafanya vizuri. Ataendelea kuwepo lakini anaweza kutolewa kwa mkopo.
Sadio Kanoute
Kiungo mkabaji mwenye uwezo mkubwa wa kuifanya kazi yake kwa ufasaha. Mbali na uwezo wa kukaba, pia anajua kufunga, Simba haipo tayari kumuachia kiungo huyo raia wa Mali. Alitua Simba
Agosti 2021, mkataba wake unaisha Juni 2024, hivyo yupo kwenye mazungumzo ya kuongezewa mkataba.
Mzamiru Yassin Kati ya viungo ambao hawatajwi sana lakini wanafanya kazi kubwa ndani ya Simba ni huyu aliyekuwa hapo tangu 2016 akitokea Mtibwa Sugar. Azam wamekuwa wakimpigia hesabu za kumsajili, lakini Simba wameamua kubaki na kiungo wao huyo.
Edwin Balua Ana msimu miezi mitano tu ndani ya Simba akitua hapo akitokea Tanzania Prisons katika kipindi cha dirisha dogo. Mechi za mwishoni alionyesha uwezo wake baada ya kupewa nafasi kubwa ya kucheza. Ataendelea kubaki Simba.
Ladaki Chasambi Huyu naye alitua Simba dirisha dogo akitokea Mtibwa Sugar, naye hakuwa akipata nafasi kubwa ya kucheza hapo awali, lakini tangu Juma Mgunda amekabidhiwa Simba katika mechi tisa za mwisho, ameonyesha ana kitu, anabaki msimu ujao kudhihirisha zaidi.
Saleh Karabaka Katika usajili wa dirisha dogo naye aliingia nyota huyu kutoka JKU ya Zanzibar. Alianza na moto na kila alipopewa nafasi alionyesha kitu. Ataendelea kuwepo.
Kibu Denis Alikuwa kwenye mvutano wa kuongeza mkataba baada ya Yanga kumfuata kuhitaji saini yake, lakini mwisho wa siku akaamua kubaki Simba kwa kusaini mkataba mwingine.
Freddy Michael Katika washambuliaji walioingia dirisha dogo ndani ya Simba na kufanya vizuri, Freddy ni namba moja kwani amemfunika Pa Omar Jobe aliyeingia naye.
Freddy raia wa Ivory Coast, alianza kidogokidogo, lakini katika miezi mitano, amefanikiwa kufunga mabao sita ndani ya ligi jambo lililowafanya viongozi wa Simba kufikiria tena kuendelea kumpa nafasi kwa msimu ujao kwani hapo awali kabla hajachanganya walitaka kumuacha.
YANGA IPO HIVI Wakati Simba wakiwa na mpango wa kuachana na nyota wengi zaidi, Yanga kwao ni tofauti. Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara msimu huu wakibeba kwa misimu mitatu mfululizo, wana mpango wa kufanya maboresho kidogo tu ya kikosi chao, hawataki kukifumua zaidi kwani wanaona wakifanya hivyo wataharibu mipango yao ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Yanga chini ya Kocha Miguel Gamondi, mpaka sasa mipango iliyopo ni kuachana na wachezaji watatu wa kimataifa ambao ni Augustine Okrah, Joyce Lomalisa na Skudu Makudubela. Kumbuka msimu uliopita ulipomalizika iliachana na wachezaji 10, kisha ikasajili saba.
Msimu huu kwa wale inaotaka kuachana nao, kila mmoja ana sababu yake ya kuachwa lakini kubwa zaidi ni mchango mdogo kwa timu, hii inawahusu Skudu na Okrah, lakini Lomalisa mkataba unaisha na tayari mbadala wake ametafutwa.
Hivi sasa Yanga ipo kwenye mazungumzo na Chadrack Boka kutoka FC Lupopo ya DR Congo ili kuja kuchukua nafasi ya Lomalisa. Ujio wa Boka unamaanisha kwamba beki huyo raia wa DR Congo anakwenda kushirikiana na Nickson Kibabage.
Okrah Raia wa Ghana ambaye alijiunga na Yanga katika dirisha dogo msimu huu akitokea Bechem United, hajaonyesha kile kiwango kilichotarajiwa hivyo mpango wa kumtafuta kiungo mwingine wa kucheza nafasi yake umeanza na jina la Clatous Chama kutoka Simba likitajwa.
Skudu Alitua Yanga mwanzoni mwa msimu huu akitokea Marumo Gallants ya kwao Afrika Kusini, hajaonyesha kiwango bora na mbadala wake anatajawa kutokea TP Mazembe ya DR Congo baada ya Yanga kuanza mchakato wa kumsajili Philip Kinzumbi. Mshtuko mkubwa uliopo ndani ya Yanga ni namna ya kiwango cha Joseph Guede alichokionyesha miezi michache iliyopita baada ya kutua hapo dirisha dogo msimu huu.
Guede Alianza taratibu, lakini alivyochanganya mashabiki wa Yanga wamenyoosha mikono juu na kusema “Huyu jamaa anajua, anahitaji muda zaidi kuonyesha uwezo wake.”
Mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast, amefunga mabao sita katika ligi akitua Yanga dirisha dogo msimu huu. Lakini bado anaendelea kuangaliwa muendelezo wa kiwango chake huku mipango ya kuongezewa nguvu ikiwepo.
Kule kwenye safu ya ulinzi, Bakari Mwamnyeto kwa sasa ameshuka kiwango huku akifanya makosa yanayoigharimu timu ikiwemo ile mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Tanzania Prisons, bao la wapinzani lilitokana na makosa yake.
Mwamnyeto licha ya hayo, lakini bado Yanga wanaamini kitafika kipindi atakuwa sawa kama hapo awali, hivyo wanaendelea kubaki naye huku wakimtumia Gift Fred kama mbadala wake ndiyo maana hawataki kumuachia Fred.
Fred amejiunga na Yanga msimu huu akitokea kwao Uganda, anatajwa kuwa mzuri katika kuanzisha mashambulizi kitu ambacho mabeki wengi wa kati kinawabeba kwenye soka la kisasa. Yanga hawataki kumpoteza.
KAULI ZA VIONGOZI Rais wa Yanga, Mhandishi Hersi Said, hivi karibuni alizungumzia ishu ya kuijenga Yanga ya msimu ujao akibainisha kwamba watasajili wachezaji bora zaidi ya wale waliopo msimu huu. “Tuna jukumu kubwa la kujenga timu yetu, tunaenda kujenga timu bora kuliko msimu huu, tunaenda kusaini wachezaji bora zaidi,” alisema Hersi.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema atawasilisha ripoti kwa Bodi ya Wakurugenzi kuainisha nini kifanyike ili kuijenga timu imara zaidi kwa msimu ujao huku akiweka wazi kwamba usajili unaokwenda kufanyika utagusa maeneo mengi kulingana na kile alichobaini muda mfupi aliokaa na kikosi hicho.
“Unakuja usajili mpya na msimu mpya hivyo lazima vitu vipya viwepo. Kuna vitu ambavyo tumeviona tangu ligi imeanza hadi mwisho.
"Nikuhakikishie tu kwamba lazima kuna mambo yatafanyiwa mabadiliko. Nitawasilisha katika bodi mambo ambayo yatatakiwa kufanyika ili msimu ujao Simba ifanye vizuri zaidi,” alisema Mgunda.
Post a Comment