Kwa mara ya kwanza baada ya misimu saba, Simba SC inamaliza Ligi Kuu nje ya nafasi mbili za juu. Mara ya mwisho kwao kumaliza katika nafasi kama hii ilikuwa msimu wa 2015/16 walipomalinza nyuma ya hawa hawa, Yanga na Azam FC.
Na wakati huo ilikuwa kabla ya ujio wa mwekezaji Mo...ulikuwa wakati wa vibakuli huku kikosi chao kikiundwa na chipukizi wengi kutoka timu yao ya vijana.
Misimu miwili baadaye mwekezaji Mo Dewji akashuka Msimbazi na upepo ukabadilika. Simba ikatoka kuwa timu ya kuishi kwa kutegemea vibakuli kuombaomba fedha na kuwa timu ya kitajiri.
Mnyama akajenga kikosi cha hatari kilichotawala soka la Tanzania na kushinda kila taji la ndani na kujenga heshima Afrika.
Ni Simba hii iliyofuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara nne na mara moja robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF katika miaka hii sita.
Na ni mafanikio haya ndio yaliifanya Simba hii ikapata nafasi ya kushiriki mashindano mapya ya African Football League, na kuipatia Tanzania nafasi nne mwenye mashindano ya klabu barani Afrika.
Lakini wakati wote wa mafanikio haya, kulikuwa na upinzani mkali kutoka kwa watu wawili wenye jina moja la HAMIS, ambao walikuwa wakikosoa vikali mchakato uliomleta mwekezaji na tabia yake ya kutofuata taratibu.
Mwenyekiti wa klabu kutoka upande wa wanachama, Said Mkwabi, akajiuzulu akitoa sababu zilizohalalisha malalamiko ya kina HAMIS wale wawili.
Na kina HAMIS wenyewe siyo wengine bali ni Hamis Kilomoni na Hamis Kigwangalla.
HAMIS KILOMONI
Bahati mbaya sana rekodi rasmi za mpira wetu zinaanzia mwaka 1965 ilipoanza ligi rasmi ya kitaifa. Lakini kabla ya ligi hii kulikuwa na ligi ya mkoa wa Dar es Salaam ambayo ndiyo ya kwanza nchini, iliyoanza 1921.
Mwaka 1964, Hamis Kilomoni akiwa mchezaji wa Sunderland ambayo 1972 ilibadilika na kuwa Simba, alifunga mabao matatu peke yake dhidi ya Yanga, kwenye Ligi ya Dar es Salaam.
Lakini ndiyo kama hivyo tena, rekodi za mashindano yale zilifutwa na rekodi pekee zilizopo ni zile zinazoanza 1965, ilipoanza ligi ya taifa.
Wakati ligi ya taifa inaanza 1965, Hamis Kilomoni alikuwa ndiyo ametoka kustaafu mpira na kuwa katibu mkuu msaidizi wa Sunderland.
Kisa cha kustaafu ghafla ilhali akiwa na uwezo mkubwa akitegemewa na klabu yake na timu ya taifa, ni kuondoka kwa katibu mkuu aliyekuwa mfanyakazi wa serikali.
Katibu huyu alihamishiwa mkoani kikazi, kwa hiyo isingewezekana kutimiza majukumu yake klabuni akiwa mbali na ofisi za klabu, hasa katika zama zile za giza.
Ikabidi nahodha Hamis Kilomoni astaafu ili aokoe jahazi...ndiyo akawa katibu msaidizi. Katika nafasi hiyo, Kilomoni akaja na wazo la kutafuta eneo lao wenyewe ili wajenge ofisi za makao mkuu ya klabu.
Hii ni kwa sababu kabla ya hapo klabu haikuwa na ofisi ya kudumu bali ilihama mtaa hadi mtaa kwa sababu ya changamoto ya nyumba za kupanga.
Ndipo Sunderland ikapata eneo pale Msimbazi na kujenga ofisi zao zinazotumika hadi sasa.
Hamis Kilomoni ndiyo alikuwa mtu wa kwanza kutilia shaka mchakato wa kumpata mwekezaji na alipambana sana kuhakikisha mambo yanakwenda kwa kufuata taratibu rasmi...lakini alipuuzwa.
Hamis huyu ambaye wakati fulani alikuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini ya klabu, alivuliwa nafasi yake na kuonekana msaliti dhidi ya ‘maendeleo’ ya klabu yao.
HAMIS KIGWANGALLA
Mwanasiasa na mfanyabiashara mashuhuri ambaye ni shabiki mkubwa sana wa Simba. Kupitia mitandao ya kijamii, Hamis huyu amekuwa mkosoaji mkuu wa mfumo uliomleta mwekezaji Mo klabuni Simba.
Amekuwa ‘akipiga spana’ mara kwa mara na kuchafua hali ya hewa kiasi cha ule upande wa mwekezaji kununa. Kuna wakati baada ya spana kuuma, mwekezaji mwenyewe akasimama hadharani na kudai kwamba spana zile zilikuwa chuki binafsi za bwana Hamis kwa sababu ya kunyimwa mkopo wa pikipiki.
Tofauti na Hamis Kilomoni, Hamis Kigwangalla hajawahi kupoa hata mara moja. Mara zote amekuwa akituma mashambulizi mazito kwa mwekezaji na mfumo wake.
Lakini mara zote kina Hamis hawa hawakusikilizwa kwa sababu matokeo yalikuwa yakipatikana pale Msimbazi, na shabiki wa kawaida hana anachokitaka zaidi ya matokeo.
Lakini sasa baada ya matokeo kukataa, kina Hamis hawa wamegeuka kuwa manabii walioona kesho tangu juzi.
Na baada ya hali ya hewa kuchafuka Msimbazi kiasi cha wajumbe wa bodi kutoka upande wa mwekezaji kujiuzulu na kuwaacha wale wa upande wa wanachama wakirusha makombora, kina Hamis wamegeuka mashujaa.
Yote kwa yote, hali sio nzuri klabuni Simba na hili silo jambo la kufurahia. Kuyumba kwa Simba ni kuyumba kwa mpira wa Tanzania kwa sababu klabu hii inabeba dhamana inayokaribia nusu ya mpira wa nchi hii.
Tuombee mgogoro huu upite salama na Simba irudi kuwa moja kwa faida ya mpira wetu. Wale wole wanaohusika mwenye mgogoro juu, wakumbuke kuwa wanachogombea ni fito za kujenga nyumba moja... wasizivunje!
BONYEZA HAPA KUTAZAMA VIDEO ZA WAKUBWA UJIFUNZE MAUTUNDU YA CHUMBANI
Post a Comment