Klabu ya Supersport United ya Afrika Kusini, inawania saini ya nyota wa Simba, Willy Essomba Onana kwa ajili ya msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zimeliambia Mwanaspoti kwamba nyota huyo raia wa Cameroon yuko tayari kuondoka katika timu hiyo baada tu ya msimu huu kumalizika licha ya kubakisha mkataba wake wa mwaka mmoja na kikosi hicho unaoisha mwakani.
Mmoja wa kiongozi wa Simba ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini aliliambia Mwanaspoti, timu hiyo ya Supersport United imefanya mawasiliano ya kumuhitaji nyota huyo huku wakiweka kiasi cha R2 milioni ambazo ni sawa na Sh280 milioni.
“Ni kweli jamaa wameonyesha nia ya kumuhitaji na kiasi ambacho wameweka uongozi unaona ni kikubwa na bora wakichukue kwa sababu mchezaji ameshindwa kuonyesha imani tuliyokuwa nayo japo, bado uamuzi ya mwisho hayajafanyika,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alinukuliwa na gazeti hili akieleza mchezaji yeyote waliye na mipango naye kwa ajili ya msimu ujao watahakikisha wanambakisha ili kutengeneza timu imara na ya ushindani.
Onana aliyefunga mabao manne katika Ligi Kuu Bara msimu huu, alijiunga na Simba Julai 5, mwaka jana akitokea Rayon Sports ya Rwanda ambapo kabla ya kutua ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi alikuwa ni mchezaji bora wa Ligi (MVP).
Mbali na kuibuka MVP akiwa na Rayon Sports, nyota huyo alikuwa pia mshambuliaji bora wa msimu ambapo alifunga mabao 16 na kuchangia mengine matano (asisti), akiwa na uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani kuanzia wingi zote mbili.
Ukiacha na kumudu vyema nafasi ya wingi ya kushoto na kulia anaweza kucheza nyuma ya mshambuliaji au mshambuliaji kivuli yaani (false number nine).
Post a Comment