NI kweli bado halijakamilika. Hata hivyo, sio ajabu kusikia kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama amemwaga wino Yanga, kwani dili la kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania lipo pazuri na hasa baada ya mabosi wa Msimbazi kushindwa kumtekelezea mahitaji aliyowasilisha mezani ili asalie kikosini.
Ipo hivi. Wakati wowote Mzambia huyo dili la kwenda Yanga linaweza kukamilika baada ya mazungumzo kati yake na mabosi wa Wekundu wa Msimbazi kuingia utata.
Utata ambao umeibuka ni baada ya mabosi wa Simba kugomea kumuongezea ada ya usajili (sign on fee) ambayo kiungo huyo alikuwa anaitaka ili asaini mkataba wa kuendelea kusalia katika timu hiyo.
Simba ni kama imeingia nyongo na Chama ambapo baadhi ya mabosi ndani ya klabu hiyo wakiona Mzambia huyo bado anahitajika, huku kundi lingine lenye nguvu likiona ni bora watengeneze timu mpya itakayokuwa bila ya mchezaji huyo.
Hatua ya pili ambayo Chama na Simba inabishana ni juu ya mshahara ambao anautaka ambao ni sawa au zaidi na ule anaolipwa sasa winga Luis Miquissone.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, mabosi wa Simba na Chama wameshindwa kuafikiana kwenye dau hilo la mshahara, kwani Mzambia huyo ametaka kulipwa Dola 25,000.
Kwa sasa inadaiwa, Luis ambaye hana namba katika kikosi cha kwanza au kupata nafasi ya kutumika mara kwa mara kikosini, analipwa na Simba zaidi ya Dola 20,000 kwa mwezi, mshahara ambao Chama ametaka zaidi ya kiwango hicho ili asaini mkataba mpya na mabosi wa Simba wanaona ni vigumu kumkubalia.
Hatua ya mwisho kwa Simba ni kama kundi linalotaka Chama aachwe linaelekea kushinda kwa vile wao ndio wanaotoa uamuzi makubwa ya bajeti ya klabu hiyo.
KULE YANGA SASA
Wakati Simba ikionekana kusalimu amri kwa Chama, kwa upande wa pili sasa, Yanga wameshakamilisha kila kitu na kinachosubiriwa ni kiungo huyo kukubali kusaini mkataba wa mwaka mmoja.
Inadaiwa awali mabosi wa Yanga walipomfuata na kuzungumza na kiungo huyo, aliwaambia watulie kwanza kwa vile anaiheshimu Simba na anaipa kipaumbele kabla ya kugeukia klabu nyingine.
Hata hivyo, inaelezwa wakati Chama anaenda kwenye kikao na mabosi wa Msimbazi, tayari alishakuwa na mkataba wa Yanga kibindoni na hatua ya mabosi wake hao kumchomolea kwa kile alichokuwa anakitaka ameona ni rahisi kwake sasa kuhamia mtaa wa pili kama ilivyowahi kutokea kwa nyota wengine waliokipiga katika timu hizo ambazo ni watani wa jadi wa soka nchini.
Taarifa za ndani ya Yanga zinasema Yanga imeshazungumza na mchezaji huyo na kukubaliana naye juu ya dau la usajili, mshahara na bonasi nyingine ikiwamo nyumba, gari na mengine kati ya aliyoyataka Chama na wanachosubiri ni muda tu waliokubaliana ili kabla ya Juni 10 awe amesaini mkataba huo alioandaliwa.
Chama anataka kutumia hatua ya Simba kushindwa masharti yake ili akasaini dili hilo la Yanga, akaanze maisha mapya upande wa pili, bila ya kuwa na bifu kwani amewapa nafasi, lakini wameshindwa kuitumia.
Kama dili la Chama la kwenda Yanga litatiki, itaifanya Yanga eneo la mbele kuwa na mafundi wanaojua mpira kwani ataungana na Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Mudathir Yanga na wengine walioiwezesha Yanga kutetea taji la Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo na jana ilikuwa ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho ilililokuwa ikilishikilia kwa misimu miwili mfululizo.
AZIZI KI YUMO
Yanga inataka kumalizana na Chama haraka ili kumhakikishia kiungo, Stephanie Aziz KI hesabu zao za kukisuka kikosi imara kwa hesabu za msimu ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Yanga inataka kufika mbali hatua ya nusu fainali au hata fainali, ikinogewa na mafanikio ya msimu huu ya kukwamia robo fainali mbele ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyotoka nao suluhu mechi zote mbili kabla ya kupigiana matuta na Wasauzi kushinda kwa penalti 3-2.
Post a Comment