Chama anajua, ila Pacome anajua zaidi - EDUSPORTSTZ

Latest

Chama anajua, ila Pacome anajua zaidi

Chama anajua, ila Pacome anajua zaidi

Ligi mbali mbali zitaanza muda si mrefu download app yetu kutazama mechi zote za ligi kuu tanzania bara na ulaya live bure kabisa pia ndani ya app yetu utaweza kutazama muvi zilizotafsiriwa kwa kiswahili pia utaweza kutazama chanel za azam tv buree kabisa kudownload app yetu bonyeza 👉🏻👉🏻HAPA

Chama anajua, ila Pacome anajua zaidi

Mashabiki wa soka nchini kwa sasa wamekuwa na mjadala juu ya uwepo wa viungo washambuliaji, Clatous Chama wa Simba na Pacome Zouzoua wa Yanga.

Wapo wanaosema Chama ni mkali zaidi kwa kazi kubwa aliyoifanya akiwa na Simba kwa zaidi ya misimu minne, kulingana na Pacome aliyecheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa kwanza.

Kuna kila dalili wawili hao wanaoshindanishwa tangu mwanzo mwa msimu uliomalizika hivi karibuni wakacheza kikosi kimoja, baada ya kudaiwa Chama ameshamalizana na Yanga inayoshikilia ubingwa wa ligi hiyo kwa misimu mitatu mfululizo.

Hata hivyo, wakati mashabiki hao wakiwa na majibu yao kwenye mitandao ya kijamii, nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika, Milambo Tabora na Yanga, Idd Moshi ‘Mnyamwezi’ amemalizia ubishi kwa kutoa maoni yake juu ya viwango vya wawili hao alipozungumza na Mwananaspoti.

Mnyamwezi ambaye ni kaka wa Haruna Moshi ‘Boban’ kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, amefanya mahojiano maalumu hivi karibuni na kuweka bayana mtazamo wake juu ya wachezaji hao sambamba na kufunguka mambo kadhaa ya soka la Tanzania akiweka bayana Boban alivyo.

Kivipi? Ebu endelea naye...

CHAMA NA PACOME

Mkongwe huyo anakiri kwa miaka ya karibuni nchini hakutatokea mshambuliaji hatari wa kigeni kama alivyokuwa, Fiston Mayele aliyeichezea Yanga kwa misimu miwili kabla ya kutimkia Pyramids ya Misri ambako moto wake unaendelea kuwaka.

Anasema aina ya uchezaji wa Mayele anajiona ndivyo alivyokuwa anacheza enzi zake kwani hata yeye alikuwa anatumia nguvu na kusaka nafasi za kufunga, kitu ambacho mshambuliaji huyo alifanya alipokuwa nchini na hata huko alipo anaendelea kufanya hivyo hivyo.

“Ingawa mifumo ya sasa imetofautiana na zamani ambapo mbele alikuwa anasimama straika mmoja, hivyo kuna wakati nilikuwa na uwezo wa kunyang’anya mipira kuanzia katikati,” anasema Idd na alipoulizwa ishu ya Chama na Pacome kwanza alicheka kabla ya kutoa ufafanuzi.

“Wachezaji wote ni wazuri na wana vipaji kwelikweli vya soka eneo la kiungo cha ushambuliaji. Kila mtu anapenda kuona wanavyocheza na kuziendesha timu,” anasema na kuongeza;

“Niseme ukweli tu, Chama ni mchezaji mzuri na ana kipaji kikubwa, ila kuna vitu ambavyo Pacome anavyo vya ziada. Uwezo wa kukaa na mpira mguuni na kunyang’anya kutoka kwa mpinzani. Ila nasisitiza tena sina maana kwamba Chama mbaya, hapana lakini kuna vitu wanazidiana ni hivyo tu kwa mtazamo wangu.”


Katika msimu uliomalizika hibvi karibuni, wawili hao walizibeba timu zao, Chama akifunga mabao saba na kuasisti saba, sambamba na kufunga mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Pacome pia alifunga mabao saba na kuasisti matatu na kufunga matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuasisti moja.

ILE FUNGATE BUANA

Kuna mambo wanayoyapitia wanasoka, baadaye yanawapeleka kwenye majuto makubwa, kama anavyosema Idd akikumbushia alipoacha fungate baada ya kufunga ndoa kisha kwenda uwanjani kuvaana na Simba na kuifungia timu yake mabao yote mawili wakati Yanga ikiwalaza Wekundu wa Msimbazi 2-0 katika mechi iliyopigwa Agosti 5, 2000.

Anasema hakikuwa kitu cha ajabu kuifunga Simba baada ya kutoka fungate, kutokana na aina ya mwanamke aliyemuoa kufahamu majukumu yake.

“Tarehe yangu ya ndoa iligongana na mechi ya dabi, viongozi waYanga walinikatia tiketi ya kwenda na kurudi Tabora, baada ya kuoa nikageuka kucheza mechi hiyo, bila shida yoyote,” anasema Idd na kuongeza;

“Wengi walikuwa hawaamini kama ningefunga mabao mawili, hadi walinipachika jina la Bwana Harusi ingawa kwa sasa limefutika kwa sababu nina watoto, jina jingine la utani ninaloitwa hadi leo ni Mnyamwezi.

“Nyuma ya kujituma kwangu kwenye mchezo huo, nilitaka mke wangu ajivunie mimi, jambo jingine kuondoa fikra potofu za kuona mchezaji akioa anakuwa anapoteza uwezo, ukiona mchezaji kiwango kinashuka kisa kaoa basi anakuwa hajitambui.”

Mabao hayo ya Idd yalikuwa ndio ushindi wa mwisho wa timu hiyo ya Wananchi dhidi ya Simba kwa miaka minane iliyofuata, kwani kutokea hapo Yanga ilishindwa kupata ushindi wowote mbele ya Simba katika mechi za Ligi, ikiishia kula vipigo ama sare mbele ya Mnyama hadi pale Mkenya, Ben Mwalala alipokuja kukata minyororo ya unyonge alipoizima Simba kwa bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Oktoba 26, 2008.

USHIRIKINA

Idd anasema katika soka vitendo vya ushirikina vipo, ingawa huwa havisaidii kwa lolote zaidi ya kutumika kama njia ya kuongeza hamasa au hofu kwa wanaovitegemea.

Anasema amewahi kushuhudia vitu vya kishirikina wakati anacheza, ambavyo walijikuta wanalazimika kuvifanya kutokana na matakwa ya timu.

“Siwezi kusema nikiwa timu gani, ila vitu hivyo zamani vilikuwepo, Mwenyenzi Mungu atusamehe, nikivikumbuka najikuta najisikia vibaya, ukiwa kwenye timu unaweza ukawa hutaki, ukikataa na timu ikifungwa unaonekana kuhujumu timu,” anasema na kuongeza;

“Tofauti na sasa mambo yamebadilika, sioni kama vinapewa kipau mbele, nadhani inachangiwa na mchanganyiko wa wachezaji wageni na wazawa.”

BOBAN KICHWA SANA

Anasema ni mdogo wake wa kuzaliwa na katika kukua kwake, alikuwa anapenda mpira, hakubali kushindwa na kitu asichokipenda udanganyifu.

“Watu wasiomfahamu Boban wanamuona mjeuri, ila ni mkimya, ana huruma, msikivu, mtoaji, mpenda watu, anashindwana na watu wasiopenda onyoofu, kwa sababu anapenda kitu mkikubaliana kiende kama ahadi ilivyo,” anasema.

Anasema 2010/2011 alipata dili katika klabu ya Gefle IF ya Sweden na kilichomrudisha Tanzania ni kutokupata haki zake.

“Boban siyo mtu wa kuongea, alikuwa na mameneja wawili mmoja Mtanzania na mwingine wa nje, kuna kiasi cha pesa walikubaliana naye, ajabu hawakuwa wanamuingizia hicho kwenye akaunti yake, akanipigia simu kinachoendelea, ili nimshauri,” anasema na kuongeza;

“Aliniambia kaka siwezi kumwaga jasho, halafu nikarudi Tanzania nikaanza kuomba pesa watu watanicheka, hivyo kama siyo riziki yangu basi Mwenyenzi Mungu atanipa njia nyingine, nilimuelewa kwani kuna maisha baada ya soka, kusema ukweli kocha wa timu hiyo alikuwa anamkubali hadi akawa anampigia simu arudi kwenye timu.

“Mfano kaka sasa hivi nimemshauri anyoe rasta zake, amefanya hivyo bila ubishi, ndio maana nasema ni msikivu tofauti na jamii inavyomchukulia, ana maisha yake mengine ambayo watu hawayafahamu kuhusu yeye.”

TUKIO GUMU

Anasema mwaka 1999, wakati anasafiri na timu ya taifa, Taifa Stars, kwenda Malawi, alipigiwa simu na mjomba wake ya taarifa ya kifo cha mdogo wake, jambo lililomuweka kwenye nyakati ngumu.

“Kwa sababu nilikuwa safarini, sikuwa na chakufanya nikafika hadi Malawi, nikacheza mechi, ingawa tulifungwa, wachezaji wenzangu, kocha na viongozi walinifariji na kunipa ujasiri, mjomba mwenyewe aliniambia hakuna kitu nitabadilisha, napaswa kupiga moyo konde.

“Baada ya kurejea Tanzania ndipo nikaenda nyumbani Tabora, tukio hilo sitakaa nilisahau kwenye maisha yangu.”

DAU LA USAJILI

Anasema wakati anasajiliwa Yanga, alipewa si chini ya Sh5 milioni ambapo kwa kipindi hicho ilikuwa pesa ndefu, aliitumia kujenga nyumbani kwao Tabora.

“Angalau nina alama ya jasho langu la soka, wakati najiunga na Yanga nilipata wakati mgumu kwenye nafasi yangu alikuwepo Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, Sekilojo Chambua ambao walikuwa kwenye kiwango cha juu, lakini nilipambana hadi nikapata nafasi ya kucheza,” anasema.

Mbali na hilo, anasema Yanga ya sasa ina mabadiliko makubwa na inajitahidi kuonyesha uwezo wa ushindani kwenye michuano ya CAF.

“Zamani hatukuwa tunaahidiwa chochote, unajituma ukifanya vizuri, tajiri anapiga simu kukupa pongezi, kwa sasa wana kila sababu ya kufanya makubwa, wanapewa bonasi kubwa na mishahara minono juu,” anasema na kuongeza;

“Jambo ninaloweza kuwashauri wanasoka wote kwa ujumla, kidogo wanachopata wajitahidi kuwekeza, kwani ni wastaafu watarajiwa wasije wakapata shida wakija mtaani.”

Kuhusu tuhuma za rushwa soka la zamani, anasema: “Japokuwa vilikuwepo ila naona kama ilikuwa ni mind game, upande unaokuwa vibaya kiuwezo unakuwa unaanzisha maneno, nakumbuka kuna siku Ally Mayay kwa sasa kaimu mkurugenzi wa michezo nchini, aliwahi kutaka kususa mechi fulani, baada ya kusikia kama kuna watu wamevuta mkwanja kutoka timu pinzani.”

Nje na hilo, anasema Simba iliwahi kuhitaji huduma yake, ila Yanga iliamua kumficha nje ya Dar es Salaam, ili asipatikane: “Nakumbuka baada ya kucheza kwa mafanikio Yanga, viongozi wa Simba walikuja, nikapewa nauli ya kwenda Tabora, kipindi cha usajili kilipoisha wakanirudisha Jangwani.”

MALENGO YA GALACTICOS

Taasisi ya Umoja wa Wachezaji wa Zamani Tanzania (TFLA), wakijulikana kama GALACTICOS, wana mpango wa kutembea kwenye klabu za soka, ili kuwapa elimu wachezaji ya kujiandaa na maisha nje ya soka.

Moshi akiwa kama mtunza hazina wa taasisi hiyo, anasema “Hatutaki wachezaji wapitie maisha magumu baada ya kustaafu soka, yapo mambo tunayoweza kuwajenga na yakawasaidia.

Anaongeza: “Pia tunasaidiana wenyewe kwa wenyewe, mwenyekiti ni Mayay, makamu ni Juma Pinto na katibu Jumanne Nyovu, nadhani tukikaa tena tutaweka mipango madhubuti.”



Download our APP from Google Playstore using the link here>>>

Join Our Telegram Channel for Daily Updates CLICK HERE

No comments:

Post a Comment

Edusportstz