Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, CPA Issa Masoud amesema shilingi bilioni 20 zinazopaswa kuwekwa na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji zimeibua matatizo baada ya mwekezaji huyo kudaiwa kuhitaji fedha alizotoa awali kama msaada zigeuzwe kuwa mtaji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Masoud amesema walipokea taarifa ambazo hazikuwa katika urasmi wake ikiwataka kama Bodi kupitisha azimio lililokuwa likisema pesa alizokuwa anazitoa mwekezaji kama msaada zihesabiwe katika hisa.
CPA Issa Masoud ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Fedha Simba, amesema katika nyaraka mbili zilizopo ndani ya Simba, moja ya Simba SC Company na nyingine ya Mo Simba Company Ltd, hakuna sehemu ambayo inamtaka Mo Dewji kutoa fedha nje ya makubaliano ya uwekezaji.
“Mo hatakiwi kutoa fedha nje ya makubaliano kama mwekezaji ambapo atatoa utakapomalizika mchakato, lakini hapa kati Mo amekuwa akitoa hela na hata baadhi ya mahojiano mbalimbali amekuwa akisema hilo.
“Lakini cha ajabu tuliletewa taarifa katika kamati yetu ya ukaguzi kwamba fedha zozote ambazo Mo alikuwa anatoa anazidai na ameelekeza zibadilishwe ziwe mtaji wake anaopaswa kutoa Simba SC.
“Hiyo imetuletea shida ambayo mnaiona sasa hivi, sisi tukakataa kwamba yale siyo makubaliano yetu lakini kiasi ni sawasawa na mtaji anaotakiwa aweke, maana yake kwamba zile zikibadilishwa kuwa mtaji bilioni 20 zitakuwa zimeisha.
“Tukatafuta njia za kumuita ili kuliweka sawa hili ili lisiende kuleta mkanganyiko kwa wanachama na mashabiki. Tulipokataa ikaonekana ni kama vile Wajumbe wa Bodi wamempinga.
“Kitendo cha kusema tunazibadilisha zile hela zote kuwa mtaji lazima yawepo makubaliano ya pande mbili (Simba SC Company inayomiliki hisa 51,000 na Mo Simba Company Ltd anayemiliki hisa 49,000), ifahamike hapa kwamba hisa za Klabu ya Simba zipo 100,000. Hawa watu wawili ndiyo wanaounda kitu kinachoitwa Simba SC Company Ltd.”
Simba SC bado ipo katika mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ulioanza mwaka 2018 ambapo hisa asilimia 51 zitakuwa za wanachama na 49 za mwekezaji ambaye mpaka sasa mwekezaji huyo ni Mo Dewji anayetarajiwa kutoa kiasi cha Sh20 bilioni za mtaji wa kununua hisa hizo.
Post a Comment