Straika wa zamani wa Simba Mkongomani, Jean Baleke yupo nchini akiwa katika mazungumzo na timu mbili za Dar es Salaam, Azam na Yanga.
Inaelezwa Baleke aliyecheza Simba kwa mkopo akitokea TP Mazembe kabla ya kutimkia Al Ittihad ya Libya Januari mwaka huu, yupo katika mazungumzo na mabosi wa Azam na Yanga akitaka kujiunga na mojawapo.
KLABU ya Pamba Jiji iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu ulioisha inaendelea kuboresha kikosi chake na sasa imetua kwa mshambuliaji wa Ken Gold, Edgar Wiliiams.
Pamba inaamini Edgar aliyeibuka kinara wa ufungaji kwenye Championship ataongeza kitu katika safu yake ya ushambuliaji kwa msimu ujao itakaposhiriki Ligi Kuu baada ya muda mrefu na mazungumzo yanaendelea.
BAADA ya msimu mmoja wa kiwango bora ndani ya Chippa United ya Ligi Kuu Afrika Kusini, timu hiyo imedhamiria kumuongeza mkataba kiungo Mtanzania, Baraka Majogoro.
Majogoro aliye kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania alijiunga na Chippa mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar kwa mkataba wa mwaka mmoja utakaotamatika mwezi huu.
SINGIDA Black Stars (zamani Ihefu) imedaiwa ipo katika mazungumzo na nyota aliyewahi kutakiwa na Simba, Victorien Adebayo kutoka Niger, sambamba na kipa kutoka AC Horoya ya Guinea, Mohamed Kamara.
Taaifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa, Singida inamtaka Adebayor aliyewahi kucheza RS Berkane na AmaZulu kabla ya kurejea kwao Niger, ili kuziba nafasi ya Emmanuel Bola Labota anayetakiwa Yanga.
MSHAMBULIAJI wa Geita Gold iliyoshuka daraja, amedaiwa yupo katika mazungumzo na Mashujaa na Pamba Jiji zinazohitaji saini ili aitumikie moja ya timu hizo kwa msimu ujao.
Mchezaji huyo aliyemaliza msimu wa 2023-2024 akiwa na bao moja, anasikilizia timu itakayokubaliana na masharti yake ili amwage saini na kuvaa jezi ya timu hizo, huku Pamba ikitajwa ipo hatua nzuri zaidi.
WAWAKILISHI wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, Azam FC imedaiwa ipo katika hatua nzuri ya kumuongezea mkataba mpya winga wa timu hiyo, Ayoub Lyanga ili asalie kikosini.
Mkataba wa Lyanga umemalizika na amekuwa akihusishwa na Coastal Union aliyowahi kuitumikia kabla ya kutua Chamazi na hilo ndilo lililowafanya mabosi wa Azam kutaka kumbakisha aendelee kukipiga hapo.
IKIWA na kiu ya kufanya vyema katika msimu wa kwanza wa kucheza Ligi Kuu Bara, KenGold, imedaiwa ipo hatua za mwisho kumrejesha nchini, Kocha Thierry Hitimana ili ainoe timu hiyo.
Hitimana aliyewahi kuzinoa Biashara United, Namungo, Simba na KMC, inaelezwa ameshaweka mezani mahitaji anayoyataka na KenGold imebakia kuridhia na kumshusha kuanza kazi baada ya timu hiyo kumaliza kama vinara wa Ligi ya Championship.
BONYEZA HAPA KUANGALIA VIDEO ZA WAKUBWA ILI UJIFUNZE MAUTUNDU
Post a Comment