Stephane Aziz Ki. Fahari ya Yanga kwa sasa. Amekuwa na msimu bora kuliko wakati mwingine wowote kwenye maisha yake ya soka.
Amemaliza msimu akiwa kinara wa mabao katika Ligi Kuu Bara. Amefunga mabao 21. Ni miaka minne tangu mchezaji wa mwisho alipofunga mabao zaidi ya 20 kwenye msimu mmoja wa Ligi.
Alikuwa Meddie Kagere wa Simba. Alifunga mabao 23 mwaka 2019. Alikuwa kwenye ubora mkubwa wakati ule.
Aziz Ki anakuwa pia kiungo mshambuliaji wa kwanza kuwa Mfungaji Bora wa ligi baada ya muda mrefu. Inafurahisha sana.
Alipotua Yanga mwaka jana hakuwa katika ubora mkubwa sana. Mashabiki wengi walikuwa wakimfananisha na Clatous Chama. Mchezaji aliyeweka ubora wa ligi yetu.
Licha ya kuonyesha ubora kwenye baadhi ya mechi bado hakuwa na msimu mzuri sana.
Bahati mbaya kwa Aziz, alitua Yanga wakati staa wa timu alikuwa Fiston Mayele. Mchezaji aliyejipambanua vyema ndani ya Yanga kwa miaka yake miwili.
Ungewaambia nini Wananchi juu ya Mayele? Aliwafanya wateteme kwa raha kila wakati. Alifunga mabao kwenye mechi muhimu.
Aliwabeba kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Alikuwa mfungaji bora wa mashindano. Alikuwa kwenye kiwango bora sana.
Ila msimu huu kila upande imekuwa ni Aziz Ki. Amefanya vizuri kwenye mashindano yote. Ameibeba Yanga kwa kadri alivyoweza. Inafurahisha sana.
Hata hivyo, kufanya vizuri kwa Aziz Ki kunawaweka Yanga katika mtihani mwingine mgumu. Wataweza kumbakisha kwa msimu mwingine zaidi? Inafikirisha.
Mkataba wa Aziz Ki umekwisha. Kazi yake kubwa ya mwisho ni fainali ya Kombe la Shirikisho pale visiwani Zanzibar leo usiku.
Baada ya hapo atakuwa mchezaji huru. Anaweza kusaini timu nyingine yoyote.
Kwa nini Yanga wamesubiri hadi mkataba wake umekwisha kabisa? Inashangaza sana.
Mchezaji alishajipambanua anaweza kucheza kwa ubora mkubwa kwa miaka kadhaa inakuwaje anaachwa hadi anakuwa huru?
Licha ya Aziz Ki kusema anawapa Yanga kipaumbele katika mazungumzo ya mkataba mpya, ukweli ni kwamba wana kazi kubwa ya kumsainisha mkataba mpya.
Ni kweli ana ofa kutoka baadhi ya timu kubwa za Afrika Kusini na Kaskazini mwa Afrika. Huko kuna malisho mazuri zaidi.
Wanaweza kumpa fedha ndefu zaidi ya ambazo Yanga wanaweza kumpatia. Wanaweza kulipa vyema zaidi ya timu nyingine yoyote nchini.
Ubaya zaidi ni kwamba akiondoka Yanga haipati chochote. Anaondoka kama mchezaji huru. Ni kama ambavyo wachezaji wengi wamewahi kuondoka nchini.
Ila swali la kujiuliza hapa ni kwanini timu zetu zinapenda kuwapa wachezaji mikataba mifupi? Kama Aziz Ki angesaini Yanga miaka mitatu kwa sasa hata wasingekuwa na presha. Wangekuwa na mwaka mwingine mmoja mbele wa kumshauri asaini mkataba mpya.
Wachezaji wengi wakubwa duniani husainiwa kwa mikataba mirefu. Yanga walipaswa kufanya hivyo kwa Aziz Ki, Pacome, Yao Kouassi na wengineo. Hii mikataba mifupi ni pasua kichwa.
Ndivyo mikataba ambayo inamfanya Chama awapasue Simba kichwa kila mwaka. Kila msimu ukimalizika wanajikuta kwenye hekaheka za kumsainisha tena. Kwa nini? Wanajua wenyewe.
Nadhani hiki kinachofanywa na Azam FC kwa Sasa kusajili wachezaji kwa mikataba ya miaka minne kinapaswa kuigwa. Ni kitu kizuri kwa ustawi wa timu.
Unapowasajili wachezaji kwa mikataba mirefu inakusaidia hata kutuliza akili kwenye usajili mwingine. Mfano Sasa Yanga ingeweka zaidi nguvu kwenye maboresho ya kikosi chake na nyota wapya wa kusajili na siyo kuhangaika na Aziz Ki.
Ila yote kwa yote acha tuone msuli wa Yanga kwenye hili. Watafanikiwa kumbakisha? Tusubiri na kuona.
Ila wakati Yanga wanapambana kumbakisha kinara wa mabao kwa timu yao na ligi, Simba wanapambana kumbakisha Denis Kibu na bao lake moja alililofunga msimu mzima wa Ligi. Kweli maisha ni kuchagua.
Post a Comment