Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amebainisha maeneo ambayo timu yao ilikosea na kusababisha kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano walioshiriki msimu huu ikiwemo Ligi Kuu ya NBC, Kombe la Shirikisho la CRDB na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ahmed amesema hayo jana baada ya Ligi Kuu kutamatika huku Simba wakimaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo ambapo wameangukia kwenye michuano ya kombe la shirikisho Afrika ambayo watashiriki msimu ujao jambo ambalo amesema hayakuwa malengo yao kabisa.
“Hatuwezi kuendelea kuumiza watu, tumetoka hali mbaya tunakwenda mbaya zaidi, msimu huu nafasi ya tatu yenyewe tumeitolea jasho kwelikweli. Tafsiri yake ni kwamba ubora wetu umepungua sana. Ukweli ni kwamba Simba yetu haiko sawa sawa, haiko kwenye ubora tunaoutaka na haiku kwenye level ya kiushindani, lazima tukafanye maboresho makubwa Mnyama arudi kwenye anga zake.
“Lazima ufanye tathmini kwa misimu mitatu tumekosa mataji, huyu mchezaji alikuwepo msimu wa kwanza nimekosa ubingwa, msimu wa pili alikuwepo nimekosa, msimu wa tatu alikuwepo na nimekosa ubingwa, nikienda naye msimu wan ne atanipa ubingwa? Tutafanya tathmini ya mchezaji mmoja mmoja kwa umakini ili tukifanya maamuzi yawe sahihi na bora kwa maslahi ya Simba. Tuwaache viongozi wetu waache maamuzi sahihi,” amesema Ahmed Ally.
Post a Comment