Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ameshindwa kujizuia kwa kumtaja kiungo Maxi Nzengeli, kuwa ni miongoni mwa wachezaji waliokibeba kikosi hicho msimu huu, tofauti na mitazamo ya wengi.
Maxi alisajiliwa na Yanga msimu huu akitokea AS Maniema Union ya DR Congo na kuwa mmoja wa nyota walioshiriki kwa kiasi kikubwa kuiwezesha timu hiyo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mbali na kuipeleka fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) itakayopigwa wikiendi ijayo visiwani Zanzibar.
Akizungumza nasi, Gamondi amesema Maxi amecheza kwa kiwango kikubwa msimu huu, jambo linalomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wake bora.
Ameeleza kuwa kwa watu wa kawaida ni vigumu kuona kazi yake kubwa anayoifanya, lakini kwake akiwa kocha huyo ni kiungo anayecheza eneo kubwa uwanjani.
"Maxi utamuona anacheza nafasi mbali mbali ikiwemo, ulinzi na hata ushambuliaji hatua yake ya kufunga mabao 10 ndani ya msimu wake wa kwanza ni kielelezo kingine cha ubora wake," amesema Gamondi, raia wa Argentina na kuongeza:
"Pia ni mchezaji mshindani kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi, asiyekata tamaa hata akikutana na mazingira magumu kiasi gani na yuko tayari kupambana kutafuta pasi na kumpa mwenzake akafunga."
Mabao 10 aliyofunga hadi sasa akiwa na Yanga, yamemfanya Maxi kuwapiku nyota kadhaa wa timu hiyo na hata wa timu nyingine ikiwamo Simba ambao wamefunga idadi ndogo ya mabao kulinganisha naye.
Katika timu hiyo mchezaji huyo amewapita Pacome Zouzoua mwenye mabao saba, Kennedy Musonda mwenye manne, Clement Mzize (6) na Joseph Guede aliyefunga matano, wakati kwa Simba amewazidi Clatous Chama aliyefunga saba, Saido Ntibazonkiza (9), Kibu Denis aliyefunga moja na Freddy Michael mwenye mabao sita.
Guede na Freddy, hata hivyo kila mmoja alisajiliwa na vigogo hao katika dirisha dogo kulingana na wakali wengine walioachwa mbali na Maxi akiwamo Kipre Junior (9) na Gjibril Sillah (7) wote wa Azam FC.
Post a Comment