Mashabiki wa FC Lupopo wameandamana mpaka kwa mabosi wa klabu yao wakigomea kuondoka kwa beki Chadrack Boka, anayetakiwa na Yanga.
Chanzo cha maandamano hayo ni mchezo wa TP Mazembe dhidi ya FC Lupopo uliopigwa Mei 22, mwaka huu ambao licha ya timu hiyo ya Boka kupokea kichapo cha bao 1-0 ugenini, lakini beki huyo alikuwa bora.
Baada ya mechi hiyo mashabiki wa Lupopo wala hawakulia na matokeo, lakini walichofanya ni kuchukizwa na hatua za timu hiyo kutaka kumuuza Boka na kuandamana mpaka ofisi za klabu hiyo wakitaka uongozi ufanye mambo mawili.
Kwanza, wametaka kutafuta beki wa maana kama Boka au zaidi, lakini kama watashindwa basi wasitishe mpango wa kumuuza wakiamini timu yao itabomoka beki huyo akienda Yanga.
Boka amebakiza mwaka mmoja katika mkataba na Lupopo akiwa mmoja wa nguzo muhimu kwenye kikosi cha timu hiyo na miongoni mwa wachezaji tegemeo.
Katibu Mkuu wa Lupopo, Donat Mulongoy ameithibitishia Mwanaspoti juu ya mashabiki hao kuwa wakali, lakini akasema klabu yao itazingatia maono yao.
Mulongoy amesema Lupopo hata kama itaamuza Boka itafanya usajili mwingine wa maana kuziba nafasi yake ingawa wanatambua kwamba beki huyo ni mtu wa maana katika kikosi chao.
"Mashabiki wanapenda wachezaji wao hasa wakiwa wanafanya vizuri kuwa wakali kama hivi tunawaelewa. Hapa Lupopo mmoja wa wachezaji wetu bora ni Boka. Kila timu ya hapa inatamani kuwa na beki kama huyu," amesema Mulongoy.
"Bado hatujamuuza Boka ni mchezaji wetu, kama hataondoka tutamuongezea mkataba mrefu, lakini kama timu inayomtaka itafika kwenye pesa tunayotaka tutafanya uamuzi, lakini pia tutatafuta beki mzuri wa kuziba nafasi yake."
Kupitia Mwanaspoti iliandika kuwa Yanga inamtaka na rais wa timu hiyo, Hersi Said alikwenda DR Congo kuzungumza na uongozi wa timu yake ili kujua namna gani watapata saini yake.
Haikuchukua muda mabosi wa Lupopo walifika Dar es Salaam kukutana na wenzao wa Yanga katika kikao ambacho hawakufikia muafaka ndani ya saa saba, kwani dau la kumpata mchezaji huyo lilikuwa kubwa.
Kutokana na hilo, mabosi hao walipeana muda ili kutafakari kama Wakongomani hao watashuka dau au Yanga watalipa Dola 100,000 kwa ajili ya mchezaji huyo anayetajwa kutakiwa Yanga ili kuridhi nafasi ya Mkongomani mwenzake, Joyce Lomalisa.
Kama dili hilo litatiki, mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza kama winga atacheza nafasi ya Lomalisa ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.
Post a Comment