Simba bado wanaendelea kuugulia maumivu ya kufungwa kwa mara ya pili katika msimu mmoja wa Ligi Kuu Bara na watani wao, Yanga lakini tayari mabosi wa klabu hiyo wamepanga kufanya uamuzi mgumu wa kufyeka mastaa saba hadi wanane wa kikosi kilichopo kwa sasa katika dirisha la usajili litakalofunguliwa Julai mwaka huu.
Wekundu wa Msimbazi walikumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Yanga katika pambano la marudiano ya Ligi Kuu baada ya awali kufungwa mabao 5-1 zilipokutana Novemba 5 mwaka jana na kujiweka pabaya katika kuwania ubingwa wa msimu huu kwani imesaliwa na pointi 46 baada ya mechi 21, ikiwa ni pointi 12 pungufu ya ilizonazo Yanga inayoongoza msimamo kwa alama 58.
Mwanaspoti imepenyezwa taarifa kwamba kipigo hicho kimezidi kuwachefua mabosi wa Msimbazi ambao wamepanga kufanya uamuzi mgumu dhidi ya kikosi kilichopo sasa na tayari kuna majina yasiyozidi manane yamezungushiwa wino mwekundu wa kufyekwa kupitia dirisha kubwa lijalo.
Ipo hivi. Wakati mechi ya juzi ya Kariakoo Dabi ikipigwa Kwa Mkapa, mabosi wa klabu hiyo waliokuwa jukwaani walikuwa wakiuangalia mchezo huo, huku wakiwa kazi nyingine ya kufanya tathimini ya mwisho ya mastaa wakijua huo unaweza kuwa mmoja kati ya michezo migumu miwili ya mwisho waliosaliwa nayo.
Baada ya matokeo hayo mabosi wa Simba wamekubaliana kwa dakika 90 za mchezo huo zimewapa majibu kuwa kuna idadi ya wachezaji wanaopaswa kupitiwa na panga kali kwa ajili ya kuunda kikosi cha kutisha cha msimu ujao.
Kumbuka juzi wakati wa mapumziko, Mwanaspoti liliwanasa vigogo wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Abdallah Salim ‘Try again’ wakilazimika kushuka chini kwenda kuzungumza machache na wachezaji muda ambao tayari kikosi chao kilishakuwa nyuma kwa mabao 2-0.
Japo Mwanaspoti haikunasa moja kwa moja kilichozungumzwa, lakini tathmini inaonyesha ni kama mazungumzo hayo ndio yaliyoibadilisha Simba ikarudi kwa nguvu mpya kipindi cha pili na kupata bao moja la kufuatia machozi lililofungwa na mtokea benchi, Freddy Michael baada ya awali kucheza vibaya kipindi cha kwanza.
Lakini baada ya mechi hiyo, mmoja wa mabosi wa juu wa Simba, aliliambia Mwanaspoti, kwa kikosi kilichopo sasa wasingeweza ‘kutoboa’ mbele ya Yanga na hata katika Ligi Kuu kwa ujumla na kwamba kuna uamuzi mgumu wataufanya mwisho wa msimu huu.
Bosi huyo, aliyekataa kuandikwa jina gazetini, alisema panga hilo litawapitia wachezaji saba mpaka wanane ambapo ndani yake yapo majina ambayo yatawashtua wengi, lakini ndio hatua ya ujenzi wa Simba mpya ya msimu ujao.
“Simba haiwezi kukumbatia majina tena, huu ndio msimu ambao kila mmoja ameumia kwa hali ya timu yetu, hizi mechi tunacheza kwa sababu ya matakwa ya kikanuni lakini tumekaa juu pale tumejionea wenyewe,” alisema bosi huyo na kuongeza;
“Hapa kuna kundi kubwa tunatakiwa kuliacha yaani kuanzia wachezaji saba au wanane tutaachana nao, muhimu hapa mwekezaji ameridhia haya yote, ingawa naona safari hii atakuwa tofauti kidogo utakapofika wakati wa usajili. Kuna mambo mengi yatakwenda kubadilishwa kuanzia huku ndani na hata huko nje, sio afya kwa klabu kubwa kama Simba kufikia hali kama hii lakini nikuhakikishie kuna majina yatawashtua kweli.”
Mtu mwingine wa karibu wa klabu hiyo, alisema hali iliyonayo Simba ni tofauti na malengo waliyojiwekea na sasa wanaenda kujitathmini kwani sasa ni kama wamemaliza msimu kutokana na pointi walizoachwa nyuma na Yanga na timu inavyocheza hakika inawakatisha tamaa, japo wanataka angalau kumaliza msimu kwa heshima tu.
WASIKIE WADAU
Kiungo wa kimataifa wa zamani wa Tanzania aliyeshiriki fainali za Afcon 1980, Mtemi Ramadhan alisema jambo kubwa analoliona ndani ya timu hiyo ni kukosa fitinesi ya kutosha kwa wachezaji.
“Ukiangalia michezo ya hivi karibuni utagundua wachezaji wa Simba wanaanza mchezo vizuri lakini kadri unavyosogea ndivyo ambavyo wanazidi kuchoka, kwangu kocha wa fitinesi anapaswa kuwajibika kwa hili na sioni anapokwepa lawama,” alisema nyota huyo wa zamani wa Simba.
Mtemi aliongeza, hata kama viongozi wataondoa wachezaji zaidi ya saba au tisa ila kwake haoni kama itakuwa ni suluhisho la kudumu, kwani hata nyota kama, Clatous Chama ambaye ndiye mhimili wa timu kuna muda anamuona anachoka zaidi awapo uwanjani.
Kwa upande wa beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa alisema viongozi wanapaswa kujitafakari kwani haiwezerani kila siku kulaumu wachezaji kwa sababu wao ndio wamekuwa wakiwaleta kutokana na jinsi walivyowaona huko walikotoka mwanzoni. “Wasitafute sehemu ya kujifichia,” alisema.
Post a Comment