Presha ya mchezo wa ‘Kariakoo Dabi’ kwa mashabiki wa Yanga na Simba nchini tayari imeanza kupanda wakati ikibakia siku moja tu kwa miamba hiyo kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho Jumamosi kuisaka heshima baina yao.
Kitendawili cha nani mbabe kitateguliwa Jumamosi hii ingawa Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali kubwa hasa baada ya mechi yao ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5, 2023 kuifunga Simba kwa mabao 5-1.
Katika mchezo huo wa mwisho mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili wakati Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI walifunga moja kila mmoja wao huku la Simba la kufutia machozi likifungwa na Kibu Denis.
Wakati pambano hilo likisubiriwa, moja ya maeneo muhimu ni eneo la kiungo kwa sababu mipango yote ya timu inaanzia hapo, huku wachezaji wakitakiwa kuongeza umakini na kuhusika kikamilifu muda wote wanapokuwa na mpira au wanapokuwa hawana.
Katika miaka ya hivi karibuni soka linachezwa kwa mifumo na sayansi zaidi na hapo ndipo thamani ya viungo inapozidi kupanda kutokana na mahitaji na faida zao katika timu japo kwa sasa washambuliaji ndio wamekuwa wakipewa heshima hiyo.
Simba na Yanga zote uimara wake kwenye viungo sio jambo la kutilia shaka kwani kila timu ina machaguo zaidi ya mawili katika kila kipande katika eneo la kiungo na vipande hivyo ni viungo wake wakabaji na wale viungo washambuliaji.
Yanga ambao ni wenyeji wa mchezo huo, eneo la viungo wazuiaji wamekuwa wakicheza Khalid Aucho, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Jonas Mkude, Zawadi Mauya na Mudathir Yahya anayecheza kiungo mshambuliaji sawa na Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI na Farid Mussa.
Kwa Simba eneo la kiungo wazuiaji huwa wanaocheza zaidi ni, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma, Babacar Sarr na Mzamiru Yassin huku kwenye kiungo chao cha ushambuliaji wakiwategemea, Clatous Chama, Kibu Denis na Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’.
Kutokana na namna timu hizo mbili zimekuwa zikicheza kwenye vikosi vyao vya hivi karibuni kuna baadhi ya wachezaji wa eneo la kiungo wenye nafasi ya kuanza katika mechi hiyo na huu ni uchambuzi wa namna wanavyoweza kuzisaidia au kuziponza.
AZIZ KI V KANOUTE
Simba imekuwa ikimtumia mara kwa mara Sadio Kanoute kama kiungo wa chini (namba sita), kwa maana hiyo jukumu lake ni kumkaba kiungo wa juu wa timu pinzani (namba 10) na kwa Yanga ni Stephane Aziz KI jambo linaloongeza mvuto wa ‘Derby’.
Aziz KI ana ubora wa kupiga pasi, chenga kukimbia na kufunga mabao kitu kitakachoongeza ushindani kwani Kanoute ambaye anasifika kwa kukaba kwa nguvu jukumu lake litakuwa ni kuhakikisha anamzuia ipasavyo ili asiweze kuleta madhara kwao.
Hata hivyo. haitokuwa rahisi kwa Kanoute kufanya hayo kwani Aziz KI amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu kwa sababu hadi sasa katika Ligi Kuu Bara ndiye kinara akifunga mabao 14, moja mbele ya nyota wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye 13.
MZAMIRU V MUDATHIR
Hapa ni vita ya kweli kati ya viungo hawa wawili ambao mara nyingi hutumiwa kama viungo wa kati, hapa huwa katikati ya uzuiaji na ushambuliaji.
Mudathir amekuwa kwenye kiwango bora pia msimu huu akifunga mabao manane katika Ligi Kuu Bara kitu kinachoweza kuleta faida zaidi kwa Yanga tofauti na kwa upande wa Simba ambao viungo wao wengi wa kukaba wamekuwa butu kwenye kufunga.
CHAMA V AUCHO
Vita nyingine tamu ya kuitazama ni kati ya Clatous Chama na Khalid Aucho kwani wawili hao wote wana uzoefu wa kutosha na mechi kubwa.
Chama ni bora zaidi kwenye kutengeneza nafasi za mabao na hadi sasa amefunga saba akiwa anaongoza kwa wachezaji wa Simba sambamba na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ kwani Jean Baleke aliyeondoka Januari mwaka huu alikuwa kinara akifunga manane.
PACOME V NGOMA
Unapotaja wachezaji waliofanya vizuri hadi sasa hutoacha kulitaja jina la nyota wa Yanga, Pacome Zouzoua kutokana na ubora wake.
Pacome mwenye mabao saba ya Ligi Kuu Bara bado hana uhakika wa kucheza mchezo huo mgumu kutokana na majeraha aliyonayo ingawa kama atacheza basi itakuwa faida kwa mashabiki wa Yanga kwani nyota huyo amekuwa na mchango mkubwa kikosini hapo.
Kama ataweza kucheza basi atakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma ambaye husifika kwa kuzuia huku akiwa na jukumu nzito la kuhakikisha nyota huyo haleti madhara kwao kutokana na udambwi dambwi alionao.
MKUDE V SARR
Mkude aliyeichezea Simba kwa takribani miaka 12 anakutana tena na waajiri wake wa zamani huku akiwa katika kiwango bora tangu alipoanza kuaminiwa na kocha, Miguel Gamondi kwenye michezo ya kimataifa baada ya kuumia kwa kiungo, Khalid Aucho.
Nyota huyo ambaye hujulikana kwa jina la utani la ‘Nungunungu’, ikiwa itacheza anaweza kukutana na bato nyingine kali ya kiungo Msenegali, Babacar Sarr ambaye hata hivyo bado hajaonyesha kiwango cha kuvutia tangu aliposajiliwa msimu huu.
Hata hivyo, Babacar aliyesajiliwa kama mchezaji huru baada ya kuachana na klabu ya US Monastir, ana uzoefu na michezo hii mikubwa jambo ambalo litaongeza ushindani kwenye eneo la katikati ikiwa atacheza kwa kushirikiana na wachezaji wenzake.
MSIKIE PLUIJM
Kocha wa zamani wa Yanga na Singida Fountain Gate, Hans Van de Pluijm anasema mchezo kati ya miamba hiyo siku zote huwa hautabiriki kutokana na ugumu wake kwa sababu mtu mmoja anaweza kufanya jambo linaloweza kuleta faida au hasara kwenye timu.
“Huwa ni mchezo mkubwa na mgumu kwa kila timu ingawa ukiangalia kwa mwenendo wa Yanga kwa sasa unaweza kuipa ushindi japo ninachoamini atakayekuwa makini kwenye kutumia vizuri nafasi na kuepuka makosa ndiye atakayekuwa na faida zaidi.”
Post a Comment