Mashabiki wa Simba kwa sasa hawana kitu kingine wanachokifikiria zaidi ya mechi ijayo ya CAF. Kwa sasa wanahesabu siku, huku wakiwa na mzuka mwingi wa kutaka kuishuhudia timu hiyo ikiivaa Al Ahly ya Misri katika mechi ya mkondo wa kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hizo zitakutana kwa mara ya saba katika pambano hilo Ijumaa ijayo kuanzia saa 3:00 usiku, Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, huku nyota wawili wa kimataifa kutoka Zambia na Burundi, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza wakiachiwa msala wa mechi hiyo.
Simba na Al Ahly zilishakutana katika mechi sita tofauti za michuano ya CAF, huku kukiwa hakuna mbabe, kwani kila moja imeshinda mechi mbili za nyumbani na kupoteza ugenini kwa idadi kama hiyo, huku mbili nyingine za michuano ya African Football League zilizoisha kwa sare mbili tofauti.
Simba ililazimishwa sare ya 2-2 nyumbani kisha kwenda kutoka 1-1 ugenini robo fainali ya AFL na kutolewa kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini, japo Al Ahly ilienda kukwama mbele ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyobeba taji la michuano hiyo ikiichapa Wydad CA.
Mashabiki wa Simba wakiwa na hamu kubwa na kuamini timu hiyo safari hii itaing’oa Al Ahly ambao ni watetezi wa taji hilo, rekodi zinaonyesha Wekundu hao wanategemea uzoefu na umahiri wa viungo washambuliaji, Saido na Chama kuamua mechi hizo mbili kati ya Machi 29 na Aprili 5.
Ipo hivi. Rekodi na takwimu walizonazo nyota hao Simba vimewapa nafasi kubwa ya kubebeshwa msala wa kuamua matokeo kuanzia mechi ya kwanza ya Machi 29 ya nyumbani na ile ya marudiano. Saido ndiye mchezaji kinara wa Simba katika michuano hiyo akiwa na mabao mawili na asisti mbili akitumika katika mechi tano kati ya sita za makundi, lakini akiwa na bahati ya kuisumbua Al Ahly katika mechi za AFL, akiasisti bao la Sadio Kanoute katika sare ya mabao 2-2 Kwa Mkapa.
Kwa upande wa Chama aliyewahi kukutana na Al Ahly tangu mwaka 2016 katika makundi akiwa Zesco United ya Zambia kisha alipohamia Simba amekutana na kikosi hicho mara sita akihusika pia kutengeneza mabao matatu likiwamo lile liloizamisha Al Ahly 1-0 kwa Mkapa likiwekwa kimiani na Luis Miquissone.
Pia katika Ligi ya Afrika (AFL), Chama alitengeneza mawili katika kila mechi, moja akimsetia Kibu Denis na jingine Sadio Kanoute, huku rekodi zikionyesha katika makundi amefunga bao moja na kuasisti pia mara moja.
Saido katika mechi tano za Simba za makundi ametumika kwa dakika 421 na kukosa mchezo mmoja tu wa marudiano dhidi ya Wydad CA iliyolala 2-0 Kwa Mkapa, lakini katika mechi ya kufuzu robo alifunga na kuasisti katika ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Kwa Chama licha ya kutumika kwa dakika chache katika mechi tatu za awali za makundi, ila uzoefu wake uliibeba timu kutinga robo fainali kwa kufunga na kuasisti dhidi ya Jwaneng, huku akiwa ndiye kinara wa mchezo kwa kikosi akipata alama 9.5 kwa mujibu wa Flashscore akifuatiwa na Saido (9.3).
Mbali na nyota hao, lakini uwepo kwa Luis Miquissone, Kibu Denis, Sadio Kanoute na wakali wengine wamelipa benchi la ufundi amani, licha ya ukweli haitakuwa mechi ya kitoto kutokana na rekodi ilizonazo Al Ahly kila inapotinga robo fainali, kwani katika misimu mitano iliyopita ilipofika hatua hiyo, mara moja tu iliondoshwa na kushindwa kusonga mbele, lakini manne ikifika fainali.
Katika fainali nne alizocheza, Al Ahly ilipoteza moja tu mbele ya Wydad, lakini nyingine zote ilibeba taji ikiwamo ya msimu uliopita ilipoitambia Wamorocco hao na msimu wa 2018-2019 ndio ilikwama ikitolewa na Mamelodi iliyoenda kutolewa nusu fainali ya Wydad iliyopoteza fainali kwa Esperance ya Tunisia iliyobeba taji msimu huo.
Simba itaialika Al Ahly katika mechi ya kwanza Ijumaa ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa kisha kuifuata Cairo, Misri Aprili 5 na mshindi atakata tiketi ya nusu kusubiri mshindi wa mchezo kati ya Petro Atletico ys Angola au TP Mazembe.
Kocha Abedhak Benchikha kwa bahati nzuri anaijua Al Ahly nje ndani kwani alishakutana nao hivi karibuni akiwa na USM Alger ya Algeria katika mechi ya Super Cup, akiifunga 2-1.
WASIKIE WADAU
Nyota wa zamani wa kimataifa wa Simba aliyewahi kuwika pia Small Simba na Mtibwa, Dua Said alisema kikubwa kinachotakiwa uzoefu tu, jambo linalowaongezea Simba pointi ya kushinda na viungo hao wawili na kocha walionao. Aidha alisema, sio rahisi kwa Ahly kuchomoka kwani rekodi zao dhidi ya Simba zimekuwa ngumu wote wamekuwa wakionyeshana ubabe.
“Saido ni wazi amekuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Simba kwani katika mechi tatu atakupa tu bao na asisti na sitashangaa akifunga mchezo ujao,” alisema Dua na kuongeza;
“Chama ndio kabisa ameshika usukani na kama ningekuwa kocha angekuwemo katika kikosi cha kwanza ili Waarabu wapate joto la jiwe mapema, hakuna ugumu kama wataonyesha uwezo tunaoufahamu kwa Mkapa.”
Shabiki wa Simba na mchambuzi wa soka, Miraji Mara Moja alisema, mchezo utakuwa mgumu na unapowazungumzia hawa ni wachezaji wazoefu ambao wanawafahamu vizuri hao Waarabu kwa sababu ameshacheza nao zaidi ya mara sita na hata kwenye timu ya taifa amekuwa na mwendelezo mzuri.
“Ukiwaangalia wachezaji kama hawa ndio wanaohitajika ijapo ni maji ya jioni na hawa kina Chasambi (Ladack) wajifunze kitu na huwezi kuwaacha wazoefu hawa nje kwenye michezo kama hiyo na watakupa kitu.,” alisema Miraji na kuongeza;
“Hawa wachezaji hawatakiwi kupata majeraha kwenye mechi za timu ya taifa na wakiwepo lazima damu imwagike Kwa Mkapa japo tupo kwenye mfungo, kwani maandalizi na wachezaji wazoefu wanaongeza ukali wa ajabu sana ambao utawatesa Ahly.”
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
Post a Comment