Ni rasmi Mwanaspoti inajua kwamba Azam imegomea mapendekezo mawili ya staa wao, Prince Dube anayetaka kusitisha mkataba aondoke Chamazi.
Imegomea ofa ya mchezaji husika ambaye alitaka kurudisha lile dau la usajili walilompa mwaka jana, lakini vilevile mkwanja ambao klabu inayomuwinda kimyakimya iliyompa atoe kwa Azam.
Dube alitaka kuwapa Azam Dola 150,000 (takriban Sh382 milioni), lakini baadaye akapanda akawaambia atalipa Dola 200,000 sawa dau la usajili walilompa ambalo ni Sh510 milioni, ila yote hayo mawili yamekataliwa na klabu hiyo inayomiliki uwanja wa kisasa zaidi Afrika Mashariki na Kati.
Habari za ndani zinasema kwamba msimamo wa Bodi ya Wakurugenzi ni kwamba atoe Dola 300,000 (takriban Sh700 milioni) ambazo ni za makubaliano ya kimkataba unaomalizika 2026.
Habari zinasema kwamba Azam wameshashtukia kwamba kuna klabu moja ya Ligi Kuu Bara inayomuwinda kwa ajili ya msimu ujao, lakini inafanya mambo kimyakimya kwa vile staa huyo bado ni mwajiriwa wao halali.
Mmoja wa viongozi wa Azam ameiambia Mwanaspoti kuwa wanajua mchezo wote, lakini hawapo tayari kumzuia mchezaji huyo isipokuwa wanataka taratibu zifuatwe kwani hawakuwahi kuwa na tatizo naye mpaka wakati anakabidhi barua ya kuomba kuvunja mkataba.
Ihefu na Yanga zinatajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazomuwinda Dube kwenye Ligi Kuu Bara ingawa pia kuna timu za Zimbabwe.
IHEFU
Ihefu kumnasa Dube inaweza kuwa ajabu, lakini bado ni kwa asilimia ndogo. Wamiliki wapya wa Ihefu wanataka kumnasa mchezaji huyo kwa gharama yoyote wakiamini atawasaidia kurahisisha safari ya mafanikio.
Kwa mujibu wa habari za ndani kutoka kwa watu wa karibu na Dube, mabosi wa Ihefu ambao zamani walikuwa wakimiliki Klabu ya Singida United iliyopanda daraja mwaka 2017, walitaka kumsajili wakati ule sambamba na Tafadzwa Kutinyu.
Lakini, Dube alichagua kwenda Afrika Kusini ambako hata hivyo hakufanikiwa na kuamua kurudi Zimbabwe.
Lakini sasa wakiwa na timu mpya, mabosi walewale wamerejea tena kwake na kuivuruga akili yake kwa ‘mzigo mrefu’ waliomuwekea mezani. Hata hivyo Yanga bado imemuingia zaidi akilini.
YANGA
Inatajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazomhitaji zaidi staa huyo wa Zimbabwe na hata mwenyewe amewaambia marafiki zake yupo tayari. Yanga wanaamini Dube anaweza kuwa mtu sahihi wa kuziba nafasi ya Fiston Mayele.
Inaaminika kwamba Yanga wamekuwa wakihangaika kumshawishi mchezaji huyo kwa muda mrefu kutua katika kikosi hicho kutokana na uwezo wake.
Hivi karibuni wakati Azam FC ikiwa mikoani kwa mechi za Ligi Kuu, Dube alionekana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa akishuhudia mechi ya Yanga ambapo ilishinda mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad.
Dube hakusafiri na Azam kwa sababu ni majeruhi ambapo amekosa michezo kadhaa hadi sasa.
Nyota huyo hajacheza mechi ya Azam FC tangu Februari 19 alipoingia kipindi cha pili dhidi ya Tabora United.
Hakusafiri na timu katika mechi mbili za mikoani - Mbeya dhidi ya Tanzania Prisons na Mwanza dhidi ya Singida Fountain Gate.
Lakini, Mwanaspoti inajua kwa kawaida Azam FC husafiri na wachezaji wake hata kama ni majeruhi kama sehemu ya kujenga umoja. Hata hivyo Dube hakusafiri ikisemekana alikataa kama sehemu ya shinikizo ili aachwe huru.
Habari za ndani ni kwamba inasemekana kuna mfanyakazi mmoja wa Yanga ambaye hapo kabla alikuwa Azam ndiye anayechora ramani ya Dube kuhamia Yanga na klabu hiyo ina uhakika kwamba, ishu itakwenda kirahisi kwani staa huyo ameshaanza ‘kuingia kwenye mfumo’.
NYUMBANI ZIMBABWE
Habari kutoka Zimbabwe zinasema timu mbili nchini humo zinapigana vikumbo kumrudisha kijana wao.
Mwanaspoti inaijua Highlanders FC, timu aliyokulia Dube ambayo kwa sasa ina wamiliki wapya wenye ‘mpunga mrefu’ wangependa kumrudisha nyota wao huyo kipenzi cha mashabiki.
Pia klabu ya Yadah FC ambayo hivi karibuni ilinasa saini ya nyota Khama Billiat iko katika harakati za kumnasa Dube. Timu hizo mbili zinaitesa akili ya Dube, lakini Yanga wanazicheki tu.
Lakini, taarifa nyingine zinasema Dube anaamini majeraha yanayomuandama pale Chamazi yanatokana na mambo ya nje ya uwanja, hivyo anataka kuondoka ili kujiepusha nayo.
Mchezaji huyo alijiunga na Azam FC 2020 akitokea Highlanders ya Zimbabwe - timu yake ya utotoni. Aliyaanza maisha ya Chamazi kwa furaha kabla hajaumia kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Novemba 25, 2020 na tangu hapo hakurudi kuwa Dube wa kabla ya kuumia.
Msimu huu pekee ameshakosa mechi zaidi ya tano kutokana na majeraha ambayo hadi sasa yanamuweka nje. Hata hivyo, kwa mujibu wa chanzo chetu ni kwamba kwa sasa hataki hata kurudi Chamazi akilazimisha kuondoka.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema Dube anatarajiwa kujiunga na timu hiyo wiki ijayo na kwamba, mchezaji huyo ana mkataba nao hadi mwaka 2026.
Hadi sasa Dube amecheza dakika 734 katika jumla ya dakika 1710 za mechi 19 za Azam FC msimu huu. Dakika alizocheza ni katika mechi 12, huku akikosa mechi saba katika mechi 19 za msimu.
Kwa kifupi ni kwamba Dube amecheza chini ya nusu ya dakika za jumla kama angecheza mechi zote msimu huu na hii ni kutokana na pancha za hapa na pale ambazo kimsingi zimekuwa zikimuandama katika misimu yote.
Katika dakika hizo 734 za mechi 12 ambazo amecheza amefunga mabao saba na kutoa pasi mbili za mabao. Mkataba wa Dube na Azam FC unatarajiwa kumalizika ifikapo Juni 2026, ikiwa na maana kwamba bado ana misimu miwili na nusu mbele.
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPAz
Post a Comment