Kocha Mkuu wa Young Africans SC, Miguel Gamondi, amesema katika mchezo wa kesho Jumatatu dhidi ya Ihefu, atahakikisha yale yaliyotokea mzunguko wa kwanza, hayajirudii zaidi ya kuondoka na ushindi.
Kauli ya Gamondi imekuja ikiwa kesho Jumatatu, timu yetu ya Young Africans SC itakuwa mwenyeji wa Ihefu katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 12:00 jioni.
Kuhusu maandalizi ya mchezo huo, Gamondi amesema: “Unajua tumecheza Ijumaa, maandalizi hayajawa makubwa sana, jana tulifanya mazoezi na baadhi ya wachezaji, leo tutafanya tena mazoezi, tulikuwa na safari ndefu, kwetu sisi kila mechi ni muhimu sana, tunajaribu kujiandaa vizuri.
“Mipango yangu kwa sasa kuwafanya wachezaji kurudi kwenye hali zao, kama unavyojua Ijumaa tuliwakosa wachezaji sita muhimu, Aucho (Khalid) hatakuwepo kwa sababu amefanyiwa upasuaji mdogo, wengine nadhani wapo vizuri.”
Katika hatua nyingine, Gamondi amebainisha kwamba, baada ya kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza ugenini dhidi ya Ihefu kwa magoli 2-1, Kesho Jumatatu ni siku ya kurekebisha makosa hayo.
“Yaliyopita siku zote nasema ni historia, (Ihefu) ndiyo timu pekee iliyotufunga kwenye ligi, kesho tuna muda mzuri zaidi wa kurekebisha kile tulichopoteza, tutafanya kila liwezekanalo ili kuwafunga na kucheza mchezo mzuri.
“Ninawaheshimu sana Ihefu hasa katika mechi zao tano za mwisho wamebadilika sana, wana wachezaji wenye vipaji, naamini itakuwa mechi nzuri.
“Kitu muhimu zaidi kwangu, mpira wa miguu ni mchezo wa kutengeneza nafasi, nadhani kuzuia ni rahisi, kama ukiwa kocha na kuwafanya wachezaji wako kuwa nyuma ya mpira wewe utakuwa ni kocha wa kuzuia.
“Ninajivunia wachezaji nilionao ni wazuri, ukiangalia kiwango tunafunga magoli manne, matatu, hiyo siyo mbaya, sidhani kama kuna timu inafunga kama sisi.
“Wananchi waje kwa wingi kutusapoti, binafsi nataka kuona tunashinda mechi hii kwa sababu sipendi kupoteza, lakini Wananchi ni watu muhimu, siku zote nimekuwa nikisema wao ni mchezaji wa 12.
“Ninaamini watakuja kwa wingi kesho Chamazi na najua wanategemea makubwa kutoka kwetu kucheza soka zuri, kupambana hadi dakika ya mwisho, hakuna kukata tamaa, hiyo ni ahadi ninayowapa, siwezi kuwaahidi ushindi, ninawaahidi kucheza vizuri na kutokata tamaa hadi mwisho.
“Tuna tahadhari, tumeifanyia utafiti Ihefu, kila timu ina udhaifu na ubora wake, kwetu inabaki kuwa siri, kama kocha siwezi kusema tunakwenda kufanya nini, lakini tutakuwa imara, tutamiliki mpira, tutatengeneza nafasi na kuuweka mpira kwenye nyavu,” alisema Gamondi.
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
Post a Comment