Miezi michache iliyopita Clatous Chama alikalia kuti kavu katika kikosi cha Simba, kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu uliomfanya asimamishwe kwa muda usiojulikana kabla ya kwenda fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika Ivory Coast akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Zambia.
Hata hivyo, kiungo mshambuliaji huyo alimalizana na mabosi wa klabu hiyo akiwamo Kocha Abdelhak Benchikha na kupiga kazi kwelikweli, kiasi cha kuzima hata zile kelele za mashabiki wa klabu hiyo waliotaka atemwe kabisa kikosoni.
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
Katika kuonyesha Chama ni kama amezaliwa upya, nyota huyo juzi usiku alioupiga mwingi kiasi cha kumfanya kocha Benchikha ashindwe kujizuia na kumwagia sifa kwa kiwango alichokionyesha kilichoisaidia Simba kuungan a na Yanga kwenye robo fainali na kuandika historia mpya Afrika ya Tanzania kuingia timu mbili kwa mpigo Ligi ya Mabingwa.
Chama alitembeza boli la kiwango cha juu wakati Simba ikiifyatua Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa mabao 6-0 katika mechi ya mwisho ya Kundi B na kumaliza nafsi ya pili ikiwa na pointi tisa, mbili pungufu na ilizovuna vinara wa kundi hilo Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Katika mchezo huo, Chama aliwavuruga wageni akiifanya Simba iwe hatari eneo la mwisho la ushambuliaji akiwa ndiye aliyeingia mara nyingi zaidi katika eneo la penalti la Jwaneng Galaxy, akifanya hivyo mara mane kuliko mchezaji yeyote ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
“Chama ni mchezaji hatari zaidi katika kukabiliana na mtu kwa mtu (one against one), na alichofanya leo (juzi) ni maajabu na kile ambacho mnakiona kutoka kwake ni kidogo katika uwezo mkubwa alionao. Ninyi bado hamjamuona Chama mwenyewe...,” alisema Benchikha.
Post a Comment