Uongozi wa Simba umesema umejipanga kisawasawa kwenye mikakati ya kumsaidia Kocha Abdelhak Benchikha kutaka kuimaliza mechi ya robo fainali dakika 90 ya mchezo wa kwanza uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Uongozi huo umesema, mikakati ya benchi la ufundi linaloongozwa la Kocha Benchikha kutaka kumaliza mechi ya robo fainali nyumbani kwa kupata mabao mengi, hivyo nao kama viongozi wameungana nao kwa kumpa kila anachohitaji kwa ajili ya kuhakikisha Wamisri wanakufa Machi 29.
Simba itakuwa na kibarua kigumu Ijumaa ya Machi 29, mwaka huu katika mcheso wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaochezwa kwenye uwanja wa huo saa 3:00 usiku.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema mipango ya Benchikha kuhitaji ushindi mnono katika dakika 90 za mchezo wa kwanza ili kumaliza kiu yao ya kutaka ushindi mkubwa ambao utawapeleka nusu fainali.
Amesema wanahitaji ushindi mkubwa dhidi ya Al Ahly ambapo benchi la ufundi linaendelea kukinoa kikosi kufikia malengo hayo kwa sababu matokeo ya idadi kubwa ya mabao yatakuwa faida kubwa kwao na mechi ya marudiano kuwa rahisi.
“Hii ni mechi muhimu sana Wanasimba, Kocha Benchikha anaendelea kukisuka kikosi kuwa imara , kikosi kimeenda visiwani Zanzibar kwa siku nane kwa ajili ya maandalizi maalum na visiwani humo ni sehemu nzuri kwa sababu ya kupata muda wa kufanya program yake mara mbili kwa siku,” amesema Ahmed.
Amesema mechi dhidi ya Al Al Ahly itachezwa Ijumaa Machi 29, mwaka huu saa 3:00, muda umezingatia maslahi mapana ya imani ya dini zote imezingatiwa kwa kuwapa nafasi ya mashabiki kuangalia mechi hiyo wakiwa tayari wameshafungulia.
“Kwa ukubwa tuliokuwa nao Simba hatuna wasiwasi na muda wowote ambao tutapangiwa kucheza, kikosi chetu kipo tayari kucheza muda huu na tumedhamilia kumfanya vibaya Al Ahly.
Hatuna mashaka na muda kwa sababu tuliwahi kucheza na Jendamarine Saa 4 usiku na tukapata matokeo mazuri, tunaimani mechi ya Ijumaa Al Ahl hawezi kutoka kwa sababu maandalizi yanayofanyia niwahakikishie hawezi kutoka kwa Mkapa,” amesema Ahmed.
Ametaja waamuzi wa mchezo huo kati atakuwa Abongile Tom akisaidiwa na Zakhele Thusi wote wawili wakitokea Afrika Kusini, Dimbiniaina Andria Tianarivelo (Madagascar) na Jelly Afred (Afrika Kusini).
“Tunaenda kucheza na Al Ahly ni mechi ngumu sana ni robo fainali ya tano katika michuano ya CAF hili sio jambo dogo tumekuwa na muendelezo mzuri, sasa tumechoka hatua hiyo na tunahitaji nusu fainali.
Safari hii hatuna cha kusikiliza wala kusikia zaidi ya nusu robo fainali ya mwisho dhidi ya Wydad Casablanca walituondoa kwa mikwaju ya penalti, safari hii ya tano hatutakuwa tayari kuona tunapoteza kama ilivyokuwa awali,” amesema Ahmad.
Ameongeza kuwa hakuna mjadala mwingine uliopo ndani ya Simba zaidi ya timu hiyo kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Al Ahly, wanahitaji kwenda kucheza nusu fainali.
“Katika mchezo huo tunaenda na kauli mbiu yetu ya ‘Tunaitaka Nusu Fainali’, robo fainali nne zilizopita zimetuimarisha na sasa tunaenda kupambana na Al Ahly kutafuta tiketi ya kwenda kucheza nusu fainali,” amesema Ahmed.
Ameeleza kuwa licha ya kutaka nusu fainali lakini hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu wanaenda kucheza na mpinzani mgumu sana na mwenye ubora lakini safari hii wamedhamilia kusaka tiketi hiyo kwa kuhakikisha wanamfunga Al Ahly uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Kuna watu wanasema Al Ahly wanapofika katika hatua hizi anabadilika na anakuwa tofauti anavyocheza kwenye makundi, tunachoweza kuwaeleza hao wanaosema wapinzani wetu wanabadilika kuwa hata sisi Simba tunabadilika naye.
Hii ni vita kubwa tunahitaji kupambana kweli kweli na ushirikiano mkubwa kuhakikisha tunashinda vita hii na mipango yetu ni kumaliza hii mechi hapa hapa Benjamin Mkapa,” amesema Ahmed.
Ameeleza kuwa kama watasimama imara, sawa sawa kuunganisha nguvu hakuna wa kumzuia Simba katika uwanja wa Mkapa ambapo wanahitaji kumaliza mchezo nyumbani.
Amesema Al Ahly watawasili nchini Machi 27, mwaka huu na viingilio ni Shilling mzunguko ni 5000, machingwa ni 10,000, VIP C 20, 000, B 30,000, A 40,0000, Platinum 200,000 na Tanzanite ni 250, 000 wanaamini viingili ni rafiki sana kwa mashabiki kununua na kujitokeza kwa wingi uwanjani .
Ahmed amesema wako kwenye mazungumzo na Jeshi la polisi la watu wa usalama barabarani kuwepo na magari sehemu mbalimbali kufika kila sehemu kuweza kusafirisha watu wanaotaka kwenda uwanjani kwa usalama.
Amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kuzingatia tangazo la Serikali kuwa upande wa timu pinzani na kusimama na timu yao ikiwemo kuvaa jezi za klabu yao na sio kwenda kuwapokea wageni hali ambayo sio utamaduni wao.
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
Post a Comment