Wakati wapinzani wa Simba SC na Young Africans kwenye hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly na Mamelodi wakitarajiwa kutua nchini leo Jumatano (Machi 27) tayari kwa mechi zitakazopigwa ljumaa na Jumamosi, taarifa zimeeleza kuwa vikosi vyao vinakabiliwa na wimbi kubwa la majeruhi.
Simba SC itaikaribisha Al Ahly ya Misri katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Keshokutwa ljumaa (Machi 29) kabla ya kesho yake, Jumamosi (Machi 30) Young Africans kuwa mwenyeji wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini uwanjani hapo.
Kuelekea mechi hizo kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari Misri na Afrika Kusini, wachezaji majeruhi kwa upande wa Al Ahly ni kiungo mshambuliaji Allou Dieng anayeuguza goti, Mlinda Lango Mohamed El Shenawy, mwenye majeraha ya bega, na kiungo mkabaji Emam Ashour aliyeumia bega wote wakiwa ni wa kikosi cha kwanza.
Kwa upande wa Mamelodi Sundowns, imeripotiwa kuwa kiungo mshambulaji Muargentina Junior Leandro Mendieta, Mlinda Lango tegemeo, Ronwen Williams, Thapelo Maseko pamoja na Teboho Mokoena ni majeruhi, huku kiungo mshambuliaji Themba Zwane akiukosa mchezo huo kutokana na kadi tatu za njano, lakini pia imeelezwa naye ni majeruhu.
Hata hivyo, habari nzuri kwa Mamelodi ni kwamba wachezaji wengine majeruhi wamepata nafuu, nao ni Mothobi Mvama Khuliso Mudau.
Uongozi wa Simba SC umesema umeandaa silaha mbili zitakazoisaidia timu yao kufikia malengo yao ya kufanya vizuri na kutinga Nusu Fainali msimu huu 2023/24.
Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Imani Kajula, ameweka wazi kuwa silaha hizo kuwa ni kutilia maanani matakwa ya Benchi la Ufundi linaloongozwa na Abdelhak Benchikha pamoja na wachezaji, lakini na mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani.
Kajula amesema kwa misimu kadhaa Simba SC imekuwa ikiishia hatua ya Robo Fainali, lakini wamefanya majaribio ya makusudi na mahususi kwa safari hii kwenda Nusu Fainali.
Amesema majaribo hayo ni kuandaa silaha hizo ikiwamo kumsikiliza Benchikha mahitaji yake kwa kupata mazingira mazuri ya kambi kwa timu kujichimbia visiwani Zanzibar kwa ajili maandalizi ya mchezo huo na silaha nyingine ni mashabiki ambao wamekuwa wakiisapoti timu wakati wote.
“Timu ilipokuwa Zanzibar tulipata mechi ya kirafiki ambayo imetupa maandalizi mazuri sana, kocha imempa ufundi, kuona madhaifu ya kikosi chake pamoja na wale waliopo Taifa Stars kurejea na kuungana na wenzao, Chama (Clatous) na wengine watarudi muda wowote kuanzia leo Jumatano (Machi 27) na kuungana na timu kambini.
“Tunaiheshimu Al Ahly ni timu bora, lakini tukumbuke tumekutana nao katika Robo Fainali ya African Football League (AFL), na kutuondoa kikanuni, pasi na shaka kila mmoja wetu tunajua hilo, lakini tunahitaji kutumia uwanja wa nyumbani kutafuta ushindi mnono ambao tutawatoa wapinzani hapa nyumbani” amesema Kajula.
Kwa upande wa Young Africans, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kuwa, baada ya kujichimbia kambini kwa muda, kocha Gamondi amewahakikishia kuwa kikosi hicho tayari kimeiva kwa ajili ya mchezo huo wa Robo Fainali, hivyo kuwa na uhakika wa kufanya vema katika mechi ya kwanza itakayochezwa Jumamosi (Machi 30), Uwanja wa Banjamin Mkapa, Dar es salaam.
Ofisa habari huyo amesema wana imani ya kupata ushindi katika mchezo wa kwanza kwa sababu wapinzani wao pia wana baadhi ya wachezaji ambao hawatocheza kwa kuwa majeruhi na adhabu kikanuni.
“Niwaibie tu siri Wanayanga kuwa hata Mamelodi pia wana wachezaji wao ambao ni majeruhi na wengine ambao hawatocheza mechi hiyo kutokana na kuwa na kadi tatu za njano, kwa hiyo wasiwe na wasiwasi, tutatumia udhaifu huo kuwashangaza,” amesema Kamwe.
PATA GB 30 KILA MTANDAO BURE HAPA
Post a Comment