Simba itafuzu robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika pasipo kutegemea matokeo ya timu nyingine ikiwa itaibuka na ushindi wa aina yoyote katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Jwaneng Galaxy itakayochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Machi 02 mwaka huu.
Sare tasa iliyopata dhidi ya Asec Mimosas ugenini huko Ivory Coast jana, imeifanya Simba kufikisha pointi sita na hivyo kama itaifunga Jwaneng Galaxy, itakuwa na pointi tisa ambazo zitatosha kuipeleka robo fainali, ikiungana na Asec Mimosas ambayo imeshakata tiketi tayari baada ya kufikisha pointi 11 na kujihakikishia uongozi wa kundi B.
Matokeo yoyote ya mechi kati ya Jwaneng Galaxy na Wydad jana hayatoweza kuizuia Simba kwenda robo fainali ikiwa itapata ushindi katika mechi yake ya mwisho ya kundi.
Jwaneng Galaxy haitoweza kuzifikia pointi hizo tisa kwani ikifungwa itabakia na pointi ilizokuwa nazo baada ya mechi ya jana ambayo kabla haijacheza ilikuwa na pointi nne.
Wydad hata kama jana ilipata ushindi na pia ikashinda mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Asec Mimosas, itamaliza ikiwan na pointi tisa sawa na wawakilishi hao wa Tanzania lakini Simba itabebwa na kigezo cha kwanza kinachotazamwa kuamua mshindi kwa timu mbili zilizolingana pointi ambacho ni matokeo ya mechi mbili baina yao.
Simba inabebwa na matokeo mazuri iliyopata katika mechi mbili dhidi ya Wydad kwenye kundi hilo kwani, mechi ya kwanza ugenini ilipoteza kwa bao 1-0 na ikapata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.
Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa baada ya sare ya juzi, nguvu zao wanazielekeza katika mechi ya Jwaneng Galaxy.
"Alhamdullilah tumepata tulichokihitaji. Sasa kazi imebaki mikononi mwetu Wana Simba March 02 dhidi ya Jwaneng, Hiyo ni mechi ya kuipeleka timu yetu Robo Fainali," alisema Ahmed Ally.
Kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin alisema kuwa watahakikisha wanapata ushindi nyumbani ambao utawapeleka hatua ya robo fainali.
"Sare sio matokeo mabaya na wala sio matokeo mazuri ambayo tumepata. Pointi moja kwetu sio haba. Tunarudi nyumbani kujipanga kwa mechi hiyo inayokuja dhidi ya Galaxy (Jwaneng).
"Wanasimba wajitokeze kwa wingi kuja kutusapoti kwani ni mechi ya kwenda kuweka rekodi nyingine ya kuingia robo fainali. Waliwahi kutufunga nyumbani lakini safari hii haitotokea. Tutapambana tuweze kwenda robo fainali," alisema Mzamiru.
Ikiwa Simba itatinga robo fainali, itakuwa ni kama marudio ya msimu uliopita ambapo iliingia hatua hiyo licha ya kuanza vibaya mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ambapo ilifungwa na Horoya kisha Raja Casablanca lakini ikapata pointi tisa katika mechi zilizofuata na kwenda mbele.
Msimu huu, Simba ilianza hatua ya makundi kwa kutoka sare katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy lakini imefanikiwa kuvuna pointi nne katika mechi tatu zilizofuata.
Post a Comment