Yanga ya Gamondi inavyomtesa Robertinho Simba

 Yanga ya Gamondi inavyomtesa Robertinho Simba

Pata 50,000 BURE Kila Siku Bonyeza HAPA


Ajira Mpya zilizotangazwa leo Bonyeza HAPA


Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA

Simba kwa sasa hawana raha. Wanachama na wapenzi wa klabu hiyo na hata baadhi ya viongozi wanatamani wamteme Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’. Wanaona kama anawazingua kwa sasa.


Ni kweli timu inapata matokeo mazuri uwanjani, lakini haiwafurahishi wanasimba kwa aina ya soka inayocheza uwanjani.


Kitu cha ajabu ni kwamba rekodi na namba zinambeba kocha huyo Mbrazili. Hajapoteza mchezo wowote wa Ligi kuu Bara tangu alipotua kikosini msimu uliopita.


Kocha huyo ameiongoza Simba kucheza mechi 15 hadi sasa, zikiwamo 11 za msimu uliopita na tano za msimu huu. Kwenye mechi za kimataifa kwa msimu huu haijapoteza mchezo wowote.


Pia katoka kuipa timu hiyo taji kwa kutwaa Ngao ya Jamii, iliyokuwa inashikiliwa kwa misimu miwili mfululizo na watani wao, Yanga. Iliifunga Yanga kwa penalti kwenye fainali kali iliyopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Oktoba 13.


Huo ulikuwa ushindi wa pili mfululizo kwa Robertinho mbele ya Yanga kwenye mechi za mashindano akiwa na Simba. Aliitungua kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita kwa mabao 2-0 na kufuta unyonge uliokuwapo ambapo Simba tangu ilipoifunga mara ya mwisho Yanga Februari 16, 2019.


Kelele zote za kutaka kocha huyo atimuliwe zimetokana na sare ya 1-1 na Power Dynamos ya Zambia kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Awali Simba ililazimishwa sare ya 2-2 ugenini mjini Ndola, Zambia na hivyo matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3 na Simba kuvuka kwenda makundi ya michuano hiyo kwa kanuni ya bao la ugenini.

Pata 50,000 BURE Kila Siku Bonyeza HAPA


Ajira Mpya zilizotangazwa leo Bonyeza HAPA


Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA


Simba imefuzu makundi ya michuano ya Afrika kwa mara ya sita, zikiwamo tano za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho, ndiye baba lao hapa nchini.


UKWELI ULIVYO


Katika Ligi Kuu Bara nako haipo pabaya, kwani ni kati ya timu tatu pekee zilizoshinda mechi zao kwa asilimia 100, sambamba na vinara Yanga na Azam FC.


Hata hivyo, kelele zinaendelea kwamba Robertinho atimuliwe, ili Juma Mgunda aliyewahi kuinoa timu hiyo arudishwe kikosini, ajabu.


Inashangaza kidogo kwa timu yenye malengo ya kutaka kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuutema misimu mitatu iliyopita, inataka kuishi kwenye dunia hii ya kutimua kocha bila sababu.


Ila kinachoonekana kuisumbua Simba na kuiumiza roho ni kule kutaka kujilinganisha na watani zao Yanga.


Kuna maeneo kadhaa ambayo Simba itapata shida sana kama itataka kuishi kama watani wao hao. Hata wao Yanga miaka saba nyuma iliyopita ilipata tabu hiyo hiyo inayoipata Simba kwa sasa.


Nayo ilikuwa ikiishi kwenye kivuli cha Simba iliyokuwa imesheheni nyota waliodumu pamoja muda mrefu, kocha mzuri na uwezo mkubwa kiuchumi uliowapa utulivu wachezaji wake.


Ile neema iliyokuwa Simba miaka hiyo, ndio imehamia Yanga kwa sasa. Ndio maana unaona Simba inateseka. Kama Simba haitashtuka itataabika sana nyuma ya kivuli cha Yanga.


Tuanze na kikosi kilichopo Simba kulinganisha na kile cha Yanga. Simba ukiondoa mabeki wa pembeni, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kipa Aishi Manula, Clatous Chama, John Boccco na nyota wachache, wachezaji wa idara nyingine wanaounda kikosi cha kwanza ni wageni. Fondoh Che Malone, Fabrice Ngoma, Willy Onana, Luis Miquissone ni wageni, hata kama Luis alishacheza misimu miwili iliyopita.


Kuna wachezaji kama Ayoub Lakred, Aubin Kramo, Shaaban Idd Chilunda, Hussein Kazi, Abdallah Khamis na wengine hawana muda mrefu kikosini.


Kibaya zaidi ni kwamba Simba ilienda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya Uturuki kwa mafungu. Wachezaji wengi walipishana kambini, hata kocha Robertinho, naye alitimka kambini kwenda kwao Brazil. Kifupi ni kwamba Simba ilikuwa na ‘pre season’ ya kuungaunga.


Iangalie Yanga sasa. Wachezaji walio wengi ni wale waliopo kwa zaidi ya msimu mmoja, hata kama kuna maingizo mapya ya kina Yao Kouassi, Gift Fred, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Nickson Kibabage na Hafiz Konkoni, bado ni watu wenye uwezo mkubwa kulinganisha na wale waliopo Simba.


TATIZO LIPO HAPA


Kambi ya Yanga iliwekwa Avic Kigamboni, jijini Dar es Salaam kwa msimu wa pili mfululizo, ikianza kwa wakati na kupata muda mrefu kwa wachezaji kuzoeana na kucheza kwa ushirikiano mkubwa, tofauti na ilivyo kwa Simba.


Pia timu nzima ina utulivu wa akili kwa sasa! Ubora wa kikosi chao, kwa mchezaji mmoja mmoja huwezi kulinganisha na wale waliopo Simba. Hata wachezaji wapya waliopo Yanga wameongezwa kwenye maeneo yaliyokuwa na upungufu na kuhitajika mtu wa kuziba. Halafu ni wenye uwezo mkubwa kisoka.


Lakini kubwa linaloiibeba Yanga ni kuwa na kikosi cha muda mrefu na chenye morali. Simba ya sasa bado haijakaa sawa, lakini mashabiki, wanachama na hata viongozi wake wanataka ikimbie mwendo wa Yanga. Hapa ndipo wanapokosea.


Hata nyumbani ukitaka mwanao aanguke, penda kumlinganisha na mtoto wa jirani. Kutoka Zoran Maki, Juma Mgunda hadi Robertinho, wachezaji hawajapata muda wa kukariri mifumo ya makocha hao kwa vile wanabadilishwa ndani ya muda mchache.


Simba isiumizwe na aina ya soka linalopigwa Yanga kwa sasa kwa sababu kocha Nasreddine Nabi aliyekaa na timu hiyo kwa miaka miwili na nusu aliweka misingi ambayo imekuja kuendelezwa na Miguel Gamondi. Wachezaji walioifikisha Yanga fainali za Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita sehemu kubwa wapo kikosini kwa sasa na wameongezewa nguvu na nyota wazoefu wa mechi za kimataifa kama kina Maxi Nzengeli, Pacome na Yao Kouassi.


Kama Simba itaendelea kujipima kwa kujilinganisha na Yanga, ijue mapema itaumia sana. Yanga ipo dunia nyingine kulinganisha na Simba. Hata uwanjani unaweza kuona timu hiyo inavyocheza. Simba inapaswa kukubali ukweli kwamba timu yao inahitaji muda mrefu kujijenga kwa vile haikupata muda wa kujijenga mapema kambini Uturuki.


Simba inaonekana kucheza hovyo kwa sasa kwa vile haikupata muda mzuri wa kujifua na wachezaji kuzoeana kwenye pre season na mbaya michuano ipo karibu karibu mno.


ROBERTINHO MJANJA


Kitu cha kuheshimu ni mbinu za kocha Robertinho kumbeba mbele ya wapinzani wao, kuanzia ilipovaana na Singida Big Stars na Yanga kwenye Ngao ya Jamii. Yanga inayosifika kwa soka tamu, ilishindwa kuitungua Simba na kuishia kutema Ngao kwa mikwaju ya penalti 3-1.


Katika Ligi Kuu Bara ilianza kwa ushindi wa mabao 4-2 kwa Mtibwa Sugar, kisha ikashinda 2-0 mbele ya Dodoma Jiji na kumalizana na Coastal Union kwa kuifumua mabao 3-0.


Katika mechi nane tofauti za mashindano, Simba imeruhusu mabao sita tu, huku yenyewe ikifunga jumla ya mabao 14, ni mechi mbili tu ambazo haikufunga mabao kwenye dakika 90 za kawaida.


Pamoja na namba hizo kumbeba Robertinho, lakini Wanasimba bado wanamkomalia kocha huyo apigwe chini kwa vile tu wanasumbuliwa na kivuli cha soka linalopigwa na Yanga kwa sasa.


Kama ambavyo Yanga ilitaabika kwa misimu kadhaa wakati Simba ikiwa bora kwa tabia ya kupuna wachezaji na kubadilisha makocha hovyo, ndivyo sasa inaisumbua Simba.


Jinamizi hilo kwa sasa naliona sasa likihamia Simba na kama hawatazinduka, watapigishwa mswaki miaka mingine zaidi baada ya misimu miwili mfululizo kuwa wapenzi wasindikizaji katika Ligi Kuu.


Hakuna siri katika kikosi cha sasa cha Simba kina baadhi ya wachezaji ambao ni kama zali liliwapata kuwepo Msimbazi, kwani uwezo wao uwanjani ni mdogo na hawana msaada kulinganisha na usajili wao ulivyokuwa.


Hata hivyo, pupa ya kutaka timu ipate mafanikio kwa haraka bila kuwapa muda wa kutengeneza muunganiko imechangia kuwaangusha makocha na hata wachezaji wengine wazuri ndani ya kikosi hicho na kuonekana hawafai kwa sasa. Huenda mambo yakaendelea kuwa hivyo hivyo hata kama Robertinho atatimuliwa na kuletwa kocha mpya, kwa vile mabosi wa Msimbazi wanakwepa kushughulika na ukweli juu ya maandalizi ya kikosi hicho na kukubali kutaka kuingizwa mkenge na mashabiki ambao wengi wao hawajui hata timu inaandaliwaje. Lakini kumbuka, Simba inaongoza ligi ikiwa haijapoteza wala kutoka sare kwenye michezo mitano, timu pekee kwenye ligi yenye ushindi asilimia 100.


Chanzo: Mwanaspoti

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post