No title

 


Lofa wa Zanzibar

Na HADITHI NYINGINE 



 

                     John Wisse


 

Darohn 5 Press Tanzania Ltd,

P.O.BOX 21345, DAR ES SALAAM, TANZANIA.

 

 

Darohn 5 Press Uganda Ltd,

P.O.BOX 32453, JINJA ROAD-BC657, UGANDA.

 

Darohn 5 Press Kenya Ltd,

Mombasa Road,

P.O.BOX 21345, NAIROBI, KENYA.

 

 

 

ISBN: 978-9987-9836-0-3 

Riwaya 

 

 

 

© 2019, John Wisse

 

 

Chapa ya kwanza, 2019

 

 



Haki zote zimehifadhiwa, hairuhusiwi kuiga, kupiga chapa, kutafsiri au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi yoyote ile bila idhini ya maandishi kutoka kwa Darohn 5 Press Tanzania Ltd.

 

Wachapaji ni

Info tech, Malaysia

 

Yaliyomo 

 

 

Lofa wa Zanzibar ------------------------------------- 4

 

 

Anguko la Ubaya-------------------------------------- 36

 

 

Nyota Nyeusi ------------------------------------------65

 

 

Chaupele -----------------------------------------------84




 

 

MAISHA YA BINADAMU yamejaa pingamizi nyingi; kila mmoja anao mtihani wake ambao huupitia ili kufika mahali atakapo. Japo ipo mitihani mingi katika maisha, wapo wachache ambao hufaulu na kuyaishi maisha ya furaha japo karaha huwa haikosi. Walio wengi hujaribu sana kuviruka vikwazo ili waangukie kwenye nuru na mahali watakapoyafaidi maisha, lakini badala yake huangukia katika shida ama dhiki zaidi. 

Maisha hayatabiriki!

Nusura, msichana mdogo kiumri, miaka kumi na miwili, alikuwa mmoja wa waliokuwa na ndoto za kuyapata maisha bora. Akiwa na wazazi wake wote alijua hataipoteza njia ya mafanikio kwa kusoma na kuutokomeza ujinga. Aliota kuwa siku moja atakuja kuwa afisa serikalini ambako angeitumikia nchi yake pia naye ajipatie mahitaji yake muhimu. Hiyo ilikuwa tamaa ya moyo alioubeba msichana mdogo, Nusura.

Akiwa darasa la sita, ungali bado mwaka mmoja tu aingie darasa la saba na kuitwa mhitimu, baba yake alifariki. Kufariki kwa baba yake, Bwana Haroub kulikuwa kwa ghafla mno. Ajali ya gari alilokuwa kalinunua baada ya miaka mingi ya kujinyima riziki na familia yake ndilo lilimtoa uhai siku ya pili tu tangu alitoe bandarini.

Kifo cha Bwana Haroub hakikufika peke yake kama yatima. La hasha! Kilikuja na mengine pia—ikiwemo kuutwaa uhai wa kaka yake Nusura, ambaye aliitwa Ibrahim, msomi aliyekuwa akifanya kazi kwenye mamlaka ya bandari upande wa Unguja. Siku ya vifo hivyo viwili vya ghafla Haroub alikuwa akiliendesha gari lake kwa mara ya kwanza tangu alimiliki. Pembeni yake alikuwepo mwanaye ambaye ni Ibrahim akijaribu kumwelekeza namna ya kuimudu gari yake vizuri awapo barabarani. Kwa nyuma alikuwepo mkewe, Bi Sofia, alitulia akitafakari ukuu wa Mungu wa jinsi alianza kujibu dua hata akawapatia riziki.

         Wakiwa           wametoka            nyumbani         kwao             pale

Kiembesamaki, waliingia mjini kati; wakaelekea njia iendayo bandarini kisha kuchepukia barabara ielekeayo Darajani. Ilikuwa ni safari ya kujipumbaza tu huku wakipima wakati wa kurudi na kwenda kumchukua

Nusura aliyekuwa skuli majira ya alasiri.

Hamadi! Wakiwa hawana hili wala lile, mbele kulitokea lori kubwa kwa ghafla mno. Haroub aliliona na Ibrahim vilevile, lakini muda ulikuwa wa kufumba na kufumbua macho. Lori lililokuwa katikati ya barabara, limekoleza moto na kuzikataa breki lilikuwa katika kasi isiyomithilika. Alipoliona tu, Haroub kwa mshtuko alipiga honi za babaiko huku akijaribu kuimudu gari iliyokuwa katika mwendo wa wastani, lakini lori ndiyo kwanza lilizidi kunguruma na kukimbia kwa kasi kuwafuata waliko.

“Kwepa! Kwepa! Pishilia mbali kisirani apite,” alisema Ibrahim kumshauri baba yake. Macho ya Ibrahim yalikuwa sawa na ya baba yake. Vile vile yalikuwa sawa na ya Bi Sofia aliyekuwa mdomo wazi, sawa na macho yake hata asiweze kusema neno.

Haroub alinyonga usukani huku na kule huku gari linayumbayumba kama kiota kwenye tawi la mti upigwao upepo; akapiga kona ya ghafla kutaka kulikwepa lori lile lakini alikuwa kachelewa mno. Ikawapasa wote, badala ya kuyakodoa macho kwa mshangao sasa kuyafumba na kumuita Maulana wakijua siku zao za kuishi zilisalia nukta tu. Kila mmoja akasali kimoyomoyo kuomba pumziko jema kwani waendako hakuna akujuaye. Basi, lori lile lililojaa mifuko ya seruji lilikuwa kama mbogo, likawavaa na kuisukuma gari yao takribani mita mia tano kutokea walipokuwa, wakirudishwa nyuma.

Yaliyotokea ndiyo hayo ya kusikitisha, vifo vya ghaflaIbrahim akapoteza maisha pamoja na babaye, Haroub. Bi Sofia alikuwa kimya kwa nyuma, kabanwa na kufinywa na vyuma kuanzia kiunoni kwenda chini huku paji lake la uso likiwa limechanika upande.

Bi Sofia alipotazamwa alikuwa bado hai. Swali: wamtoeje Bi Sofia kutoka mahali aliponasa? Lazima anasuliwe na si kumvuta kwa mikono pekee, angeweza kunyofoka na kuacha viungo ndani kwenye vyuma. 

Ikaitishwa kreni ya bandari haraka na gari moja la msamaria. Kwanza kreni ikawa na kazi ya kulinyanyua lori lililojaa mifuko ya seruli, lililokuwa limepinduka na kuikalia gari ya Haroub kwa juu yake. Baada ya hapo kreni na gari la msamaria viligawana jukumu—moja ikavuta huku na nyengine ikavuta kule. Bi Sofia akanasuliwa na kukimbizwa hospitalini akiwa bado mahututi.

Huo ndio ukawa mwanzo mgumu wa maisha ya Nusura aliyeachwa na kakaye aliyemwachia ziwa, Nuru—wote wakiwa wanasoma katika skuli za kulipia, Nusura akiwa katika skuli ya msingi na Nuru akiwa kidato cha tatu katika shule ya upili.

Kukatika ghafla kwa Haroub na mwanaye wakiwa wote wategemewa ilikuwa ahamani isiyoelezeka. Achilia mbali kuwa hawatakuwepo tena kuyakidhi mahitaji, bado Nuru na Nusura waliachiwa mzigo mkubwa wa ulezi—wamlee mama yao ambaye ajali ile ilimwacha na kilema. Kwani alipotoka hospitali baada ya majuma kadhaa, Bi Sofia alikuwa kiwete asiyeweza kujitegemea mwenyewe, zaidi alihitaji usimamizi wa watu wengine. Kiuno kilikuwa teketeke—akapooza kuanzia kiunoni kwenda chini. Ikiwa hiyo haitoshi, kuanzia kichwani hadi kiunoni, nusu yake hakuwa hai. Hivyo ni kusema Bi Sofia alikufa robo tatu ya mwili wake na kubakiwa na robo iliyo hai.

 

 

 

 

 

 

 

 

II

 

 

HALI ALIYOKUWA nayo Bi Sofia iliwalazimu Nusura na kakaye, Nuru kukaa kitako na kupanga hatua za kuchukua ili maisha yao ya skuli yaendelee. Vilevile maisha ya mama yao kipenzi yabakie kuwa ya tumaini hata kama alikuwa na kilema cha kustaajabia. Wakaitana na kuketi ili kuyajadili yaliyokuwa mazito kwao.

Walichokubaliana ni kwamba, kwanza waelekee bandarini alikokuwa akifanya kazi Haroub. Nia yao ni moja tu, kuomba wasaidiwe namna ya kupata kiinua mgongo au pensheni ya baba yao japo iwavushe wakati huo wakiwa wanajipanga. Ikawa ni ahadi kwao kwenda huko kesho yake asubuhi na mapema.

Palipopambazuka, siku ya kwenda bandarini ilifika. Nusura na Nuru waliifuata njia kutoka Kiembesamaki hadi zilipo ofisi za mawakala wa meli kwa miguu. Kwakuwa baba yao alikuwa akifanya kazi hapo, moja kwa moja wakaielekea ofisi moja ili wapate kuuliza. Wakamkuta mtu mmoja akiwa ndani ya ofisi akiendelea na shughuli zake. Nuru kwa uungwana alisabahi kisha aliuliza, “Tunauliza ilipo ofisi ambayo marehemu

Haroub alikuwa akifanyia kazi.”

“Haroub huyu aliyekufa kwa ajali?”

“Ndiye!”

“Eeh! Mlikuwa mnamdai?” “Hapana!” alijibu Nuru.

Mtu yule aliwatazama bila kuwapa jibu lolote. Akanyanyuka alipokuwa kisha akaelekea mlangoni ambapo alisimama na kuangaza macho pale nje ya ofisi.

Akaita, “Nasri! Njoo mara moja.”

Aliyeitwa Nasri alikuwa kijana mdogo ki umri— yapata rika moja na Nuru. Kwanza ndio umri wa balehe iliyopevuka ilikuwa imemsonga. Kijana yule akaingia ofisini na kusimama mbele ya mwanaume aliyewakaribisha.

“Ati wale madalali wenzake na Haroub walikuwa na ofisi hapa bandarini?” aliuliza mwanamme yule ambaye mbele ya meza yake palikuwa na utambulisho wa jina lake, Hamdan Shemhuna.

“Hapana! Nakumbuka Haroub alikuwa akiishi kwa kudandia ofisi tu. Tangu Shirika la meli la Oman lifunge ofisi zake hapa, madalali walikosa ofisi. Hata walipolipwa juzijuzi hapa, hakuna kati yao aliweza kukodi ofisi,” alijibu Nasri.

Shemhuna akawatazama Nuru na dada yake, Nusura. “Hivyo mnataka nini labda? Na ninyi ni akina nani kwa marehemu Haroub?” aliwauliza.

“Sisi ni wanawe!” alijibu Nuru.

“Poleni sana kwa kufiwa na baba, pia kaka” alisema Nasri.

Hata walipofatilia walielezwa zaidi na baadhi ya madalali wa bandarini pale kuwa, baada ya Shirika la meli la Oman kusitisha shughuli zake katika bandari ya Unguja, kila dalali alilipwa pesa yake. Ndipo wakakumbuka kuwa, muda uliotajwa kuwa madalali walilipwa stahiki zao ndio uleule ambao baba yao alinunua gari lililomtaifisha uhai pamoja na kaka yao kisha kumtia kilema mama yao.

Tumaini walilokuwa nalo likazama na kupotelea gizani. Lakini bado maisha hayakusimama kuitii dhiki yao. La hasha! Yaliendelea kwa kuchomoza kwa jua na kuzama huku midomo na tumbo vingali vikihitaji kula chochote na kunywa. Kadiri siku zilivyokwenda ndivyo ugumu wa maisha uliendelea. Ikafika hata wakati wakakosa hata mlo na kubaki matumbo matupu. Waliisaka hisani kutoka kwa watu hadi nao wakawachoka. Cha kuomba hakikidhi hitaji bali huliahirisha tatizo kwa muda tu. Hivyo ndivyo ilikuwa kwa Nuru na Nusura.

Hali ilipokuwa tete iliathiri hata masomo yao. Nusura ilimpasa kuwa nyumbani akimuuguza na kumhudumia mama yake ambaye hakuweza kusimama wala kujihudumia—kila kitu alihitaji msaada. Kwa maana hiyo Nuru alilazimika kuwa msaka riziki ya familia— akaivaa nafasi ya marehemu baba yake baada ya kuiahirisha shule. 

Hata kama Nusura na Nuru wangetaka kwenda shuleni, nani angelipa karo ya shule katika shule za mlengo wa kibepari—shule za watu binafsi alizokuwa akizimudu baba yao wakati wa uhai wake? Hakuwepo.

Ushikwapo shikamana na uchwewapo na jua lala. Hivyo ndivyo ilikuwa kwa Nuru na dada yake. Ilikuwa lazima yao kufanya kilichostahili kufanyika—kikubwa walilichumia tumbo.

Nuru hakuchagua pa kuokota riziki. Aliugawa muda wake; asubuhi alikuwa akisaidia watu kubeba mizigo ya wasafiri bandarini ambapo aliokota kiasi cha fedha alichoweza kukarimiwa na Maulana. Jua lilipopanda Nuru alielekea nyumbani kupeleka riziki aliyoiokota ili paandaliwe chakula cha mchana. Baada ya chakula cha mchana Nuru alikuwa kiguu na njia kuelekea ufukweni, akiombaomba msaada kwa wageni ambao alitumia lugha yake ya kiingereza aliyoiokota kuwasiliana nao na kuelewana.

Ikawa hivyo siku hadi siku hata ndoto zao zikaenda mbali kwa kila mmoja. Nusura akafumwa na huduma za mamaye pekee na Nuru akawa mtumwa wa hiari wa familia yake. Mawazo ya shule ikawa basi tena.

Ulipopita mwaka mmoja, Nuru alikuwa kayazoea maisha ya kubangaiza. Alijua aingie wapi na atokee wapi. Hata siku zilipokuwa hazisomeki alijua wapi atakopa ama atakwapua ili tu maisha yasogee. Ikawa hivyo nendarudi. Lakini si kweli kuwa Nuru alifanya hivyo akaridhika kuwa hilo ndilo fungu lake. Nia ya maisha mazuri ilimzidi bado. Sasa afanyeje wakati bado hali si shwari kiuchumi?

Siku moja dada yake alipata wazo, akamwalika kaka yake wakaketi. Akamwambia, “Ni vema kaka ukaoa. Mke utakayeoana naye angalau anisaidie kumlea mama huku najaribu kurudi shuleni. Nahisi kuipoteza njia yangu.”

Nuru alitafakari sana na mwisho akauona uamuzi wa dada yake kuwa huenda ukawa wa manufaa. Hata hivyo alisita kuoa kwani angemuoa nani angali akiwa lofa asiye na kitu? Lakini penye nia pana njia.

Nuru aliyekuwa akipendwa sana na wasichana wa kila rika na kila hali kwa ucheshi wake alikuwa na wakati mgumu wa kuamua. Japo nia yake ilikuwa kuoa, sasa alitaka kuoa mwanamke mwenye umri mkubwa kushinda yeye na angalau awe mwenye unafuu wa maisha ili awafae nyumbani kwao. Kati ya wasichana aliokuwa akiwamendea, Nuru akampa nafasi Ramla, mtoto wa baharia mwenye asili ya kiarabu. Alijua Ramla anaweza kuwa mke wa manufaa kwake kwani ki umri alikuwa kamzidi yapata miaka saba. Isitoshe baba yake Ramla alikuwa na mali na hakuwa akiishi Unguja bali aliishi Ugiriki kwa ajili ya shughuli zake za meli. Kwa maana hiyo Nuru akaona ni rahisi kula na Ramla japo alikuwa na ndugu zake wengine.

 Hatimaye Nuru alipomuoa Ramla mambo yakawa kama zamani. Ndoa yenyewe ilikuwa mradi tu ndoa. Nuru hakulipa mahari hata chapa moja kwani nduguze Ramla walimkatalia Ramla alipotaka kuolewa kwa kutoa mahari yeye mwenyewe. Hiyo ikawa sawa na kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi. Ramla na Nuru walikwenda kwa imam wakafunga ndoa yao bila lele wala kelele. 

Wakati penzi lao likiwa changa, Ramla aliihudumia familia ya Nuru karibu kwa kila kitu. Lakini hisani aliyoitegemea Nuru ilikuja kukatika ghafla mno wakati babaye Ramla alipokuja kurudi Unguja. Alipopata habari kuwa Ramla aliolewa tena kwa gharama zake mwenyewe ilimpasa kuwatuma ndugu zake wamfuate. Hiyo siku wakaongozana yeye Ramla na Nuru kwenda kuonana na babaye Ramla, baharia aishiye Ugiriki.

Babaye Ramla aliwapokea kwa maneno makali. Alimlaumu Ramla kwa kuchukua uamuzi wa kuolewa kwa mtu masikini. Mbali tu ya kumlaumu kwa lugha ya kistaarabu, yeye alisema, “Unawezaje kuolewa na lofa kama huyu? Kati ya lofa wote waishio Unguja na Pemba, huyu ndiye lofa kushinda wote Zanzibar. Mtu asiye mbele wala nyuma—aishiye kwa kuombaomba bila kazi maalumu unadhani utachuma naye nini kama si kuchuma janga kisha ukaja kula nasi. Yaani hujajua tu kuwa hapa Zanzibar wapo malofa wengi kama huyu ambao wanamendea kulelewa na watu wenye uwezo wao kifedha. Hawana mapenzi bali wanataka riziki— wanadhiki.”

Maneno yale yalimuumiza mno Nuru japo alichokuwa akielezwa kilikuwa na ukweli. Nuru alikuwa lofa kweli, tena karubandika asiye na kitanda wala shuka, ila alimiliki mwili wake tu ambao nao ulikuwa ukiandamwa na dhiki kila wakati. 

Pamoja na maneno ya kukatisha tamaa aliyoyatoa baba yake, Ramla alikuwa akimpenda Nuru kwa dhati na ndiyo maana alikwangua sehemu kubwa ya mali na kumhisani Nuru na familia yake. Japo babaye alimtolea maneno ya kuchukiza, hayakumbadili msimamo wake katika kupenda. Bado alihesabu kuwa Nuru ni wake hata siku ifike wazeeke, wafe na kuzikana.

Waliondoka kwa baba yake Ramla kila mmoja na njia yake, Nuru akiwa mkataliwa na Ramla akiwa mkatazwa. Vurugu alizozisababisha baba yake Ramla dhidi ya familia ya Nuru zilitosha kumfanya Nuru aachane na Ramla hata kama alikuwa akimpenda kama kiungo chake muhimu. Hakutaka kuyasikia tena maneno ya kuumiza kwani kuwa lofa halikuwa kusudi la Nuru, bali ni maisha tu na wakati ulimpasa kuwa hivyo.

Nuru akaamua kuirudia kazi yake ya zamani. Hakukubali kumtariki Ramla japo hakuwa karibu tena naye. Nuru alikuwa mtu wa kushinda kisiwani Nungwi akidanga riziki kwa watalii. Hata siku moja alipopata hamu ya kumuona mmewe, Ramla alifunga safari hadi Nungwi ambako alimkuta Nuru akiwaburudisha watalii wa kizungu kwa huba.

Sokomoko lililozuka halikusamaheka kwa Ramla ambaye alikuwa kaapa kuyamaliza maisha yake pamoja na Nuru hata kama walikuwa na dhiki kiasi ghani. Nuru hakuonesha wasiwasi kwa alichofumwa akiwa anakifanya na wanawake waliomzidi umri kwa miaka zaidi ya ishirini—wenye umri zaidi ya mamaye. Hata alipohojiwa sababu ya kufanya hivyo alisema, “Nafanya hivi si kwa kupenda, ni lazima ili mkono uende kinywani. Hawa wametoka Ulaya na pesa zao na wamekuja hapa kufurahi.”

“Hivyo wamekufuata wewe ili uwafurahishe?” aliuliza Ramla.

“Pesa zao ndizo zimenivuta wala si uzuri wao. Hapa nafanya haya kwa pesa, hata nikitoka hapa dhiki itakoma japo kwa juma moja au mawili ndipo nitatulia.”

“Huu si ustaarabu wetu! Ni aibu ambayo mwenye imani hawezi kustahimili—umeniudhi mno Nuru na sasa nimeyaamini maneno ya baba. Wewe ni lofa! Tena lofa kuliko wote Zanzibar, huenda hata duniani kote.”

Ramla hakuwa na breki, moja kwa moja alirudia nyumbani. Nyumbani nako alipaona hapafai kwani alihitilafiana na nduguze. Akahisi aliyoyaona kwa mmewe yalionwa na kila mtu katika Unguja yote, sasa yatamfedhehesha. Ramla akaamua kutoroka nyumbani kwao na kukimbilia Oman ili akae mbali na Nuru pia familia yake isimsumbue tena.

Mwaka mmoja baadaye, wakati Nuru akiendelea na shughuli za kutembeza watalii na kuwahudumia kwa siri alimpasha habari dada yake. Siku hiyo Nusura alipata huzuni ya ghafla. Kakaye, Nuru alimdokeza kuwa alipanga safari ya kwenda Uropa kusaka maisha ya nafuu. Akamhakikishia kuwa akirudi maisha yao yatakuwa ya maana kushinda yale alikuwa akiyaonja kutoka kwa Ramla. Nusura alipatwa wasiwasi hasa ni wapi Nuru angepata nauli ya kumfikisha Ulaya. Hilo alilijibu Nuru mwenyewe siku ambayo alikwenda nyumbani na mwanamke wa kizungu na kumtambulisha.

Nuru alimwambia Nusura, “Huyu anaitwa Laura, rafiki yangu kutoka Sweden, ambaye huwa ananisaidia mara kwa mara awapo hapa Zanzibar. Sasa anataka twende naye hadi Ulaya ili akanisaidie kupata kazi ili maisha yetu yawe angalau kama ya watu wengine walio nafuu,” alisema Nuru.

Nasra alikuwa mzito kukubaliana na kaka yake. Damu ni nzito kuliko maji—Nuru aende ulaya kweli? Si kwamba atatusahau akienda huko? Nusura alijiuliza baada ya kuzikumbuka habari za wana waliopotea kwa kuzamia Ulaya na Amerika kisha wakawa raia wa huko. Hilo ndilo lilimpa shaka Nusura katika waza yake. Akamkataza kaka yake akisema, “Kama maisha mazuri yanapatikana pia hapa, yatafute hapa unapoheshimika kuliko kwenda mbali na nyumbani. Mbona kuna watu wengi hapa Zanzibar wanamaisha mazuri kuliko hata huko Ulaya?”

“Una hakika hao matajiri walijichumia pepo wakiwa hapa? Je kama walisafiri ndipo wakaleta riziki hapa kisha kupumzika?” aliuliza Nuru.

“Hapana! Hebu hesabu miji ambayo vijana wake walitoroka na watalii na kwenda huko Ulaya na hao wanawake wa kizungu, ni wangapi walisharudi na mafanikio?”

“Kila mtu anayo bahati yake,” alisema Nuru kisha akaondoka na kumwacha dada yake akiwa njiapanda.

Pamoja na kupingwa vikali na dada yake, Nuru aliondoka baada ya siku tatu—akaenda Ulaya na Laura. Alichokiacha ni kipande cha barua kuwajuza kuhusu safari yake na kuwaachia kiasi cha pesa cha kusukuma siku, akiahidi kuwa atakuwa anatuma pesa mara kwa mara. Hiyo ndiyo ikawa safari ya Nuru na kumwacha Nusura akihangaika kumlea mama yake.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

III

 

 

MZIGO ALIOACHIWA Nusura ulikuwa mzito. Ilimpasa kujilea yeye mwenyewe kisha amlee mama yake katika umri wake ule mdogo. Alichokuwa akikihofu ni kuchuuzwa kisha kufanyiwa hila na aliowaomba hisani, hivyo akaomba dua kuwa awe na njia nyoofu. Hakutaka kukaa gizani wala machochoroni kwa hisani ya chochote, ila alitafuta riziki kwa kufanya vibarua hali ilipozidi kuwa tete. Kakaye hakuwa katuma chochote na karibu mwaka ulikuwa unaeleka kukatika. 

Nusura alishakuwa rafiki kwa wavuvi wa samaki, akiwasaidia kuuza mtaani na wakati kuwapaa magamba ili wateja waondoke na kitoweo kilicho tayari. Alichokuwa akilipwa Nusura kwa kazi hiyo ni fungu la samaki ambao aliwatwaa nyumbani akala na mama yake. Bado alikuwa na tumaini kuwa siku moja kaka yake atarudi na kumpunguzia adha alizokuwa akizipitia. Maisha ni magumu lakini yeye Nusura aliyaonesha ukomavu wa akili na kuyakabili. 

Hata lini shida ikazoeleka na dhiki ikawa rafiki wa mwanadamu? Ukweli ulio kweli haipo siku kama hiyo kwa mwanadamu. Dhiki ilimfanya Nusura kutia juhudi kutaka kuishi vizuri lakini kila alipotaka kufanya jambo, wakati ulikuwa ukuta kwake—hakupaswa kwenda mbali na mamaye aliyehitaji huduma kila wakati.

Siku moja kama kawaida yake Nusura alitoka, akaenda baharini. Akiwa huko akingoja wavuvi kurudi ufukweni alipatwa wazo. Nusura alisimama na kuinamisha kichwa chake na kuwa kama suke la mpunga lingojalo kuvunwa baada ya kukomaa. Upepo uliovuma ulipompitia, gauni lake lilipepea kama bendera. Lilivutika upande na kujaa hewa kama purutangi, karibu upepo umnyanyue kwa jinsi alikuwa kanyauka na kuwa mwembamba kama unyasi wa jangwani. Dhiki! Yote hayo yaliletwa na dhiki—ukosefu wa riziki.

Alikuja kuzinduliwa na mawimbi ya bahari ambayo yaliivamia fukwe na kumsepetua yalipokuwa yakitapika takataka na kutambaa kurudi yalikotoka. Nusura alijizatiti miguuni, akiilazimisha miguu iliyokuwa imenyauka kama mfagio wa chelewa kusimama jadidi baada ya kuitanua. Alipohakikisha kuwa mawimbi yamepita ndipo alinyanyua kichwa kutazama kule ambako maji yalitokea. 

Macho ya Nusura yalipepea, yalitopea mbali, hadi katikati ya bahari iliyokuwa imechafuka. Huko katika upeo wake aliyaona mawimbi makubwa yakinyanyuka na kupigana kisha kushikana na kuachana. Katikati ya dhoruba lile kali, aliiona meli ikiwa katika mwendo wa konokono. Nusura hakuwa ametabasamu kwa kipindi kirefu, lakini meli ile ilimtekenya alipoiona ikielea kama chelezo na kwenda taratibu kama tembo wafanyavyo nchi kavu. Mdomo wake uliokuwa umechacha kwa ukimya uliyaacha meno yake meupe wazi. Alifurahi.

Nusura alipiga hatua na kupanda kwenye tumbawe, pembeni kidogo baada ya kutoka kwenye mchanga ambapo palifikiwa na maji ya bahari. Alisimama juu na kuyakodoa macho yake makubwa, mazuri yaliyo kama kitunguu kichanga kwa duara. Kwa sababu ya dhiki, yameshaingia ndani ya fuvu la kichwa na kuwa kama mashimo ya bao, akawa kama mlevi aliyehujumiwa na gongo kwa jinsi aligofuka. Aliyapanua macho kuitazama meli ile ambayo sasa iliyakata maji taratibu kama kobe asafiriye kwenye rundo la mchanga. Nusura alijikuta anairudisha mikono nyuma na kukishika kisogo. Wakati huo meli aliyoiona ilikuwa inaelekea bandarini kutia nanga. Kwakuwa alijua kusoma, akayasoma maneno yaliyo ubavuni mwa meli yakisema: OMAN, LANGO LA

RAHA. 

Ghafla Nusura alifikwa na maneno. Akajisemea, Hilo ndilo lango la kwenda Arabuni, kwenye maisha ya stara na starehe. Nami siku itafika nitaenda huko. Siwezi kuwa kama kaka yangu aliyekwenda kimoja—mimi nitarudi.

Moyo wa Nusura ulifumwa hamu ya kufika Oman, alikokuwa akisikia mara kwa mara kuwa wasichana wengi walikwenda kusaka maisha na kubahatika kuokota maisha ya hadhi na heshima. Walijipatia pesa na mali nyingi kutoka Arabuni na kuzinyanyua familia zao zilizokuwa zimenasa katika tope la umasikini. Hilo alikuwa na uhakika nalo kwakuwa alishawaona wasichana wakirudi na kitu cha kuonyesha kwa watu na si alikotimkia kakaye—huko hajawahi kabisa kuona mtu akitajirika. 

Basi, Nusura akiwa mhanga wa maisha ya dhiki pale Unguja, alihisi heri ilikuwa njiani, ila tu alingoja siku ifike aende Oman. Japo aliwaza hayo, Nusura aliketi juu ya jabali akiwa anatafakari zaidi. Kila alipotafakari namna ya kufika Arabuni, aliliona giza likitanda mbele yake. Hakuwa akijua wapi angelianzia na wapi angelimalizia—asafiri hadi huko, na hata kama angekuwa na pa kuanzia, angewezaje kwenda? 

Kwanza, Nusura hakuwa hata na gwala lile la kumpatia kinyozi japo azikwangue nywele zake zilizochakaa kichwani na kuwa kama mafungu ya uyoga kwa jinsi mabutu aliyosuka yalisimama. Jambo la pili; je mama yake angemwacha na nani akitaka kuondoka? Basi aliishia kukitingisha kichwa baada ya kuyawaza magumu yaliyo ndani ya familia yake.

Nusura aliamua kurudi nyumbani baada ya kukaa ufukweni kwa muda mrefu bila kumuona mvuvi aliyekuwa akimtarajia. Huenda kuchafuka kwa bahari ndiko kuliwaogopesha wavuvi kuifuata mitego yao na kuanua samaki hivyo Nusura akarudi mikono mitupu.

Nyumbani kwao alipokelewa na nzi waliokuwa wakirukiarukia vyombo vilivyojaa shombo la samaki waliokula jana yake. Kabla ya kuingia ndani aliinama na kuvikusanya vyombo vyote na kuvifunika kwa kipande cha chandarua chakavu ili angalau nzi wasiendelee kuving’ong’a na kuvitapikia uchafu. Aliingia ndani.

Alipofika ndani alipokelewa na harufu kali ya mkojo na kinyesi. Mamaye ambaye alikuwa hajiwezi alikuwa kalipiga kumbo beseni alilowekewa kwa ajili ya haja kubwa na ndogo. Haja ilipomwagika ilitapakaa chumbani ndipo harufu kali ilikiteka chumba. Nusura alishika pua na haraka alielekea chumbani aliko mama yake.

“Nini kimetokea mwanangu?” aliuliza Nusura kadiri alivyozoea kumwita mamaye wangali rafiki wa chanda na pete. Nusura hakukarahishwa na hali aliyokuwa nayo mamaye hata akakata tamaa. Alikuwa akimhudumia vyovyote ilivyowezekana alimradi tu siku zisogee huenda tumaini la maisha bora likaja na upepo.

“Bahati mbaya mama yangu, niliteleza nikalipiga kumbo beseni, ndipo ikawa hivyo,” alijibu mama yake Nusura akiwa na mnyweo wa sauti kwa hali yake ilivyo taabani. Ni muda sasa yupo kitandani akigeuka na kugalauka, lakini si kunyanyuka na kwenda kutafuta riziki. 

Mama huyu akajikaza na kusema na mwanaye. Akamwambia, “Nimeita sana Nusura, nilipokosa sauti ya kunipokea basi nikabaki mkimya, ulikwenda wapi kipenzi changu?” aliuliza Bi Sofia, mamaye Nusura.

“Nilikwenda fuoni kutafuta samaki,” alijibu Nusura akiwa anasafisha sakafuni kwa fagio la chelewa. “Lakini mguu wangu huko si wa heri, sikubahatika kupata hata hao dagaa mchele. Naona bahari imechafuka hata wavuvi sijabahatika kuwaona,” aliongeza Nusura.

“Bahari leo imechafuka?” aliuliza mamaye utadhani hakusikia alichosema Nusura.

“Tena kuchafuka kwenyewe si kwa polepole. Nimesubiri sana lakini sijamwona mvuvi yeyote, hata Razaki ambaye hurudi fuoni kwa wakati hakuonekana. Sijui leo siku itakwendaje,” alisema Nusura kwa sikitiko huku akitoka na beseni la taka kwenda mahali kutupa.

Aliporudi ndani aliokota vyombo ili kwenda kuviosha, Nusura alikumbuka kuwa hakuna sabuni ndani. Kwanza aliguna, akasema na nafsi yake ndipo mguno wake ulichupa hadi masikioni mwa mama yake aliyekuwa chumbani akimsikiliza.

“Kulikoni unaguguma peke yako?” aliuliza mamaye Nusura.

“Hata sabuni hakuna mama.”

“Sabuni imeisha!” alistaajabu mama Nusura. “Hebu tazama hapo dirishani, kama niliiona jana,” aliongeza mama Nusura.

“Haipo. Kunguru watakuwa wameiokota baada ya kuwa nimeisahau. Nakumbuka nilipotoa vyombo nje, kabla sijapatwa wazo la kwenda fuoni niliitoa na kuiweka juu ya uchanja.”

“Basi Kunguru wameshaichopoa, hakuna namna tena,” alisema mama Nusura kisha kukohoa kidogo. Hata alipokohoa bado sauti ya kikohozi chake si ya mtu aliye hai—ni sauti dhaifu inayotokea tumboni, tena tumbo lenyewe ni la mtu mwenye njaa ya siku mbili au tatu. Hajiwezi.

Nusura afanye nini sasa wakati anaishi kinyume na jina lake—hana wa kumnusuru! Alichofanya ni kutoka ndani akachepukia nje. Kuna mahali alilenga kwenda, dukani. 

Nusura alipiga hatua za haraka kuelekea dukani. Alimkuta muuza duka akiwa ndani ya duka lake. Alipomtazama muuza duka, Nusura ndipo aliwaza namna ya kuanza kueleza shida yake. Nafsi haikuwa huru kuomba hisani ya kukopeshwa kila siku. Muuza duka alipomwona aliacha kazi ya kubandika bei ya bidhaa na kumtazama kwanza Nusura. 

“Karibu kiziwanda wa Bi Sofia,” alisema Makame, muuza duka maarufu pale Kiembesamaki, katika mtaa wa Halingumu, hapo Unguja. Makame alimtazama mara mbilimbili Nusura. Moyo wake ukaenda pande mbili kwa wakati mmoja. Upande mmoja ukapuuza na upande mwingine ukabakia kuchachatika kwa tamaa ya kumhujumu Nusura kutokana na shida zake.

Wakati yakitokea hayo tayari Nusura alitoa itikio kinyonge akisema, “Asante Makame.”  

Japo aliitika, bado jicho la Makame lililoganda kifuani kwa Nusura, penye vichuchu vilivyochomoza lilimfanya Nusura kuinamisha kichwa kwa aibu. Akatamani hata ageuke na kumpa mgongo Makame ili asimtazame kwa jicho laini namna ile. Angefanyaje sasa nje ya asili ya umbile lake? Nusura angali akifikicha vidole vya mikono yake aliibwaga shida yake huku anang’ata kucha kama panya. Akasema, “Nina shida Makame.”  

Makame sikio likasimama wima kwa kauli ya Nusura. Kulia shida kwa mwenye nacho ni kualika mengi. Kwanza kudharauliwa, kushushwa hadhi na kwa banati kama Nusura ni kuchuuzwa—kunyonywa kwa hila kwa usemi wa nipe n’kupe!

Makame akasema baada ya ukimya uliojaa tabasamu la mamba, “Shida haliliwi muuza duka, shida hutatuliwa na serikali Nusura. Ukiwa kwangu sema unahitaji bidhaa nikuhudumie, nikufae au tufaane,” alisema Makame akiwa kashika kopo la kuchotea pimo la bidhaa yoyote kati ya alizokuwanazo.

“Basi nahitaji nihudumie kipande cha sabuni, japo nikaogeshe vyombo,” alisema Nusura. 

Makame alitega mkono kupokea pesa lakini Nusura alibaki kimya akimtazama. Alilazimisha tabasamu. “Sina pesa, nikopeshe nitaleta pesa jioni,” aliongeza Nusura.

Makame alitafakari. Alimtazama Nusura kisha alitingisha kichwa. “Nilikueleza matatu—kukuhudumia ili utoe pesa, nikufae kwa maana mimi nitoe hisani bure na unisikilize nitakacho, na tatu tufaane. Wewe ushakua nadhani unajua nikikupa nawe…..” Nusura alitaka kuondoka lakini Makame alimuita, “Nusura usiondoke, acha nikupe. Lakini kumbuka kuwa, biashara yangu bado changa, usiponilipa kwa wakati jua nitafunga duka. Hakikisha kabla jua halijapunga mkono wake magharibi, uwe umeniletea,” alisema Makame huku akiandika kwenye daftari la kumbukumbu. “Imekuwa alfu tayari, ulete pesa yote ifikapo muda huo, lasivyo sitakuonea haya tena, ” aliongeza Makame.

“Kaka yangu atakuwa njiani yu aja, yote haya Makame yatakwisha,” alijibu Nusura angali akipokea kipande cha sabuni kutoka kwa Makame.

“Kaka yako mpumbavu yule—tangu lini mtu akakimbia kwao, ati kaka akaenda kuolewa Ulaya ili apatiwe pesa ya bure? Huyo lofa hata usimtarajie. Mambo yakiwa magumu wewe kubali yaishe—tukuoe kisha tumlee Bi Sofia aishi. Huyo lofa wa Zanzibar akija pia apate pa kufikia.

Nusura alichukizwa na maneno ya Makame, akapiga hatua haraka kwenda nyumbani. Alipokaribia kufika aliona kuna watu wawili, wote wanawake wakiwa wamesimama pembeni ya nyumba yao. Walikuwa wamemuona ndipo wakaamua kusubiri kabla hata ya kubisha hodi. Nusura alipokaribia aliwakaribisha baada ya kuwafahamu. “Karibuni, nilienda dukani mara moja,” alisema Nusura.

“Tumekaribia. Salama lakini?” alisema mwanamke mmoja, kati ya wale wawili.

“Alhamdulilah tu salama, lakini hali ya bi mkubwa bado,” alijibu Nusura.

“Bi Sofia bado hali haijatengemaa?” aliuliza mwanamke wa pili.

“Tena ni afadhali ya jana wifi yangu. Kila jua jipya lifikapo kwanza nd’o hali yake inatibuka. Hadi nakata tamaa,” alieleza Nusura. Aliekea kwenye vyombo akaificha sabuni kwenye bakuli na kurudi kuwapatia wageni vigoda wakaketi. “Yaani hata sijui itakuwaje, lakini nakuona wifi yangu umekuwa tipwatipwa! Maisha huko ulikokuwa si haba!”  

“Alhamdulilah kuna neema. Je, kaka yako tangia aondoke bado hajarudi?” aliuliza Ramla. 

Zainabu waliyeambatana naye, ambaye umri wake ulielekea kuwa wa makamo, sura yake kidogo ilianza kusinyaa na mwili uliukataa ujana.

“Nuru hajawahi kurudi, hata ile salamu tu hatujawahi kuisikia tangu aende Bara Uropa,” alieleza Nusura akiwa kashika tama. “Tangia aende na yule mwanamke wa kizungu basi tena, katupa mti na jongoo wake. Hata sijui….” Nusura machozi yalianza kumbubujika.

“Wala usilie Nusura. Huwezi kujua anayokabiliana nayo huko Uropa. Ipo siku Mungu atamleta, lakini unapaswa uelewe kuwa, kwa sasa wewe unatakiwa kupigania hatima ya maisha yako na maisha ya mama. Ukikalia kuomboleza hapa, nakwambia utavuna msiba na machozi hayatakauka. Mwanamke kutafuta, ona mimi tangia kaka yako aniache na kuzuzuka na mzungu, nilipokwenda Arabuni na sasa kurudi, hali yangu ni ile ya zamani?” aliuliza Ramla.  

Nusura alimtazama tena kisha alitabasamu. “Hali yako ni nzuri kuliko awali, umependeza sana, mashaallah!  Tena unatamanisha,” alieleza Nusura.

“Basi nikukate kauli wifi yangu,” alisema Ramla. Alimsogelea Nusura na kumnong’oneza.  

Nusura aliponong’onezwa alijikuta anatabasamu. Akauliza, “Mimi?”

“Ndiyo, tena ikiwezekana ndani ya siku hizi chache. Baada ya likizo yangu tu, tunaondoka wote,” alieleza Ramla.

“Lakini wifi, mama yangu atabaki na nani sasa? Hata hivyo, kwenda Arabuni ni gharama kubwa sana, hiyo nauli nitaipata wapi miye pamoja na hati ya kusafiria sijui—vitu vingi sina,” Nusura alionesha wasiwasi.

Ramla alimtazama Nusura kisha alitabasamu. “Yote hayo utalipiwa na huyu umwonaye hapa. Ukifika huko utalipwa mshahara mzuri na utakuwa na uwezo wa kulipa gharama zote kwa mishahara miwili tu, na utakuwa huru kukusanya pesa kwa ajili ya maisha yako,” alisema Ramla.

“Kweli Ramla?”  

“Tena kweli isiyo na mawaa.”

“Je, mama yangu sasa, nitamwacha na nani? Tena kwa hali aliyonayo—mh!”

“Kama utaafiki, tutaajiri mtu mwengine wa kumsaidia kwa muda mfupi tu, ambaye tutamlipa. Isitoshe weye hutakaa muda mrefu huko, miezi sita ikishapita utarudi ukiwa vizuri nakwambia. Hata kama kumtibia mama itakuwa jambo rahisi na si kuwa lofa—ombaomba kama kaka yako,” alieleza Ramla.

Maneno ya Ramla yalimwingia Nusura. Aliinama akatafakari na kuwatazama wageni wale. “Ramla, inalazimu umjuze mama kuhusu hili, kwangu hakuna pingamizi. Nataka maisha ya nafuu si ya dhiki kama haya,” alisema Nusura.

Zainabu na Ramla walikaribishwa ndani ili kumjulia hali Bi Sofia. Hali yake ilikuwa ya mwele asiyejiweza, lakini mdomoni alikuwa buheri.

“Mama, najua utapona kwa uwezo wa Allah,” alisema Zainabu.

“Amina, mwanangu!” aliitikia Bi Sofia huku akiwa anaficha noti mbili za elfu kumi alizokirimiwa na Zainabu. Alizisokomeza kwenye titi lake. “Allah akuzidishieni wanangu. Ilipotoka irudi mara alfu na awapatie nyengine nyingi kwa kila hitaji la moyo na mwili,” Bi Sofia alitia maneno na dua. Aliikusanya mikono akachezesha midomo kwa kunong’ona ikiwa ni dua ya kimya kimya.

“Mama, kama nilivyokueleza. Najua ni vigumu kuamua kwa sasa, lakini hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kukusaidia,” alisema Zainabu baada ya kumueleza Bi Sofia nia yake ya kutaka kumchukua Nusura na kwenda naye Oman.

“Nimeelewa mwanangu, lakini wasiwasi wangu ni mmoja tu; huyu Nusura kwa sasa ndiye miguu yangu, yeye hufika popote nitakapo kufika. Nikiwa na shida hii ama ile nikimwagiza hufika popote, sasa akiondoka sijui nani atanifaa kiasi hichi?” aliuliza Bi Sofia. “Angelikuwepo mume wangu, pengine hata haya yote yasingelikuwepo,” alisema Bi Sofia akiwa kaitazama picha ya mumewe iliyokuwa ukutani. Machozi yalimbubujika akiwa kajawa huzuni. “Mume wangu, Allah mrehemu, apumzike salama aliko!” alisema Bi Sofia akiwa chekwe kwa machozi machoni.

Bi Sofia alikumbuka mazito ya kuondokewa na mumewe aliyekuwa dalali wa meli pale bandarini. 

Kumbukumbu za mwanaye na mmewe zilimchukua Bi Sofia na kumzamisha kilioni—akalia na kuyakamua machozi mengi. Ramla na Zainabu walimbembeleza Bi Sofia na kumweleza mengi ya kumtia moyo. Walimhakikishia kuwa watampatia msaidizi kwa muda ambao Nusura atakuwa Oman akifanya kazi, ila baada ya miezi sita, lazima Nusura angerudi kuja kumtibia akiwa na uwezo zaidi kifedha. Bi Sofia alilainika baada ya kusikia hayo.  Akasema, “Basi kama Allah kataka iwe hivyo, na iwe. Nimekubali, ila tu Nusura asin’tupe kama kaka yake alivyofanya.”

“Mama siwezi kukutupa, asilani abadani, sitakutupa mama yangu,” alieleza Nusura akiwa kakenua hadi vigego vyake vikaonekana.

“Basi mtu wa kukusaidia atakuwa tayari leo jioni. Pamoja na kukupatia msaidizi, tutahakikisha kila kitu unachohitaji kwa muda wa miezi hiyo kinapatikana ndani. Tutahemea kila hitaji la chakula na akiba kidogo ya fedha ya dharula tutakuachia,” Zainabu alitilia sukari maneno yake na kumfanya Bi Sofia abubujikwe machozi zaidi. Si machozi ya ombolezo mara hii, bali ni machozi ya furaha akiwa haamini kile kilielekea kutokea.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

IV

 

HATIMAYE NUSURA alikipa kisogo kisiwa cha Unguja, akatokomea Oman. Huko akapokelewa katika mji wa Oman na familia ya Bi Raiya. Safari yake ilimchukua hadi kwenye familia aliyohitajika akiwa kaongozana na Ramla pia Zainabu. Alikabidhiwa kwenye familia moja yenye maisha ya daraja la juu.

Kwakuwa kuku mgeni hakosi kamba miguuni, Nusura alikuwa makini awapo ugenini. Kila alichokuwa akitakiwa kukifanya alikifanya kwa haraka, tena kwa umakini na ukamilifu. Alijipa hebedari ya kufanya kila kitu kwa wakati unaofaa ili apate kuwafurahisha wenyeji wake ambao huenda wangemtunuku hata zawadi kwa uhodari wa kazi yake. Wakati huo Ramla na Zainabu hawakuwa naye tena, nao walikuwa ambako Nusura hakuwa akifahamu na hakujua kile walikifanya.

Muda ulizidi kwenda, mwezi mmoja ulikatika, Nusura akiwa kijakazi katika nyumba ya kigeni. Kwa muda wote huo hakuwa amenusa harufu mbaya ya kumchukiza ndani ya nyumba ile. Kazi yake ilikuwa ya kupika na kupakua, kufua na kuanika kisha kuanua. Alikuwa na kazi ya kusuka na kufumua nywele na wakati kusafisha nyumba na kuiweka katika hali ya kupendeza kila wakati. Hakuna kazi ilimpiga chenga na kumshusha thamani Nusura. Kadiri muda ulivyozidi kwenda ndivyo alizidi kuwa mzoefu. 

Kufika kwa Nusura katika nyumba ile, ambayo ilikuwa na watoto wa kike watatu na wanaume watatu, ilikuwa kama ngekewa kwa familia ile. Mama mwenye mji ule aliyeishi katika utaji na wanawe—vile vile alivyokuwa Nusura, alimwita Nusura na kumkalisha kitako baada ya mwezi mmoja kumalizika. Akamwambia, “Nusura, kazi zako zimenipeperushia mbali dhana yangu kuwa watu wa Zenji wengi ni wavivu na wakaidi. Kwako nakupa kongole kwa ustadi wa kazi zako,” alisema Bi. Raiya, mwarabu aliyejaa utulivu machoni.

“Asante mama,” aliitikia Nusura akiwa makini kusikiliza.

“Kwa mwezi mmoja ulioishi na mimi, ni kipimo tosha cha kuwa unafaa kuandikwa kazini, hivyo rasmi nakujulisha kuwa nimekuandika kazi. Nitakulipa dala mia tatu kila mwezi,” alieleza Bi Raiya.

“Asante mama, Mungu akuongezee,” alisema Nusura akiwa kapiga magoti.

“Hiyo pesa ni nyingi, ni zaidi ya laki sita ya huko utokako,” aliongeza Bi Raiya. “Kwa kuanzia, mwezi huu wa kwanza sitakulipa wewe chochote. Pesa hii namlipa Zainabu aliyekuleta kisha miezi mingine mitatu inayofuata utapata dala mia na hamsini. Baki ya fedha nusu kila mwezi nitamlipa Zainabu kama mdhamini wako aliyekuleta,” alisema Bi Raiya.

Nusura aliinama. Nafsi yake iliungua na kuugua. Aliponyanyua kichwa alikuwa na chozi lililochuruzika na kuangukia sakafuni, kwenye kibaraza walipoketi. Haraka alipeleka kiganja na kifikicha macho kisha kuyafuta machozi. “Nimeelewa mama,” alisema Nusura kwa shingo upande.

“Usilie Nusura, hiyo ndiyo hali halisi ya maisha ya huku. Zainabu hajakuleta bure, alitumia pesa yake hivyo lazima arejeshe pesa. Kama hujui, kuanzia sasa ufahamu kuwa, anayekufanya kuwa hapa Oman ni Zainabu. Unapaswa umheshimu na umsikilize. Yeye ndiye anayo hati yako ya kusafiria. Ndiye aliye na hati yako ya kufanya kazi hapa, hivyo akiamua jambo lolote ufanye ni lazima ufanye. Ukikaidi anaweza kukufanya lolote,” alieleza Bi Raiya. Nusura alikuwa kainama kama mkungu wa ndizi.

Nusura aliyapokea masharti ya kazi yake. Aliendelea kufanya kazi kwa bidii kama alivyokuwa kaahidi. Kazi zilizoeleka kuwa ni kudeki nyumba na kuweka samani za ndani katika hali ya kupendeza wakati wa asubuhi, mchana na jioni. Alikuwa anapaswa kupika chakula, kufua, kupasi nguo na kuwaosha miguu wanafamilia. Kazi ya kila mwisho wa juma ilikuwa ni kumfumua nywele Bi Raiya na kumwosha kisha kumpaka hina kadiri alivyohitaji. Kazi zilimfanya Nusura kukosa muda wa kupumzika kwani alikuwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kulala. Kwa jinsi kazi zilikuwa, kwa nadra alipata saa nne peke yake za kupumzika huku saa ishirini zote za siku akiwa wima akifanya kazi.

Mwezi wa pili ulipomalizika, Nusura alitegemea kuipata nusu ya fedha aliyoahidiwa. Alinuia kumtumia mama yake ili angalau apunguze makali ya maisha na ikiwezekana apate nafasi ya kwenda kutibiwa. Tofauti na tarajio, Nusura hakupata pesa aliyokuwa kaahidiwa, ambayo ni laki tatu kama nusu ya mshahara wake baada ya kumlipa Zainabu. Ukimya ulipokuwa umezidi, Nusura alimuuliza Bi Raiya, “Mama, naweza kupata ile pesa nusu, ambayo ulisema itabaki baada ya kumlipa Zainabu pesa yake?”  

Bi Raiya alimtazama kwa jicho asilolizoea. Akasema, “Nusura, hiyo pesa unaitaka uifanyie nini? Tazama, hapa nyumbani unapata kila kitu, tena huhitaji kuwa na pesa. Sema nilikuwa sijakuambia, pesa zako zote nitazitunza hadi siku unapokwenda likizo kwenu ndipo nitakupatia. Nafanya hivyo kwa wema, kwani ukirudi nyumbani upate kufanya jambo la maana,” alieleza Bi Raiya. Nusura lilimshuka shuu! Aliinama akiwa na maumivu moyoni, kama mtu ambaye alitiwa mkuki wa moto kifuani. Mwili ulipoa akanywea na kupoteza hamu ya kula hata kunywa. Wakati huo Bi Raiya alielekea nje ya nyumba ile.

Bi Raiya aliporudi alikuwa kaambatana na wageni watatu, wote ni wanaume. Kila akiwatazama, Nusura hakuwa amewahi kuwaona kwa kipindi chote alichokuwa kaishi katika nyumba ile. 

“Nusura, hawa ni wageni wangu. Watakuwa hapa kwa kipindi wanachohitaji kuwa. Unapaswa kuwapikia, kuwafulia na kuwafurahisha kwa kila hali waitakayo,” alisema Bi Raiya. “Pia, mzigo huu kauweke chumbani mwako,” aliongeza Bi Raiya akiwa anampatia begi dogo Nusura. 

“Sawa mama, nitawahudumia,” alijibu Nusura kwa uchangamfu. Hakujua ukarimu aliokuwa akielezwa ni wa namna gani. Akilini Nusura alijua ukarimu aliokusudiwa kuufanya ni kupika na kupakua, kufua na kupasi nguo akisahau jambo lililokuwa limejificha sirini mwa nafsi ya wanaume wale pamoja na Bi Raiya.

Usiku ulipoingia, baada ya chakula cha usiku, Nusura alisafisha vyombo kama kawaida yake. Aliiweka nyumba katika hali ya usafi na kuingia chumbani mwake. Hakuwa ameufunga mlango wa kuingilia chumbani akawa ameingia kuoga kwenye choo cha ndani ya chumba. Uchovu ulimchukua na kumfanya aoge haraka akitaka kuwahi kupumzika ili pia apate kuamka mapema. 

Aliipurua kanga yake na kujidodeka sabuni kisha kulifungua bomba lililoyamimina maji kwa wingi. Alijisugua kisha alijifuta kwa kanga yake tayari kabisa kuelekea kilipo kitanda. Alipoufungua mlango na kutupa macho chumbani, aliona kuna mtu akiwa kaketi kitandani. Moyo ukapasuka kama mwamba uliotiwa baruti na kupasuliwa paa! Nusura alipigwa ganzi mwili mzima. Macho yake yalipanuka na kuongezeka ukubwa akiwa kaishika kanga yake ambayo ilikuwa juu ya mwili mtupu. Matiti yake yaliyojaa yalichezacheza kila wakati ambao moyo ulifurukuta kwa hofu. 

Mwanaume aliyekuwa kitandani alimtazama kwa uchu huku Nusura akimtazama kwa hofu, walitazamana. Hatimaye Nusura alipiga hesabu zake, aliutazama mlango wa kutokea chumbani mule akajua ndio ulikuwa uamuzi sahihi kuuchukua. Nusura alinyanyua mguu wa kushoto, ulifuata wa kulia haraka huku mkono mmoja ukiwa umeishika kanga vizuri na mkono mmoja ulikivamia kitasa na kukishika kisha kukinyonga ili atoke. Hamadi! Kitasa kilikuwa kigumu, mlango ulikuwa mgumu, haukuweza kufunguka. Mwanaume yule alisimama na kuizoa kanga ya Nusura ikajaa kiganjani. 

Nusura alijua kilichokuwa kinafuata hivyo alipiga kelele, “Niacheee!”  

Mwanaume yule alimnyakua Nusura kama mwewe afanyavyo kwa kifaranga cha kuku. Alimbeba juu juu na kumtua kitandani kisha kumjaza lile kanga mdomoni ili tu asiweze kupiga kelele ambayo ingeweza kusikika kwa watu wasiohusika na ubazazi ule. Furaha ya nusura na tumaini la maisha ya stara ilitibuliwa. Ukawa mwanzo wa maisha ya sononeko, manyanyaso na upweke ulioshinda umri na kimo chake—akataifishwa usichana wake. 

Kazi yake ya kuwa kijakazi ikawa zaidi ya kupika. Aliongezewa majukumu ya kuwaburudisha wanaume wote waliokuwa wakiitembelea nyumba ile. Si kuwa aliwastarehesha kwa hiari yake, la hasha! Nusura alilazimishwa kwa kufungwa minyororo wakati fulani na kusukumwa kama mtamba kwenda kwa midume iliyo na roho za ibilisi. Si kazi ya bure aliyofanya, wala si kazi ya kumnufaisha yeye, kila mwanaume aliyemparamia alilipa fedha nyingi kwa mwajiri wake, Bi Raiya. Kama Nusura aliambulia pesa hizo basi ilikuwa ni harufu ya noti zile wakati ambao Bi Raiya alikuwa akizihesabu kibarazani.

Nusura alitamani sana kukutana na Zainabu pia Ramla ili angalau apate kuwaeleza yaliyomsibu. Tamaa ya kuwaona watu wale, nasaba ya atokako haikuwa rahisi. Kila alipotaka kuwasiliana nao kupitia kwa Bi Raiya hakupewa nafasi hiyo zaidi ya kupata kemeo kuwa, “Hupaswi kuzungumza na yeyote zaidi ya nitakaye mimi,” alisema Bi Raiya na kumfanya Nusura kubaki njiapanda.

Nchi ya kigeni ilimtenda, ilimpokea kwa bashasha na ilimgeuza kuwa zulia la kufutia uchafu wa kila namna. 

Nusura alikuwa kaketi kibarazani akiutazama ukuta uliokuwa ukimzuia. Ulikuwa ukuta mrefu na juu yake ulizungukwa na nyaya za umeme ambazo mtu hawezi kuzivuka akiwa salama. Ni hamu yake kuwa atoroke huenda huko nje ya ukuta angeliweza kupata msamaria wa kumrudisha nyumbani kwao. Bado aliugulia akilalama, “Nilidhani nimepata mwarobaini wa kuiondoa dhiki, kumbe nimeingia katika lango la dhiki! Ee Mola niokoe katika magumu haya,” alijisemea

Nusura angali yu katikati ya kilio.

Hali ya Nusura ilizidi kudhoofu akiwa mwenye mawazo mengi kumzidi. Uzuri wa sura yake ulianza kufifia tena, hata macho yake ya duara yaliyokuwa yameanza kuonekana na tumaini, yenye kumvuta na kumtia ashiki kila mwanaume yaligeuka na kuwa kama mashimo ya bao la kienyeji kama alivyokuwa huko Unguja. Alikonda na kuwa mwembamba zaidi ya alivyokuwa Unguja. 

Afya ya Nusura ilidhoofu. Hata alipopiga hatua alipepesuka kama mlevi. Midomo ilibabuka huku kikohozi kizito kikiwa sehemu ya maisha yake. Taratibu midomo ilianza kuota madonda huku akiuguza maumivu yasiyoisha katika sehemu zake za siri. 

Uzuri ulimpa taraka Nusura, alibakia na mwili kama gofu la kiumbe aliyeliwa na funza alipokufa porini. Hakuwa anatazamika tena, hata wanaume waliokuwa wakimfuata walikoma kama vile maji yakomavyo kutoka baada ya bomba kukatwa. Hodi zilikoma hata kule kuiona sura ya Bi Raiya ikawa kwa nadra. Sasa Nusura alinuka si kunukia; hakuvutia aliogopesha.

Siku ilifika, Nusura alikuwa kajilaza chumbani kwake. Alisikia sauti ya Bi Raiya akiwa anaongea kwenye simu. Alinyanyuka kitandani na kutega sikio lake kama jani la mgomba, “Hallo Zainabu, lofa wako ameisha, hana thamani tena. Amenyauka wala hawezi kuvutia tena, na ninavyoona atakuwa na ujauzito, sasa ufanye namna umtoe arudi kwao,” alisema Bi Raiya.

Nusura alishtuka na kulipapasa tumbo lake hasa baada ya kusikia kuwa huenda akawa na ujauzito. Nusura alikuwa msichana mbichi asiyetokwa ukoko wa utoto shingoni japo alikuwa kavunja ungo, sasa alikuwa mbichi wa miaka kumi na mitano wakati anaingia Oman. 

Mazungumzo ya Bi Raiya na Zainabu yalimfanya awaze na kuomba, hata kama kweli alikongoka na kuwa kama baiskeli mkweche, ni heri arudishwe kwao kuliko kufia ugenini na kutupwa kama mzoga. 

“Mungu, mja wako ninusuru na ubaya pamoja na dhiki zote hizi, nirudishe nyumbani,” aliomba Nusura akiwa anatingishika kwa njaa na kiu. Hakuwa na hadhi tena ya kupika na kupakua, vile vile hakuwa na hadhi ya kulishwa na kunyweshwa, zaidi alipaswa kufa kisha afungwe kwenye mifuko na kutwaliwa kwenye mashimo ya taka. 

Jioni ilipofika Nusura alimwona Bi Raiya kafika na mgeni ambaye alikuwa mwanaume. Alimjua mwanaume yule kuwa ndiye alikuwa hasa mpenziwe wa dhati. Kwa vyovyote hali ilivyokuwa, ilikuwa lazima kwa Bi Raiya kuingia ndani hadi chumbani na bwanake wakafurahishana. Muda huo ndio Nusura aliutumia. Walipoingia chumbani, alitoka taratibu hadi kwenye ile gari ya mgeni. Nusura alikusudia kutoroka. Alifungua buti la gari ile ambalo halikufungwa baada ya Bi Raiya kupokea kasha la zawadi kutoka kwa bwanaye. Nusura alichupa ndani na kulifunga akingoja mwanaume yule akitoka basi iwe salama yake kuwa nje ya jumba lile la dhiki na mateso. Kweli ilikuwa.

Gari ambayo Nusura alikuwa ndani yake ilimchukua hadi kwenye hoteli moja ya kitalii. Iliegeshwa mahali palipokuwa na maua mengi marefu. Aliposikia waliokuwa ndani ya gari wametoka na kuelekea walikokusudia, Nusura alipachua kichuma ndani ya buti lile na kulifungua. Alichungulia nje kama nguchiro kwenye kichuguu. Alibaini kuwa mahali pale palikuwa na mchanganyiko wa vurugu na utulivu. Alichoropoka kutoka ndani ya gari na kuambaa kinyonge akidemadema kama mlevi aliyeupiga mtindi ukamkalia kila sehemu ya maungo ya mwili wake. Alitokomea gizani.

Nusura alipoliingia giza nalo giza lilimmeza hata asione alikokuwa akielekea. Njia aliyoifuata Nusura ilikuwa ni kichochoro kilichomwelekeza kuliko majumba ya malofa, wasio na umeme wala taa za kandili ila tu walitumia mishumaa na vibatari. Alipoona mwili umechoka, alijivuta akaegemea mti wa mtende ndipo baridi na upepo wa usiku kuchwa vilimwishia.

 

 

 

V

 

NUSURA HAKUJUA ni wakati gani aliokotwa. Alipofumbua macho aliona kuwa yupo sehemu iliyozungukwa na vyuma. Sakafuni palikuwa na baridi kali lililomfanya atingishike kama kifaranga kilichoopolewa kutoka kwenye ndoo ya maji. Alipojaribu kusimama ndipo alipobaini kuwa alikuwa kituo cha polisi. Mbele yake kulikuwa na askari akiwa tayari kumchukua maelezo. Akamuuliza, “Unaitwa nani?”  

Nusura alijieleza. Kila kitu alichokieleza kilikuwa kigumu kufahamika. Lugha hakuwa akiielewa hadi pale alipotafutwa mkalimani akawezesha mazungumzo hayo. Nusura alitaja wazi maovu yaliyomkuta hadi kutoroka kutoka ndani ya jumba lile. Alitaka watu wale kuadabishwa lakini walimtaka kwanza awapatie dola mia tatu ndipo waweze kutekeleza alilolitaka, na kama hakuwa na kitu basi ilimpasa kwenda jela kwa miaka mitatu kwa kuwa nchini Oman bila kibali. 

Nusura moyo ulisinyaa. Dhiki aliyoikimbia aliikuta ikimngonjea tena sehemu aliyoamini atanusurika. Akaambiwa, “Huna hati ya kusafiria na viza ya kuingia Oman; huna kibali cha kazi na umeonekana kufanya ukahaba kinyume na taratibu za Oman; unapelekwa mahakamani,” alisema askari mmoja.  

Nusura aliinama. Alilia kwa nguvu. “Vitu vyote anavyo Zainabu na Bi Raiya,” alijitetea Nusura.

“Unataka kuwatoroka? Ngoja, cha moto utakiona,” alisema askari mmoja mwenye sura iliyojaa makunyanzi. Alifungua kitabu cha usajili wa majina ya watu mbalimbali ambao ni wageni. “Unaitwa Nusura Haroub Mkiwa, mkazi wa Zanzibar, umekuja kufanya kazi. Kafala—mdhamini wako ni Zainabu Majid, mfanyabiashara Oman kati,” alieleza askari yule na kumfanya Nusura akubali kwa kutingisha kichwa. “Basi napiga simu sasa ili wakukute hapa,” aliongeza askari yule.

Askari yule alinyanyua mkonga wa simu baada ya kubonyeza vitufe vya namba huku akisoma kwenye karatasi zilizokuwa mbele yake. Akapiga simu na ikapokelewa. 

“Hallo, naongea na Zainabu Majid?” aliuliza askari na alijibiwa. “Unatakiwa ufike kituo cha polisi haraka, sasa hivi,” askari alikata simu.

Baada ya taktibani dakika ishirini, Zainabu na Bi Raiya waliwasili. Sura zao zilijaa ndita na walikuwa na kisirani kisichofichika. Kuanzia hapo kukawa na sokomoko. 

“Nusura kaniibia dola alfu moja,” alisema Bi Raiya.  

Nusura yalimfikia maneno yale, yalimwingia na kumchoma vikali. Badala ya yeye kuwa alipwe dola takribani alfu moja na mia tano kwa muda aliofanya kazi, alishitakiwa kuwa aliiba pesa za Bi Raiya. Hakutokwa na neno zaidi ya kumwaga chozi lililozidi kuifubaza sura yake. Akawaza kuwa ni heri angekuwa lofa kisiwani Zanzibar kuliko kuwa mhanga wa dhiki ugenini.

“Lazima atafungwa—miaka mitatu jela,” alisema askari kwa kusisitiza. Zainabu alimtazama Nusura kwa jicho la kuibia. Hakutaka kumtazama barabara kwani alihisi aibu. Dhamira yake upande mwingine ilimsuta. Zainabu alikumbuka jinsi alimtoa Nusura kwao akiwa na tumaini la kujipatia riziki. Akatokwa na kauli akisema, “Msimfunge, kwa kumhurumia huyu yatima, tumkatie tiketi arudi kwao.”

Nusura alimshukuru Mungu hata kwa kauli ile iliyorejesha tumaini tena kwake. Alikusanya mikono na kushukuru kwa kuiinua juu. “Asante Maulana. Nirejeshe nyumbani salama,” alisema Nusura kimoyomoyo.

Nusura alichukuliwa baada ya hati yake ya kusafiria kuwa imewasilishwa na Zainabu. Alipelekwa hadi ulipo uwanja wa ndege wa Muscat. Alipandishwa kwenye ndege na safari ya kurudi Unguja ilianza. Aliondoka kwa kishindo na furaha nyingi nyumbani sasa alirudi kwa unyonge, tena kwa kimya kisichokuwa na hodi.

 

 

 

VI

 

ALIPOTIA MGUU UNGUJA, Nusura alimkuta kakaye Nuru akiwa karudi kutoka Bara Uropa. Hali aliyoitarajia arudi nayo haikuwa ambayo alimkuta nayo. Safari yake barani Uropa ilikuwa ya mahangaiko na dhiki nyingi. Huko naye alikutwa na masaibu yasiyo hesabika. 

Nuru alimweleza dada yake kuwa, “Uropa si mahali salama kwa wasiohitajika, malofa kama nilivyokuwa nikiitwa. Huko niligeuzwa mtumwa; nikifanya kazi na aliyelipwa ni yule mzungu aliyenidhamini kuwa mimi ni mchumba wake. Sikuwa na haki ya kutoka ndani na kwenda matembezini. Kila muda alinichunga na kunilinda kama mfugo wake. Sikuweza hata kuwa na rafiki wapya kwa jinsi alitegesha kamera kila mahali akinilinda nilitoke.

Kila nilichokimwagia jasho jingi, mwanamke yule alilipwa kupitia akaunti yake ya benki. Nilibaki na dhiki isiyokuwa na mfano. Nilichuuzwa na kuwa mtumwa wa kumstarehesha mwanamke yule na rafikize kama mme bwege,” alieleza Nuru angali na simanzi imemzunguka.

“Pole kaka, mimi nawe tutakuwa tumejifunza. Si kweli kuwa Uropa na Arabuni kuna neema kwa malofa wote waishio Zanzibar na kote ulimwenguni—wapo ambao hubahatika lakini wengi huishi kwa shida. Hilo ni lango la dhiki, lango liendalo gizani kwa tumaini la mwanga uonekanao kwa mbali kama chambo—hata giza linao mwanga wake. Ni heri kubaki hapa tukajibidisha na kudunduliza japo kidogokidogo tukawa na furaha,” alisema Nusura aliyenusurika dhidi ya hali mbaya iliyokuwa ikimwandama tangia atie mguu Oman.

Bi Sofia ambaye alikuwa kapooza bado alikuwa na hangaiko lake. Japo Mungu alimtunzia uhai, bado aliendelea kuwaombea dua wanawe ili siku ije wapate nafuu ya maisha. Pesa kidogo ambazo alikuwa akizipata Nuru baada ya kurudi na kuanza shughuli ya uvuvi, kwa mwezi ule mmoja na nusu, zilimsaidia kupata japo baiskeli ya miguu mitatu. Mwezi uliofuata walimchukua na kumpeleka tena hospitalini ambako waliendelea kumchunguza kisha kumpatia tiba. Japo hakuweza kusimama tena, angalau sasa aliweza kukaa na mikono yake ilishika vitu huku hali ya kupooza taratibu ilitoka na akawa na ulemavu wa viungo wa kuvumilika bila adha nyingine.

 Hakuisha kuwausia wanawe akisema, “Wanangu, mkataa kwao mtumwa. Msidhani kuwa waliosema zimwi likujualo halikuli likakwisha walikuwa zumbukuku, hapana. Watu wale walijua kuwa, ukiwa kwenu hata kama utapata shida na dhiki, heri kuliko kuwa ugenini wasikokujua. Dhiki ya mwenye tamaa huzaa laana. Mtu kwao, pendeni mlipozaliwa,” alieleza Bi Sofia kisha walicheka kwa furaha.  

Wakati wanataka kuingia ndani, walisikia mshindo wa mtu kwa nyuma yao—alikuwa Ramla. Haliye haikuwa ya kutamanika kama alivyokuwa awali. Alikuwa kachoka na nguo zilipepea mwilini kama bendera. Nuru alipomuona alishtuka. Lakini kabla ya kusema neno, Ramla alipiga magoti chini akaanza kulilia msamaha kwa Nuru na Nusura. Alisema, “Sikujua kama utapata mateso yote hayo kwakuwa sikuwa nimejua. Hata mimi yamenipata yaliyokukuta wewe—Zainabu si mtu mwema. Alituchuuza na kutufanya watumwa ugenini. Nuru, nisamehe mme wangu. Nilipaswa nikushauri baada ya kukuvumilia lakini sasa nimepatwa na makubwa. Naugua!”

Nuru alitoa macho. Akamsogele Ramla aliyesema, “Hustahili hata kunigusa—nimeambukizwa Ukimwi.”

Nuru aliinama na chozi likamponyoka. Naye akayakumbuka yake—naye akasema, “Hata mimi ni kama wewe. Tamaa iliniponza!”

Nyumba ya Bi Sofia ilikumbwa na simanzi Nusura alipoeleza kuwa ana ujauzito aliotoka nao Oman. Kila mmoja akaweka mikono kichwani. Wachuma janga ugenini wakarejea kula na wa kwao! Iliwapasa kusameheana kisha kuyaanza maisha mapya. Ramla akairejea ndoa yake. Nusura alilea ujauzito na kupata mtoto wa kiume akamwita, Haroub. Wakashikama wote na kuahidi kuishinda dhiki kwa kuitafuta riziki.




 




 





 


0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post