Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Kama mambo yakienda yalivyopangwa kipa Mcameroon, Simon Omossola (25) anaweza kusaini Simba muda wowote kuanzia sasa. Lakini kikosi kikiendelea kujifua Uturuki leo kinatarajia kuwapokea mastaa wanne wakiwemo watatu wapya.
Mwanaspoti linajua Simba imeachana na dili la kipa Mbrazili Caique da Santos kwa sababu mbalimbali ikiwemo kigezo cha lugha, lakini sasa iko siriazi na Omossola aliyesaini miaka miwili na FC Saint Eloi Lupopo Krismasi iliyopita.
Habari zinasema mezani Simba yamebaki majina ya makipa wawili moja ni wa Lupopo aliyetoka AS Vita ya DR Congo, Omossola na lingine ni la Mbrazil mwingine aliyependekezwa na kocha Robertinho baada ya dili la Caique kukwama.
Hata hivyo, Omossola anaonekana kupigiwa chapuo na viongozi wengi wa jopo la usajili hivyo wakiafikiana huenda akawa mbadala wa Beno Kakolanya na atakayeziba pengo la Aishi Manula anayeuguza majeraha hadi Novemba.
Simba inaamini uzoefu wa Omossola katika mashindano ya Afrika na timu ya taifa ya Cameroon vitaisaidia kufikia malengo.
Pia Omossola anazungumza Kiingereza na Kifaransa, hivyo itakuwa rahisi kuwasiliana na mabeki ingawa dau lake linatajwa si chini ya Sh400 milioni.
KAMBINI
Mfungaji bora (mabao 16) na mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda msimu uliopita, Mcameroon Willy Onana aliyetua kutoka Rayon Sports, winga Muivory Coast Kramo Aubin aliyetokea Asec Mimosas na beki Mcameroon Che Malone Fondoh aliyetokea Coton Sports ndio watakaojiunga na kambi leo huku wakiambatana na Mkongomani Jean Baleke aliyejiunga Simba katika dirisha dogo la msimu uliopita na kuifungia mabao nane kwenye ligi.
Mastaa hao waliondoka nchini jana alfajiri na leo watajiunga na timu kuanza kujifua sambamba na 17waliotangulia awali hivyo kikosi kufikisha wachezaji 21.
ISHU YA CHAMA
Awali Kramo, Onana, Baleke na Che Malone walitakiwa kusafiri msafara mmoja na staa wa timu hiyo, Clatous Chama kutokea Tanzania, lakini jambo hilo lilikwama na Chama kubaki nchini lakini muda wowote kuanzia leo atakwenda.
Hata hivyo, imefahamika kuwa Chama amemalizana na viongozi wa Simba katika kikao kilichofanyika jana na sasa atapewa mkataba mpya wenye mabadiliko kwenye baadhi ya vipengele pamoja na mshahara.
Baada ya Simba kumaliza sakata hilo, Chama anatarajiwa kusafiri na baadhi ya viongozi wa Simba sambamba na kiungo mpya Fabrice Ngoma hadi uturuki kambini tayari kwa kuanza kazi upya. Wote watapokewa na benchi la ufundi chini ya kocha msaidizi Ounane Sellami aliyeachiwa timu na kocha mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kwa muda.
Post a Comment