Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wanaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo mkabaji wa Singida Big Stars, Yusuf Kagoma katika kuelekea dirisha kubwa la usajili.
Young Africans imepanga kukiboresha zaidi kikosi chake ili kifanye vema katika msimu ujao, ambao wanakwenda kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hiyo, tayari imeanza mazungumzo na baadhi ya wachezaji huku wengine wakiwapa mikataba ya awali kwa ajili ya kuwasajili kati ya hao yupo mshambuliaji wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Young Africans, mabosi wa timu hiyo, wapo katika majadiliano ya kumsajili kiungo huyo mkabaji mzawa mwenye uwezo wa kunyang’anya mipira na kuchezesha timu.
Chanzo hicho kimesema kuwa wamewaangalia viungo wote katika msimu huu, na kumuona Kagoma ndiye bora zaidi ya wengine.
Kimeongeza kuwa kikubwa wanataka kujiimarisha kwa ajili ya michuano ya kimataifa na kitaifa watakapocheza katika viwanja vigumu nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
“Katika timu tunahitaji kuwa na wachezaji wazawa wenye uwezo na uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa na mashindano ya ndani ambayo tunakwenda kushiriki katika msimu huu.
“Hivyo tunategemea kuanza mazungumzo na menejimenti ya Kagoma kuona uwezekano wa kuipata saini yake katika usajili huu mkubwa utakaofunguliwa hivi karibuni.
“Tumepata taarifa za awali kuwa Kagoma mkataba wake ulimalizika mara baada ya mchezo wa mwisho wa ligi ambayo ilimalizika Ijumaa iliyopita, hivyo tupo katika nafasi nzuri ya kuipata saini yake,” kimesema chanzo hicho.
Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said hivi karibuni alizungumzia usajili kwa kusema kuwa: “Kama uongozi tutafanya usajili kwa kufuata mapendekezo ya kocha, tupo tayari kumsajili mchezaji yeyote tutakayemuhitaji.”
Chanzo: Dar24
Post a Comment