Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Meneja wa Idara ya Digital wa Klabu ya Yanga, Priva Abiudi Shayo (Privaldinho) amesema kuwa timu yao haina presha kuelekea mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Mabingwa Afrika dhidi ya USM Alger licha ya kufungwa mchezo wa kwanza.
Priva amesema hayo wakati kikosi cha timu hiyo kikiondoka nchini kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi nchini humo huku akiongeza kuwa wanayo matumaini makubwa na wanaamini wataibuka na ushindi.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jumapili iliyopita katika Dimba la Mkapa, Yanga ilifungwa bao 2-1, hivyo katika mchezo wa mkondo wa pili inahitaji ushindi wa angalau bao 2-0 ili iweze kujihakikishia kunyakua ubingwa huo.
“Watu wanaweza kudhani kwamba Yanga imekata tamaa, hapana, sisi tuna matumaini na malengo, kwa hiyo tunakwenda kupambana kuhakikisha tunatimiza malengo yetu.
“Kama tuliweza kupata matokeo Tunisia, Nigeria na Afrika Kusini hatuwezi kushindwa Algeria. Watu wajue kwamba hakuna klabu nyingine kwenye haya mashindano kuanzia hatua ya makundi ambayo imeshinda mechi tatu ugenini, kwa hiyo niwaambia Wanayanga wala wasiwe na presha.
“Tunajivunia nafasi tuliyofika na historia ambayo tumeiweka kwenye soka la Tanzania, ni lazima tupambane kuhakikisha tunapata matokeo. Tukishinda tutamshukuru Mungu, tukifungwa pia tutamshukuru Mungu, chochote tutakachokipata sisi tupo tayari kupokea.
“Kwa hapa tulipofikia ni mafanikio makubwa na tunapaswa kujipongeza na kujivunia, tukishinda ni kama tumeshinda na tukifungwa ni kama tumeshinda,” amesema Privadinho.
Post a Comment