Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Licha ya Yanga kukubali kumuuza kiungo mshambuliaji, Feisal Salum 'Feitoto' kwenda Azam FC, timu hiyo bado itaendelea kula fedha wakati nyota huyo atakapouzwa ndani au nje ya nchi.
Yanga ilimuuza Feitoto kwa Azam FC kwa dau lililofichwa kwa pande hizo mbili, lakini waliwekeana vipengele ambavyo timu hizo zitaendelea kunufaishana kwa mchezaji huyo.
Habari ambazo Mwananchi limezipata ni kwamba kwenye mkataba wa mauziano, Yanga imeweka kipengele kwamba ikitokea Feitoto anauzwa, basi klabu hiyo itapata sehemu ya fedha ya usajili.
Chanzo ndani ya Yanga kililidokeza gazeti hili kwamba Ikitokea Azam ikamuuza Feisal nje ya nchi, klabu hiyo itapata asilimia 25, hivyo kuwa biashara nzuri kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa hawataki kuona mchezaji huyo akicheza timu nyingine hapa nchini zaidi ya Azam FC, hivyo kuweka kipengele kigumu lakini chenye faida.
"Kwa hapa ndani tumeweka kwamba akienda katika timu yoyote ile, basi tunachukua Sh1 bilioni, iwe kwa mkopo au kuuzwa," kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe kuzungumzia jambo hilo simu yake iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi kwenye mtandao wa Whatsapp alijibu meseji ya salamu na alipoulizwa jambo hili alitoka hewani.
Habari ambazo Mwananchi limepenyezewa ni kwamba Yanga pia imelipwa Dola za kimarekani 130,000 ambazo kni takribani Sh300 milioni.
Feisal amesaini mkataba wa miaka mitatu, ambao utamfanya akae kwenye timu hiyo ya Chamazi hadi 2026.
Chanzo: Mwanaspoti
Post a Comment