Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Habari njema kwa wachezaji wa Kitanzania wenye ndoto ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya kutokana na taarifa za ujio wa makocha wa timu za vijana za klabu ya Valencia CF inayoshiriki Ligi Kuu Hispania 'La Liga' kwa lengo la kusaka na kunoa vipaji vya wachezaji wa kike na kiume.
Makocha hao wabobezi kwenye soka la vijana watakuwa nchini kwa siku tano kuanzia Julai 24 hadi 29 kwenye viwanja vya JK Youth Park jijini Dar es Salaam.
Akiongea na Nje ya Bongo, mmoja wa makocha hao, Miguel Martinez 'Mista' alisema wanasubiri kwa hamu safari ya kuja Tanzania kutokana na mazuri ambayo wameyasikia kwa nchi hiyo ya kitalii ikiwa pamoja na wachezaji waliojaliwa vipaji,"Naamini itakuwa wiki ya kipekee kuwa Tanzania, tumejiandaa kutoa elimu kwa wachezaji ambao watajitokeza ili kujua nini ambacho soka la Ulaya inahitaji,"
"Kwa wale ambao tutavutiwa nao tunaweza kuona njia bora za kuwasaidia zaidi baada ya kempu, kama kutakuwa na mwenye kipaji kikubwa zaidi hatuwezi kusita kuondoka naye, tumesikia mengi mazuri kuihusu Tanzania na binafsi natambua ubora wa vipaji kutoka Afrika ni mambo machache sana ambayo yamekuwai changamoto kwa wachezaji wa Afrika na yote hiyo ni kukosa misingi angali wakiwa wadogo,"
"Wachezaji wengi wa Kiafrika wanavipaji asilia, mpira siku hizi umebadilika unahitaji mchezaji kuongezewa mambo ya msingi ili kipaji kifanye kazi vizuri na kwa ukuba wake," alisema kocha huyo. Mista, ni mwanasoka wa zamani wa Hispania ambaye alicheza kama mshambuliaji, kwa sasa ni miongoni mwa makocha wa timu hizo za vijana za Valencia.
Alianza maisha yake ya soka akiwa na timu ya vijana ya Real Madrid lakini akajijengea jina akiwa na Valencia, akiisaidia klabu hiyo kushinda jumla ya mataji manne makubwa katika kipindi cha miaka mitano na kufunga jumla ya mabao 48 katika michezo 218 ya La Liga kwa misimu kumi. Hivyo ni kocha mzoefu.
Valencia CF ni miongoni mwa timu ambazo vijana wake wanafanya vizuri kwenye soka la vijana la Hispania mfano mzuri ni, Valencia Juvenil A chini ya miaka 19 ambao wamemaliza msimu wakiwa vinara wa kundi lenye timu 16, vinara wa makundi mengine ni Las Palmas, Real Madrid, Real Betis, Barcelona, Athletic na Celta Vigo.
Akademi ya Valencia imetoa wachezaji wengi wakubwa barani Ulaya na miongoni mwao ni pamoja na David Silva ambaye alikiwasha akiwa na Manchester City ya England kabla ya kutua Real Sociedad, Isco alitamba akiwa na Real Madrid kabla ya kupotea kwenye soka la ushindani na Raul Albiol yupo Villarreal.
Katika moja ya mahojiano yake, Mkurugenzi wa akademi ya Valencia CF, Luis Martinez aliwahi kueleza muundo wa kipekee wa akademi hiyo unavyosaidia kupunguza matumizi makubwa ya fedha," Ni jambo zuri na kubwa kwetu kutengeneza vijana ambao watakuwa msaada...,"
Valencia CF wamekuwa na programu ambazo wamekuwa wakizitoa kwenye mataifa mbalimbali kwa lengo la kueneza utamaduni wa soka lao, wamekuwa wakifanya hivyo kwa zaidi ya miaka mitano.
Hemed Tawah ambaye ni Mtanzania na madau wa Nje ya Bongo alisema ujio wa jopo la makocha wa vijana wa Valencia ni fursa kwa Watanzania hivyo wanapaswa kuichangamkia lakini pia alifichua kwamba atakuwa sehemu ya msafara huo kama mwenyeji, "Sidhani kama naweza kutingwa kiasi cha kushindwa kuja Tanzania kwa ajili ya jambo hili, wachezaji wapata elimu na wale ambao watawavutia pengine wataondoka nao,"
"Yapo mambo mengi mzuri ambayo nimeyaona na yanaweza kuwa na faida kwa nchi yangu, utaratibu kwa mchezaji ambaye anataka kuwa sehemu ya mpango huu wanatakiwa kujisajili kuwasiliana na mimi kupitia barua pepe hemedtawah@spanishprofootball. com, au wanaweza kunicheki Whatsapp kwa namba +225784508548 ili niwape usaidizi juu ya namna ya kufanya," anasema.
Chanzo: Mwanaspoti
Post a Comment