Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema ipo mbioni kuanza marekebisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ili kuurudishia hadhi yake.
Waziri wa wizara hiyo, Dk. Pindi Chana, aliliambia Bunge, jijini hapa jana wakati anahitimisha bajeti ya Michezo alisema ujenzi utaanza mara moja baada ya kumalizika kwa mechi kati Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Niger.
Alisema uwanja huo sasa utatumika katika mechi za kimataifa na michezo mingine itacheza kwenye viwanja mbadala ili kuupunguzia mzigo na kuepusha kuharibika.
Aliongeza serikali pia itajenga viwanja vya mpira vyenye hadhi za kimataifa viwili katika mkoa wa Dodoma na Arusha ikiwa ni maandalizi ya kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwaka 2027.
“Ili ukidhi AFCON unahitaji viwanja nane vya kimataifa, lakini kwa kuwa tumeomba pamoja na Kenya na Uganda tukichanganya vitatimia, wanatarajiwa kuja wakaguzi kutoka CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika) kuona namna gani tumekidhi vigezo,” alisema Chana.
Aliongeza wanaipa kipaumbele suala la ushiriki wa michezo katika shule za msingi na sekondari na kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kila shule inatakiwa kuwa na kiwanja cha michezo ili watoto wapate fursa ya kushiriki vyema.
Pia Chana alisema wizara yake imeunda kamati ya kuratibu vazi la taifa ili kuharakisha mchakato huo na imeshawapa maagizo ya kuharakisha vazi hilo linapatikána na hivi karibuni watawasilisha ripoti maalum kuhusiana na maoni waliopokea kutoka kwa wadau.
Alisema pia wana mpango wa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili kuweka utaratibu wa kutoa vibali kwa wadau wanaotaka kuendesha mashindano ya Ndondo kwa sababu michuano hiyo ni moja ya sehemu ya inayozalisha vipaji.
Akijibu baadhi ya hoja za wabunge, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ alisema wizara hiyo imeshaanza kufanya mawasiliano na Wizara za Fedha, Nishati na Madini ili kukamilisha ujenzi wa viwanja vikubwa viwili vitakavyojengwa Arusha na Dodoma huku pia wakijipanga kufanya ukarabati viwanja vilivyoharibika.
Chanzo: Dar24
Post a Comment