Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Kila wachezaji wa kigeni wanapofanya vizuri, kuna mjadala fulani ambao umekuwa ukiibuka ambapo baadhi ya watu hudai kuwa wanaua vipaji vya wachezaji wazawa.
Kwamba uwingi wa wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu unasababisha kushuka viwango kwa wachezaji wazawa na hivyo inaleta athari kwa timu ya taifa.
Sawa ni uhuru wa watu kutoa maoni lakini hoja hii huwa inashangaza sana na inaonekana hawa wanaotaka idadi ya wachezaji kigeni ipungue huwa wanaendeshwa na mihemko tu.
Jaribu kuwaza kitu kimoja. Kila timu katika ligi inaruhusiwa kusajili wachezaji 12 tu wa kigeni kati ya 30. Maana yake kila moja ikiwa na wachezaji 12 wa kigeni, idadi ya jumla ya wageni kwenye ligi yetu itakuwa ni 192 ambao hawafiki hata nusu ya idadi yote ya wachezaji wa ligi kuu ambao ni 480.
Kwa hesabu hiyo ya kawaida tu, maana yake wachezaji wazawa ni wengi zaidi kwenye ligi yetu maana ikiwa kila timu itasajili wageni 12, idadi ya wachezaji wazawa itakuwa ni 288.
Lakini kiuhalisia, wachezaji wa kigeni hawazidi 90 kwani ni timu zisizozidi nne zinazoweza kila moja kuwa na wachezaji 12 wa kigeni na kuna timu hazina kabisa wageni.
Tuachane na hayo masuala ya hesabu sasa tuangalie kilichopo. Licha ya kuaminishwa kuwa wageni wanabania nafasi za wazawa, pale Simba na Yanga kuna wazawa wamekuwa ni Wafalme na hawashikiki hivi sasa licha ya uwepo wa hao wageni.
Pale Yanga, mabeki wanne ambao wanaunda safu ya ulinzi wote ni wazawa ambao ni Dickson Job, Kibwana Shomary, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca lakini yupo Mudathir Yahya anayetamba kwenye eneo la kiungo.
Ukienda Simba pale, kuna Mzamiru Yassin amekuwa wa moto kwelikweli na ndani ya Azam FC, Sospeter Bajana ana uhakika wa nafasi na anafanya vizuri.
Hawa hawajakubali kumezwa na mikwara kuwa wageni wanabania nafasi zao. Wamevuja jasho na wakajihakikishia namba kiasi cha kuwafanya wale waliokuwa wanashikilia msimamo wao kuhusu wageni kuwa kimya sasa hivi.
Chanzo: Mwanaspoti
Post a Comment