Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema wamefanya maandalizi ya kucheza fainali ya kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya USM Alger katika uwanja wa Benjamin Mkapa hapo kesho
Akizungumza katika Mkutano maalum na Wanahabari kuelekea mchezo huo, Nabi alisema wamefanya maandalizi maalum ya kimbinu kwa kuzingatia ubora na udhaifu wa USM Alger
"Tumejiandaa kwa ajili ya mchezo wa fainali dhidi ya USM ALger. Maandalizi tumeyagawa katika sehemu kuu tatu, ya kwanza ni utimamu wa mwili wa mchezaji, kumjua mpinzani na tatu ni mbinu gani za kutumia kumkabili, " alisema Nabi
Aidha alithibitisha kumkosa kiungo Khalid Aucho ambaye atakosa mechi zote mbili za fainali baada ya kuwa na kadi sita za njano
Nabi amesema ni pigo kwa kikosi chake kumkosa Aucho lakini amesema uwepo wake nje utakuwa na faida kutokana na uzoefu, atawasaidia wachezaji wenzake ili kuhakikisha wanafanya vizuri
Nabi ameeleza kujivunia mshambuliaji Fiston Mayele katika kikosi chake akiamini kinara huyo wa mabao katika michuano hiyo ni mmoja wa washambuliaji bora barani Afrika kwa sasa
"Tuna bahati kuwa na Mayele kwenye kikosi chetu, ni mshambuliaji wa daraja la juu Afrika, Uzoefu wake pamoja na wachezaji wengine utakuwa msaada mkubwa kwetu kwenye hatua hii ya Fainali, "aliongeza Nabi
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, beki Dickson Job amesema benchi la ufundi limemaliza kazi katika viwanja vya mazoezi, sasa ni jukumu lao wachezaji kuhakikisha wanatekeleza kile walichoelekewa ili kuweza kushinda
"Tayari walimu wametupa maelekezo ya nini tunapaswa kufanya ndani ya uwanja. Kazi imebaki kwetu wachezaji kwenda kupambana ili tushinde mchezo huo," alisema Job
Post a Comment