Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Licha ya ushindi mnono wa mabao 4-1, Pamba imeondolewa kwenye mechi za mtoano kusaka nafasi ya kwenda Ligi Kuu, huku Mashujaa ya Kigoma ikisonga mbele.
Mashujaa imesonga mbele kufuatia ushindi wa jumla wa mabao 5-4 baada ya kupata ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kufuatia ushindi huo, sasa Mashujaa inasubiri timu itakayocheza nayo kwenye playoff kutoka Ligi Kuu na endapo ikipata ushindi wa jumla kwenye michezo miwili itakuwa imepanda daraja.
Pamba imepata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mashujaa ya Kigoma leo (jana jumapili) kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza katika mchezo wa marudiano ambao umepigwa kuanzia saa 10 jioni.
Mchezo huo ambao umechezeshwa na Mwamuzi, Benedicto Magai umegubikwa na matukio yaliyoibua hisia za mashabiki ikiwamo kuipa Pamba penalti mbili ikiwemo moja ambayo kipa wa Mashujaa ameokoa lakini ikaamuliwa irudiwe huku mchezaji wa Mashujaa, Athumani Dunia akilimwa kadi nyekundu.
Pamba imetangulia kupata bao mapema dakika ya tano kwa penalti likifungwa na Rogers Gabriel ambaye alifunga tena kwa penalti mnamo dakika ya 47, huku Bruno John akifunga bao la tatu dakika ya 65 na Dany Teffe akifunga la nne dakika ya 73.
Bao la dakika ya 55 ambalo limefungwa na Mohamed Stambuli 'Banka' limezamisha matumaini ya Pamba huku likiipa Mashujaa FC ushindi wa jumla wa mabao 5-4.
Msimu huu timu hizo zimekutana mara nne, ikiwamo michezo miwili ya Ligi ya Championship ambayo Pamba alishinda yote kwa mabao 2-0 kila mchezo, Kisha ushindi wa leo wa mabao 4-1 huku Mashujaa ikishinda 4-0 mchezo wa kwanza wa Playoff.
Tumaini pekee la Pamba sasa limebaki kwenye busara ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ambalo tayari limepokea maombi ya timu hiyo yaliyotumwa Mei 16, mwaka huu kuomba ufafanuzi wa kanuni na uchunguzi sakata la upangaji matokeo linalomhusu mmiliki wa timu ya Kitayosce ya Tabora, Yusuph Kitumbo ambayo imepanda daraja kwenda Ligi Kuu.
Pamba ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi ya Championship msimu huu, huku vinara, JKT Tanzania na mshindi wa pili, Kitayosce zikipanda moja kwa moja kwenda Ligi Kuu, huku Mashujaa ikikamata nafasi ya nne.
Chanzo: Mwanaspoti
Post a Comment