Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wanaendelea kupata Baraka za kutoboa Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu, kufuatia uwezo na kiwango walichokionesha kwenye michuano hiyo.
Young Africans itacheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USMA Jumapili (Mei 28), kisha itakwenda Algeria kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Juni 03.
Baraka za safari hii kwa Young Africans zimetolewa na Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Sudan Al Hilal Omdurman ya nchini Sudan, Florent Ibenge ambaye anaamini Wananchi wana kila sababu za kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho na kuweka historia ya kipekee kwa Tanzania.
Ibenge ambaye msimu uliopita alitwaa Ubingwa wa Michuano hiyo akiwa na RS Berkane ya Morocco, amesema anaipa nafasi kubwa Young Africans kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, kutokana na aina ya wachezaji waliokuwepo hivi sasa, ambao wengi wao anawafahamu.
Ibenge amesema wachezaji hao baadhi wamepita katika mikono yake akiwafundisha katika kikosi cha AS Vita ya DR Congo ambao muda wowote wanaweza kukupa matokeo mazuri ya ushindi.
Ameongeza kuwa, kama ikitokea Young Africans ikapoteza ubingwa wa Michuano hiyo, basi itakuwa bahati mbaya, lakini wana uwezo mkubwa wa kuubeba msimu huu.
“Mimi ninaifahamu vizuri sana Young Africans, na hiyo imetokana na aina ya wachezaji ambao wanao msimu huu, wengi wao ninawafahamu, niliwahi kuwa nao AS Vita.
“Sioni kama wana cha kupoteza katika mashindano haya ya Kombe la Shirikisho Afrika, wana uwezo mkubwa wa kubeba kombe hili, kama ikitokea wakilikosa basi bahati mbaya.
“Kikubwa wanachotakiwa wachezaji hao waamue matokeo mazuri wakiwa uwanja wa nyumbani watakapoanzia kabla ya kurudiana ugenini,” amesema Ibenge
Baadhi ya wachezaji ambao Ibenge amewafundisha na sasa wanaitumikia Young Africans ni Fiston Mayele, Tuisila Kisinda, Yanick Bangala, Bernard Morrison, Jesus Moloko na Djuma Shaban.
Post a Comment