Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Kocha Mkuu wa Simba SC Robertinho ameanza kuhusishwa na mpango wa kusajili baadhi ya wachezaji ambao watakiboresha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na Michuano ya Kimataifa.
Simba SC msimu huu 2022/23 imeshindwa kuchukua Kombe lolote baada ya kutolewa kwenye Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kabla ya kutupwa nje pia katika hatua ya Nusu Fainali Kombe Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ huku matumaini ya ubingwa wa Ligi Kuu yakitoweka kutokana na kuzidiwa alama saba na watani wao wa jadi, Young Africans.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil anatajwa kuwa katika mipango ya kumsajili Kiungo Mshambuliaji kutoka Uganda na Klabu ya Vipers SC Milton Karisa, kuelekea msimu ujao.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Uongozi wa Simba SC, zimeeleza kuwa tayari Robertinho ameshawasilisha kwa uongozi majina ya wachezaji anaowataka akiwamo Karisa ambaye amewahi kufanya naye kazi Vipers SC.
“Robertinho ameshamaliza awamu ya kwanza ya majina ya wachezaji ambao anawataka kwa ajili ya msimu ujao na amefanya haraka kutokana presha kubwa ambayo ipo ndani ya timu baada ya kufanya vibaya.”
“Miongoni mwa majina ambayo amekabidhi kwa uongozi yupo yule mshambuliaji wa Vipers ya Uganda kwa sababu moja ya maeneo anayotaka kuweka sawa ni la ushambuliaji na ikizingatiwa uwapo wa michuano mikubwa ambayo ipo mbele yetu,” kimeeleza chanzo cha taarifa hii
Wengine wanaotajwa kupendekezwa na Kocha huyo ni beki wa kati wa Rayon Sports ya Rwanda, Abdul Rwatubyaye, kiungo wa Geita Gold, Edmund John na kipa wa Vipers FC ya Uganda, Alfred Mudekereza.
Wakati mpango huo wa Usajili ukianza kushika kasi ndani ya Simba SC, wachezaji wanaotajwa huenda wakaachwa mwishoni mwa msimu huu ni Joash Onyango, Nassoro Kapama na Habib Kyombo.
Wengine ni Mohammed Ouattara, Jimmyson Mwanuke, Augustine Okrah, Nelson Okwa, Ismail Sawadogo na Victor Akpan, huku wengine wakijadiliwa akiwemo Erasto Nyoni na Peter Banda.
Chanzo: Dar24
Post a Comment