Baada ya tambo za takribani wiki nzima, mzizi wa fitna unakwenda kukatwa pale uwanja wa Benjamin Mkapa leowakati watani Simba na Yanga watakapoumana kwenye mchezo wa ligi kuu ya NBC
Mchezo huo una umuhimu wa kipekee kwa kila timu na pengine hiyo inaweza kuwa sababu ya kuongeza ushindani
Simba wakiwa wenyeji wa mchezo huo, itakuwa rasmi wameondoka katika mbio za ubingwa kama watapoteza
Ushindi kwao hautamaanisha wamerejea katika mbio za ubingwa kwa asilimia 100 pia kwani bado watakuwa na deni la alama tano dhidi ya Yanga
Ili waweze kuwa mabingwa watalazimika kuiombea Yanga mabaya katika mechi nne zitakazokuwa zimesalia huku wao wakitakiwa kushinda mechi zote
Kwa Yanga ushindi dhidi ya Simba leo utawapa uhakika wa kutetea ubingwa wao kwa msimu wa pili mfululizo
Kama Yanga itashinda leo, itahitaji alama mbili tu kutoka mechi nne zitakazokuwa zimesalia ili kurejesha ubingwa Jangwani kwa mara ya 29
Wakati Simba wakiwa na mabadiliko katika benchi lao la ufundi, Yanga wanakwenda kucheza dabi ya 9 wakiwa na Kocha Nasreddine Nabi
Takwimu zinaibeba Yanga katika mchezo huo kwani mara ya mwisho kupoteza mchezo wa ligi dhidi ya Simba ni miaka mitatu iliyopita
Nabi amekuwa mbabe wa dabi kwani katika mechi nane alizoiongoza Yanga, ameshinda nne, katoka sare tatu na kupoteza mchezo mmoja
Je leo ataendeleza ubabe wake dhidi ya Simba? Mtanange utapigwa kuanzia saa 11 jioni
Vita kubwa inatarajiwa kushuhudiwa kati ya washambuliaji Wacongoman Fiston Mayele wa Yanga na Jean Baleke wa Simba
Baleke amekuwa katika kiwango bora cha kupachika mabao, akifunga mabao saba katika mechi tano za ligi kuu alizocheza tangu alipojiunga na Simba
Hii itakuwa mechi yake ya kwanza ya derby lakini amebeba matumaini makubwa ya Wanasimba kutokana na form aliyonayo
Mayele ndiye kinara wa mabao katika ligi kuu, akifunga mabao 16. Hii itakuwa mechi yake ya saba ya derby akiwa amefunga mabao matatu katika mechi sita alizokutana na Simba
Safu ya ushambuliaji ya Simba inaonekana kuwa hatari zaidi baada ya ongezeko la Saido Ntibazonkiza ambaye anashirikiana vyema na Baleke na Clatous Chama kinara wa pasi za mabao
Hata hivyo Yanga wanajivunia ukuta imara wakiwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi kwenye ligi msimu huu
Yanga wameonyesha wana uwezo wa kulinda ushindi hata wa bao moja kwa dakika 90 lakini ni tofauti kwa watani zao Simba
Katika mechi mbili zilizopita kwenye derby, Simba ilitangulia kufunga lakini ikapoteza moja na kutoka sare moja baada ya dakika 90
Matumaini ya mashabiki ni kuwa watashuhudia mechi nzuri yenye ushindani wa aina yake siku ya leo
Post a Comment