Msimamo wa ligi kuu Tanzania Bonyaza HAPA
Saa 24, tangu tiketi za mchezo wa Simba na Wydad Casablanca sambamba na ule wa Raja Casablanca na Al Ahly ziwekwe sokoni, tiketi hizo zimeuzwa zote huku mashabiki wakitakiwa kulipa Sh 160,000 ili kumwona Jean Baleke akiwa uwanjani.
Michezo hiyo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa inatarajiwa kupigwa wikiendi hii na mwakilishi wa Tanzania, Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Mohammed IV, Ijumaa Aprili 27, kuivaa Wydad huku Raja ikivaana na Al Ahly Aprili 29, kwenye uwanja huo huo.
Kiingilio cha chini cha mchezo kati ya Wydad na Simba ambayo ina mastaa wakubwa, Clatous Chama na Jean Baleke wenye mabao manne kila mmoja kwenye michuano hiyo, ni Dirham 30, sawa na Sh6,000 za Kitanzania, huku kiingilio cha juu ni Dirham 700 (Sh160,000).
Kwa upande wa mechi ya Raja na Al Ahly kiingilio cha chini ni Dirham 50 (Sh11,100), huku cha juu ni Dirham 500 (Sh115,000).
Tiketi hizi zilikuwa zikiuzwa mtandaoni kuanzia Aprili 23 na ilipofika Aprili 24, ziliisha na mamlaka kutangaza, hata hivyo kwenye mchezo wa nyumbani wa Simba dhidi ya Wydad, kiingilio cha juu kinachojulikana kwa jina la Platnium hakikuwa tofauti sana na hiki kwani ilikuwa Sh150,000.
Uwanja wa Mohammed IV utakaotumika kwa michezo yote miwili unaripotiwa kuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki wasiopungua 45,891 hadi 50,000.
Moja ya silaha kubwa za Raja na Wydad ni mashabiki wao wanaojitokeza kwa wingi hususan kwenye mechi muhimu kama hizo na hushangilia kwa nguvu zote kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo bila kujali matokeo.
Simba inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na faida ya bao moja ililolipata kwenye mchezo wa kwanza Kwa Mkapa ikishinda 1-0 na mashabiki wa Wydad walianza kuhimizana mapema kuingia kwa wingi kwa kuwa wameanza kupata hofu ya Simba kutokana na kiwango walichoonyesha.
Al Ahly yenyewe inaingia ikiwa na faida ya mabao mawili iliyoyapata ikiwa nyumbani kwenye ushindi wao wa mabao 2-0 lakini bado ngoma inatajwa kuwa ngumu kwa kuwa kuchomoka nchini Morocco linaonekana kuwa jambo gumu.
Chanzo: Mwanaspoti
Post a Comment