Wachezaji wa Simba SC wakiongozwa na Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke na Kiungo kutoka Zambia Clatous Chama wanahitaji ushindi wa aina yoyote leo Jumamosi (Machi 18) ili wapate bonasi ya Sh 250Mil walizowekewa na mabosi wa timu hiyo.
Simba leo Jumamosi wanatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kuvaana Mabingwa wa Soka nchini Guinea Horoya AC katika mchezo wa mzunguuko watano wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo, Simba SC wanahitaji ushindi wowote ili wajihakikishie kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mmoja wa mabosi wa Simba SC, kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la timu hiyo, amesema kuwa mabosi na wachezaji hao walikutana jana Ijumaa kufanya kikao sambamba na kula chakula cha jioni kambini kwao Mbweni nje kidogo ya Dar.
Bosi huyo amesema kuwa, kikao hicho kitakuwa cha kuwapa hamasa na morali kuelekea mchezo huo ili kuhakikisha wanapata ushindi na kujiweka katika nafasi nzuri.
Ameongeza kuwa wachezaji kwa pamoja chini ya Nahodha Mkuu wa timu hiyo, John Bocco wameahidi kupambana ili kufanikiwa malengo yao ya kufuzu Robo Fainali.
“Bodi ya Wakurugenzi kwa pamoja jana usiku walikutana na wachezaji na Benchi La Ufundi mara baada ya mazoezi ya jioni kwa ajili ya kufanya kikao kifupi kambini.”
“Kikao hicho maalum kwa ajili ya kuwapa hamasa pamoja na kuwapa ahadi ya bonasi ya Sh 250Mil watakazopewa kama wakifanikiwa kupata ushindi dhidi ya Horoya.”
“Fedha hizo ni tofauti na zile ambazo walizoahidiwa na na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan za kila bao Sh 5Mil atakazowapa baada ya kufunga bao,” amesema bosi huyo.
Akizungumzia hilo Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema: “Bonasi ipo kwa wachezaji katika kila mchezo ambayo inatofautiana na ukubwa wa mchezo.”
“Kuelekea mchezo wetu dhidi ya Horoya ni lazima iwepo utofauti ya Bonasi kwa wachezaji wetu, na hiyo ni kutokana na umuhimu wa mchezo huo,”
Post a Comment