KOCHA Mkuu wa kikosi cha Geita Gold, Fred Felix Minziro, ameweka wazi kuwa ni kweli kuna uwezekano mkubwa wakampoteza straika na nahodha wa kikosi chao, George Mpole ambaye anatajwa kupokea ofa kutoka klabu za Simba na Yanga.
Mpole amekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wako kwenye nafasi kubwa ya kuondoka ndani ya kikosi cha Geita Gold kutokana na uwezo mkubwa ambao ameuonyesha msimu huu akifanikiwa kuhusika katika mabao 21 katika michezo 30 ya Ligi Kuu aliyocheza msimu huu, akifunga mabao 17 na kuasisti mara nne.
Mpole ambaye alijiunga na Geita Gold akitokea Polisi Tanzania msimu uliopita, amesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja ndani ya kikosi cha Geita Gold, unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao, na tayari Simba na Yanga zimefanya mazungumzo naye huku pia akiwa na ofa kutoka nje ya nchi.
Akizungumza na Championi Ijumaa, kocha Minziro, alisema: “Ni jambo lililo wazi kuwa tuko katika nafasi kubwa ya kumpoteza Mpole kuelekea msimu ujao kutokana na kile ambacho amekionyesha msimu huu, tunatamani kubaki naye, nami binafsi nimefanya mazungumzo naye kuona uwezekano wa kumbakisha.
“Lakini kama mchezaji naye anatafuta maisha hivyo anaweza kufanya uchaguzi ambao anaona unamfaa, nasi tumejiandaa kwa chochote ambacho kitatokea.”
Stori: Joel Thomas
The post Kocha wa Geita Fred Felix Minziro Afunguka Mpole Kutua Simba, Yanga appeared first on Global Publishers.
Post a Comment