IMEFAHAMIKA kwamba, mshambuliaji mpya wa Yanga, Mzambia, Lazarous Kambole, ndani ya kikosi hicho alichosaini mkataba wa miaka miwili, atakuwa analipwa zaidi ya shilingi milioni 278.
Kambole amejiunga na Yanga akitokea Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini akiwa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake.
Mchezaji huyo ni wa kwanza kutambulishwa ndani ya Yanga kuelekea msimu ujao ambapo bado timu hiyo inaendelea kusaka majembe mengine ya kuimarisha kikosi chao.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa, mshambuliaji huyo amekubali kijiunga na timu hiyo baada ya kuwekewa ofa ya mshahara wa dola 5000 kwa mwezi ambazo ni sawa shilingi 11,619,200 za Kitanzania.
Akiwa amesaini mkataba wa miaka miwili, Kambole ndani ya mwaka mmoja wenye miezi 12, atakuwa akilipwa dola 60,000 sawa na shilingi 139,430,400 za Kitanzania.
Hivyo hadi mkataba wake wa sasa wa miaka miwili wenye miezi 24 ukimalizika, atakuwa jumla amelipwa dola 120,000 ambazo ni sawa na shilingi 278,860,800 za Kitanzania.
Ikumbukwe kuwa, msimu uliopita Yanga walimfuata mshambuliaji huyo kwa ajili ya kumsajili, lakini walishindwa kufikia muafaka kutokana na kuhitaji mshahara wa dola 10,000 sawa na shilingi 23,238,400 za Kitanzania, wakati Yanga walipanga kumpa mshahara wa dola 3500, sawa na shilingi 8,133,440 za Kitanzania.
NA IBRAHIM MUSSA
The post Mshambuliaji Mpya wa Yanga, Mzambia, Kambole Achota Milioni 278 Miaka Miwili appeared first on Global Publishers.
Post a Comment