Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amesema katika kipindi alichokuwa kazini amekutana na changamoto kadhaa, ikiwamo kifo cha Rais John Magufuli.
CDF Mabeyo alisema changamoto hiyo ilikuwa kubwa, lakini Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ ) lilisimama kidete kwa utulivu na kuhakikisha nchi inafuata misingi ya katiba.
Kauli hiyo kwa mara ya kwanza ameizungumza juzi usiku, katika mahojiano maalumu aliyoyafanya kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV.
“Ninyi ni mashuhuda tukampoteza Rais aliyekuwapo madarakani, lakini tulisimama kidete kwa utulivu mzuri kama jeshi tukitimiza wajibu wetu kwa mujibu wa Katiba,” alisema CDF Mobeyo.
“Tukampokea Rais Samia Suluhu Hassan na naamini tunaendelea vizuri mpaka sasa wananchi wako watulivu wanaendelea kufuata miongozo kama inavyotolewa na Serikali.”
CDF Mabeyo pia alizungumzia milima na mabonde katika safari yake ya uongozi wa jeshi hilo, akisema hali hiyo ipo na itaendelea kuwepo kulingana na kipindi kilichopo.
Katika wakati wa uongozi wake kulikuwa na mazingira tofauti kwa kuwa matishio ya usalama wa mipaka yanabadilika, hivyo ilikuwa changamoto kubwa.
“Nchi yetu inakabiliwa na viashiria fulani vya ugaidi na ujue viashiria hivi vinaleta matishio yasiyo na mipaka, adui haonekani waziwazi lakini tumeweza kushirikiana na wananchi vizuri,” alisema CDF Mobeyo.
“Kama mtakumbuka mwaka 2017 kulikuwa na mapango ya Amboni kule Tanga, baadaye ugaidi ukazuka Mwanza, ikafuatiwa na Kibiti ambako ilikuwa ni kama kitovu, lakini tukaendelea mpaka sasa tumehakikisha mpaka wetu upo vizuri.
“Ugaidi mtu anaweza kutumika bila hata yeye kujijua, tunashukuru Watanzania wengi wamekuwa wakishirikiana na Jeshi kutoa taarifa. Hatukuishia hapo tumeendelea kuwa msaada kwa majirani zetu kuhakikisha tunalinda amani, hasa katika ukanda huu wa SADC,” alisema.
Hata hivyo, mkuu huyo wa majeshi alisema hali kwa sasa ni nzuri na Jeshi lina vikosi ambavyo vimeendelea kulinda kwa kuwa baada ya kutoka Kibiti magaidi waliteremka Kusini Mtwara.
Alisema mpaka sasa hakuna changamoto ya kiusalama maeneo hayo na Jeshi limeendelea kushughulikia usalama wa kikanda huku mipaka yetu ikiwa salama.
“Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na katika majukumu ni kuhakikisha dunia inakuwa na amani, lazima tusaidie na tutaendelea kusaidia nchi nyingine katika ulinzi wa amani, ni jukumu ambalo haliepukiki na tunapata manufaa kwa kujifunza mambo mengi kitaaluma katika ustawi wa jamii, tunaneemeka mtu mmoja mmoja na Taifa,” alisema CDF Mobeyo.
Hata hivyo, alisema Tanzania haijawahi kuagiza wanajeshi waliokwenda kulinda amani warejee mpaka watakapomaliza jukumu na kila wakipoteza wanajeshi wamekuwa wakitoa taarifa kwa umma, “tukipoteza askari wetu huwa hatufichi, lazima taifa lijue.”
Post a Comment