Arusha. Wanafunzi wanaosoma kidato cha tano katika shule ya Sekondari Arusha Science iliyopo kata ya Laroi mkoani Arusha wametengeneza gari linalotumia mwanga wa jua (sola) ikiwa ni utekelezaji wa mafunzo kwa vitendo ambayo wamekuwa wakifundishwa shuleni hapo.
Gari hilo ambalo linatumia mwanga wa jua lina uwezo wa kutembea kilometa 160 likiwa na mzigo mwepesi baada ya hapo linahitaji kuchajiwa tena na tayari limeshatumia Sh3.5 milioni katika utengenezaji wake.
Walter Tairo (19) na mwenzake ni Glenyce Amani (17) ni miongoni mwa wanafunzi waliotengeneza gari hilo ambalo walianza mradi huo mwaka jana na kufanya hivyo ni kuweza kuonyesha kwa vitendo vile vyote wanavyofundishwa shuleni hapo .
Walter amesema gari hilo halitumii mafuta na linasaidia kuokoa gharama ambapo linatumia mwanga wa jua na ni miongoni mwa magari ambayo yanatunza mazingira kutokana na utengenezaji wake.
Glenyce amesema kuwa wanafunzi walioanzisha wazo la kutengeneza gari hilo wako sita
"Wanafunzi tulioleta wazo la kutengeneza gari hili tuko sita na wote ni kidato cha tano ambapo gari hili lina uwezo wa kusaidia shughuli mbalimbali shuleni hapa hata majumbani kwa ajili ya kubeba mizigo midogo midogo na linasaidia kutatua changamoto ndogondogo katika jamii "amesema Glenyce ambaye ni mwanafunzi wa kike.
Amesema kuwa muda mwingi wamekuwa wakifanya kwa vitendo yale wanayofundishwa ambapo kila mwanafunzi ana mradi wake anaoutekelza.
Mbali na ubunifu huo pia wanafunzi hao wameweza kubuni jokofu linalotumia sola.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo akizungumza katika mahafali ya kwanza ya kidato cha sita shuleni hapo, amesema elimu inayotolewa shuleni hapo ni ya kiwango cha juu huku ikizingatia masuala ya teknolojia na sayansi kwa vitendo tofauti na shule nyingi ambazo zimekuwa zikitegemea elimu ya nadharia.
Profesa Tumbo amesema kuwa, changamoto kubwa iliyopo ni wengi wa wanafunzi kuogopa kusoma masomo hayo wakati ndio yanauzika ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake mwanzilishi na Mkurugenzi wa shule hiyo, Profesa Nuhu Hatibu amesema wanafunzi hao walikaa pamoja na kuja na wazo la kutaka kutengeneza gari kutokana na masomo wanayofundishwa darasani, hivyo walivyoonyesha wazo lao tukawapa ushirikiano ikiwemo kuwanunulia vifaa walivyokuwa wakihitaji.
Profesa Nuhu amesema kila mwanafunzi shuleni hapo anakuka na wazo la kuanzisha mradi wake ndipo shule inawasaidia kuendeleza kama walivyofanya hao vijana wa kutengeneza hilo gari.
"Kwa kweli vijana hawa wameonyesha ubunifu wa hali ya juu, sisi wenyewe tumefurahi kupata wanafunzi wenye uelewa mkubwa kaisi hiki wa kutengeneza gari na sisi tunaahidi kuwasaidia hadi watimize malengo yao kwani ndio ndoto kubwa ya shule yetu"amesema Profesa Nuhu
Profesa Nuhu amesema kuwa wanajikita kwenye vitendo zaidi badala ya elimu ya darasani ili kuwawezesha wahitimu kujiajiri badala ya kwenda kukaa mtaani na kutafuta ajira.
Amesema kuwa malengo yake makuu ya shule hiyo ni kuwa shule bora Afrika ambayo itatoa wataalamu wabobezi wa maswala ya sayansi na kuweza kuwaandaa kuwa wabunifu na wajasiriamali ambapo hadi sasa hivi wamekwisha kupokea bunifu 27 zinazofanywa na wanafunzi hao, huku bunifu 10 zikikamilika kwa asilimia 100 na miradi hiyo inatumika hapo shuleni.
Post a Comment