Viongozi 20 Chadema Waachiwa Kwa Dhamana



Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Taifa (Bavicha), John Pambalu (watatu kulia) na Katibu Mwenezi Bavicha, Twaha Mwaipaya wapili (kushoto) wakiwa kwenye kijiwe cha kahawa na baadhi ya wakazi wa mjini Babati mkoani Manyara kwenye kampeni yao ya 'Join The Chain' kabla ya kukamatwa na Polisi.
Babati. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) John Pambalu, Katibu Mwenezi, Twaha Mwaipaya pamoja na viongozi wengine 18 wa Chama hicho Wilaya ya Babati mkoani Manyara waliokuwa wamekamatwa na Jeshi la Polisi wilayani humo wameachiwa kwa dhamana.

Viongozi hao walikamatwa leo Jumatano Mei 25, 2022 wakidaiwa kufanya mikutano kwenye vijiwe mjini Babati wakitoa elimu ya kudai Katiba mpya.

Akizungumza na Mwananchi leo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa Manyara, Benjamin Kuzaga amethibitisha kuachiwa viongozi hao.

Amesema kuwa “Wamepewa dhamana” amejibu Kamanda Kuzaga kwa ujumbe mfupi kupitia WhatsApp.


Hata hivyo, alipotumiwa ujumbe kuulizwa sababu za viongozi hao kukamatwa, Kamanda Kuzaga hakujibu ujumbe huo.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Babati, Edgar Mwageni amesema viongozi hao walikamatwa wakiwa wanazunguka kuzungumza na baadhi ya wanachama wao mjini Babati wakihamasisha juu ya kampeni yao ya kitaifa ya chama hicho ya "Join the Chain".

Mwegeni amesema jana Jumanne walikaa kikao cha ndani katika Ukumbi wa AVIT mtaa wa mji mpya na kuzungumza juu ya umuhimu wa Katiba mpya bila usumbufu wowote.

"Haijulikani ni sababu ipi ilisababisha maofisa hao kukamatwa lakini huenda walikamatwa kwa sababu ya mkusanyiko usiokuwa na kibalii," amesema.





0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post