Timu ya Ihefu Kitoka Mbeya yarejea Tena Ligi Kuu, Katwila aweka heshima



RASMI! Ndivyo unaweza kusema kuelezea kurejea tena kwa Ihefu Ligi Kuu baada ya leo kuizamisha Pan African 1-0 katika mchezo wa Championship uliopigwa uwanja wa Highland Estate wilayani Mbarali mkoani hapa.

Ihefu iliyoshuka daraja msimu uliopita, leo ilihitaji ushindi haswa ili kujihakikishia zaidi kurudi Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 65 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wao, Kitayosce waliposhinda leo na kufikisha alama 60 na kubakiza mechi moja kila timu.

Kwa matokeo hayo vijana hao wa mkoani hapa wanaungana na vinara DTB waliotangulia Ligi Kuu wiki iliyopita na sasa msimu ujao zitaungana na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga.

Katika mchezo wa leo wenyeji walisubiri hadi dakika 69 walipopata bao kupitia kwa Isah Ngoah baada ya wapinzani kuwakazia dakika 45 za kwanza kwa kwenda mapumziko kwa suluhu.


Akizungumza na Mwanaspoti Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zuberi Katwila amesema matokeo hayo ni juhudi za timu kwa ujumla, huku akiwapongeza nyota wake kwa kuwa wavumilivu tangu waliposhuka daraja hadi leo wanarejea tena.

Amesema wapo wachezaji ambao walipata ofa baada ya timu kushuka lakini aliwaomba kutogawanyika lakini hata dirisha dogo hakutaka kuongeza wachezaji wengi alipowaleta watatu pekee.

“Kila mmoja ana mchango wake kwenye timu, vijana wamepambana, mashabiki, uongozi na benchi la ufundi, kila mmoja amehusika katika nafasi yake, kuna ambao walitaka kuondoka baada ya kushuka daraja lakini niliwaomba tubaki, hii ni heshima,” amesema Katwila.


Kupanda kwa Ihefu kutafanya msimu ujao Mkoa wa Mbeya kuwa na timu nne za Ligi Kuu kama Mbeya City, Prisons na Mbeya Kwanza zitaweza kupambana kubaki katika mashindano hayo.



0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post