Dahh Maskini Kocha Pablo Abariki Kipigo Kitakatifu Cha Yanga...Inauma



WAMETUZIDI! Ni kauli ya Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco akikiri wapinzani wao, Yanga wamekuwa bora kuliko vijana wake hasa dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Licha ya kukiri kuzidiwa na Yanga hasa eneo la kati, Pablo amesema kikosi chake kimefanya jitihada mbalimbali za kusawazisha na kupata ushindi ikiwemo kufanya mabadiliko ya wachezaji lakini haikufua dafu na kujikuta wakiwa na siku mbaya kazini.

Mbali na hilo Pablo amelia na majeruhi ndani ya kikosi chake ambayo yamesababishwa na idadi kubwa ya mechi za mfululizo na hali ya hewa.

Katika mchezo huo Simba imewakosa wachezaji muhimu Clatous Chama, Jonas Mkude, Peter Banda, Aishi Manula, Israel Patrick, John Bocco, Paschal Wawa na Shomari Kapombe.


Pablo amesema kukosekana kwa wachezaji wake hao kutokana na kuandamwa na majeraha ni miongoni mwa sababu za kikosi chake kushindwa leo kumfunga mtani wake na kutinga fainali.

"Walikuwa bora kwa dakika 45 za kwanza na wamecheza vizuri zaidi yetu, tumejaribu kubadilika na kurudi mchezoni kipindi cha pili lakini ni kama pia hatukuwa na bahati tumekosa bao dakika za mwisho mpira ukigonga mwamba,". amesema na kuongeza;

"Ni kweli tuna majeruhi wengi kwenye timu wengine walikuwa sehemu ya mchezo lakini dakika za mwisho wamekosekana, kuwa na majeruhi wengi kikosini kunaletwa na sababu nyingi sana mfano mfululizo wa mechi unaoleta uchovu lakini pia hali ya hewa,".


Simba imeng'olewa kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam baada ya kufungwa bao 1-0 na Yanga katika mchezo ambao umepigwa leo saa 9:30 alasiri kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.




0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post